Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kutembelea “Mlima wa Moto”

Kutembelea “Mlima wa Moto”

Kutembelea “Mlima wa Moto”

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI ITALIA

NI SEHEMU chache ambapo unaweza kuona mandhari yenye kuvutia sana ya volkano ileile iwe uko mashambani, ufuoni, au jijini. Ikiwa jiji hilo ni Catania, basi unatazama Mlima Etna, wenye urefu wa zaidi ya meta 3,300 ulio sehemu ya kaskazini ya pwani ya mashariki ya Sicily, na ambao ndio mlima mrefu zaidi wenye volkano hai barani Ulaya.

Volkano Ambayo Imechunguzwa kwa Muda Mrefu

Waarabu waliotawala Sicily kwa muda mrefu waliita volkano hiyo Mlima wa Moto, na bila shaka jina hilo linafaa Etna kwa sababu mara kwa mara mlima huo umekuwa ukitokeza lava moto sana kutoka kwenye kina chake. Utendaji wa Mlima Etna unathibitishwa na maandishi ya Pindar na Aeschylus ambao walieleza mlipuko uliotokea 475 K.W.K. Zaidi ya mara moja, lava yenye moto imefanyiza kwa njia ya ajabu kijia chembamba kutoka mlimani na kuingia baharini. Milipuko hiyo ilitukia mnamo 396 K.W.K., 1329 W.K., na 1669 W.K. Mlipuko wa 1669 W.K. ndio unaojulikana zaidi kati ya ile ya “kisasa.” Wakati huo, ukanda mrefu wa lava wenye upana wa kilometa mbili hivi na urefu wa kilometa 25 ulitiririka na kufunika kuta za jiji la Catania, ukaharibu kabisa nyumba za watu zaidi ya 27,000, na kukaribia kujaza bandari ya jiji hilo.

Inafikiriwa kwamba utendaji wa volkano hiyo uliongezeka katika karne ya 20, kwani volkano hiyo imelipuka mara kadhaa. Mnamo 1928, mlipuko mkubwa zaidi uliharibu kijiji cha Mascali. Katika miaka michache iliyopita, wenyeji wa eneo hilo wamekuwa wakitatizwa na kuhangaishwa na milipuko ya lava na jivu.

Historia ya “Mama Mkubwa”

Inadaiwa kwamba Mlima Etna ulianza kufanyizwa miaka 170,000 iliyopita kutokana na milipuko ya magma, au miamba iliyoyeyuka. Volkano ndogo zipatazo 250 zenye umbo la pia zilizo kandokando ya volkano kuu, zilitokea nyakati mbalimbali ambapo volkano hiyo ililipuka. Volkano hizo huonekana kama watoto wanaomzunguka mama yao, na kwa sababu hiyo volkano hiyo ilipewa jina la utani Mama Mkubwa.

Ukisafiri kwa gari au kwa gari-moshi kuona mandhari ya Mlima Etna, utaona mandhari mbalimbali maridadi. Mandhari hizo ni kama vile Monti Rossi (Milima Myekundu) karibu na Nicolosi, Mashimo ya Silvestri, na bonde kubwa la Valle del Bove (Bonde la Fahali), ambayo yanaweza kuonekana kutoka Giarre na Zafferana.

Ingawa watu hawajaelewa kabisa jinsi volkano hiyo ilivyotokea, ni ya zamani sana. Miamba iliyoyeyuka ilipolipuka chini ya bahari na katika sehemu za pwani, ilitokeza pwani iliyo kaskazini ya Catania. Sehemu fulani ya pwani hiyo inajulikana kama Riviera dei Ciclopi au Pwani ya Mazimwi, yenye majabali meusi ya lava. Mbele tu ya jabali huko Aci Trezza, kuna miamba yenye maumbo ya ajabu, inayoitwa Faraglioni ambayo inaibuka kutoka baharini.

Unapendwa Isivyo Kawaida

Huenda ukashangaa iwapo watu wanaoishi chini ya volkano hiyo huogopa kwamba italipuka wakati wowote. Mlima Etna unapotulia, wenyeji wa eneo hilo husahau kwamba volkano hiyo ipo. Mwandishi Mfaransa Guy de Maupassant wa karne ya 19 aliandika hivi katika kitabu Journey to Sicily: “Jitu limetulia. Limelala pale mbali.” Mlima huo unapoanza kutoa moshi huenda wenyeji wakautazama kwa muda mfupi. Hata hivyo, mambo hubadilika wanaposikia mngurumo usiku wa manane, na kuona sehemu ya nje ya nyumba zao na barabara zikiwa zimefunikwa kwa jivu, au pua na macho yao yakiwa yamejaa jivu. Kwa hekima, wakati huo wao huuogopa Mlima Etna, hasa wanapoona mto mwekundu wa lava ukitiririka kutoka mlimani na kuharibu kila kitu njiani.

Licha ya hayo, watu wanaoishi katika eneo hilo huona Mlima Etna kuwa “jitu lenye urafiki.” Ukweli ni kwamba ingawa umesababisha madhara makubwa, yaani, kuharibu miji, mazao, na hivi karibuni zaidi, umeharibu sehemu wanazotembelea watalii, mlima huo umeua watu wachache sana. Baada ya milipuko hiyo kuharibu kazi ambazo watu walikuwa wamefanya, wenyeji hao wenye bidii huanza maisha upya.

Mshairi Mwitaliano Giacomo Leopardi alifafanua vizuri jinsi watu walioishi karibu na mlima huo walivyopenda mashamba yao. Aliwafananisha watu hao na mretemu, kichaka ambacho mara nyingi hukua katika maeneo ya volkano. Maua yake ya manjano ni maridadi nayo hung’aa. Hayo husimama wima na kubaki hivyo hadi lava inapotiririka na kuyafunika. Mara tu mlipuko unapokwisha na mwamba kupoa, mretemu huanza kukua tena, ukiwa imara na wenye nguvu, na kuchanua tena maua licha ya hali ngumu!

Mlima Etna Unabadilika

Kwa maoni ya wataalamu wa milima ya volkano, hilo “jitu lenye urafiki” linaonekana kuwa linabadilika. Mlima Etna haujalipuka hivi karibuni, lakini sasa, linasema gazeti Focus, “mlima wenye volkano ambao tumeuona ukiwa na utendaji fulani lakini si hatari unaanza kushukiwa.” Kulingana na onyo lilitolewa na watafiti Wafaransa na Waitaliano, Mlima Etna “unabadilika polepole kutoka kuwa volkano inayovuja, yaani, volkano inayotoa lava na gesi polepole, na kuwa volkano inayolipuka kwa fujo.” Kwa hiyo, Paola Del Carlo, mtafiti katika Taasisi ya Kitaifa ya Italia ya Jiofizikia na Volkano ya Catania, anasema kwamba “katika miaka 30 iliyopita, bila shaka utendaji [wa volkano hiyo] inayovuja na kulipuka umeongezeka, na ni vigumu kutabiri kwa usahihi kitakachotukia wakati ujao.”

Uzuri Usio na Kifani

Licha ya kutisha na kuogopesha, Mlima Etna una uzuri usio na kifani. Unapofunikwa na theluji wakati wa majira ya baridi kali au kuwa na rangi ya kahawia wakati wa kiangazi, au unapoutazama kutoka pwani, au unapotikisa dunia na kuwaogopesha watu, au unapolipuka usiku, volkano hiyo huthibitisha nguvu za Yule aliyeuumba. (Zaburi 65:6; 95:3, 4) Ukipata nafasi ya kutembelea jiji maridadi la Sicily, usisahau kutembelea Mlima Etna. Utauona kwa mbali ukitoa moshi wake daima. “Usiwe na wasiwasi ukisikia mngurumo,” ndivyo wenyeji husema. “Hivyo ndivyo Mlima Etna huwasalimu watu.”

[Ramani katika ukurasa wa 15]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

ITALIA

SICILY

Ml. Etna

[Picha katika ukurasa wa 14]

Mchoro wa Mlima Etna wa 1843

[Hisani]

Culver Pictures

[Picha katika ukurasa wa 15]

Julai 26, 2001

[Picha katika ukurasa wa 15]

Julai 28, 2001, Catania ikiwa nyuma yake

[Picha katika ukurasa wa 15]

Oktoba 30, 2002

[Picha katika ukurasa wa 15]

Septemba 12, 2004

[Picha katika ukurasa wa 16]

Miamba yenye maumbo ya ajabu, inayoitwa Faraglioni

[Picha katika ukurasa wa 17]

Wenyeji huuita Mlima Etna “jitu lenye urafiki”

[Picha katika ukurasa wa 15]

All photos: © Tom Pfieffer; map: Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.

[Picha katika ukurasa wa 16]

Background: © WOLFGANG KAEHLER 2005, www.wkaehlerphoto.com; Faraglioni: Dennis Thompson/Unicorn Stock Photos;