Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Wasafishaji Wenye Kushangaza wa Baharini

Wasafishaji Wenye Kushangaza wa Baharini

Wasafishaji Wenye Kushangaza wa Baharini

Na mwandishi wa Amkeni! nchini Fiji

Wao “husonga polepole kwenye matope yaliyo katika sakafu ya bahari. Wako kila mahali, kuanzia maeneo ambako mikondo yenye nguvu hukutana na ile isiyo na nguvu hadi sehemu zenye kina kirefu zaidi za bahari. Kama kikundi cha kongoni wadogo wanaotembea polepole chini ya bahari, wao hula chembechembe ambazo hutiririka kutoka juu ya bahari.”—Philip Lambert, msimamizi wa Jumba la Makumbusho la Kifalme la British Columbia.

HUENDA ukashangaa kusikia kwamba mtu anaweza kusema kwa njia ya kishairi kuhusu mbilimbibahari wa kawaida tu. Kwani, mnyama huyo amefafanuliwa kuwa “aina fulani ya soseji ya mpira isiyo na kichwa.” Je, mbilimbibahari ana umbo tata zaidi kuliko inavyoonekana?

Wao Hutimiza Mengi

Inasemekana kwamba mbilimbibahari ni wa jamii moja na kiti cha pweza na nyamizi. Ingawa wanaonekana kama konokono, wao ni tofauti sana na konokono wa baharini, ambao hawana magamba. Kufikia sasa, zaidi ya jamii 1,100 za viumbe hao zimepatikana. Wengi wao, kutia ndani wale wanaoweza kuliwa, wana ngozi laini. Wengine ni maridadi sana. Jamii nyingi za mbilimbibahari zina ngozi yenye vitu kama vipele ambavyo hufanya zifanane na tango zilizo na vipele.

Mbilimbibahari wengine ni wadogo sana hali wengine wanaweza kufikia urefu wa meta tano. Hata hivyo, wengi wao, wana urefu wa sentimeta 10 hadi 30. Inakadiriwa kwamba mbilimbibahari hufanyiza zaidi ya asilimia 90 ya viumbe wote wanaoishi katika kina cha meta 8,000, na hilo hufanya wawe viumbe wanaopatikana kwa wingi zaidi katika mitaro fulani ya bahari. Ingawa wengi wao huishi kwenye sakafu ya bahari, jamii chache zinazoishi ndani ya maji yenye kina kirefu zinaweza kuogelea.

Mbilimbibahari hupatikana katika bahari zote ulimwenguni nao hula mchanganyiko wa matope. Kama vikundi vya wasafishaji, viumbe hao husafisha matope na vitu vilivyooza kwenye sakafu ya bahari kwa kumeza kiasi kikubwa cha takataka hizo, kuchuja vitu hivyo, na kuacha mchanga ukiwa safi. Mbilimbibahari 2,000 hivi wanaweza kuishi katika ekari moja ya matumbawe.

Chakula cha mbilimbibahari kinatia ndani viumbe wadogo sana na changarawe iliyo kwenye sakafu ya bahari au ile inayopita katika mikondo. Viumbe hao wana minyiri 30 hivi inayofanana na manyoya ambayo ina ncha za pekee zenye hisi zinazotumiwa kutambua na kukamata chakula. Kisha mbilimbibahari “hulamba” mnyiri mmoja baada ya mwingine kabla ya kuendelea kutafuta chakula.

Aina fulani za mbilimbibahari huwa kama “wakaribishaji” nao huwakaribisha “wageni.” “Wageni” hao ni samaki na viumbe wengine ambao huishi katika utumbo wa mkaribishaji nao hutoka usiku ili kutafuta chakula. Wao hutia ndani jamii 27 za samaki anayeitwa pearlfish, wa jamii ya Carapidae. Wanapotishwa, wao hukimbilia mahali pao pa kujificha. Nyakati nyingine wao hula viungo vya uzazi na vya kupumua vya mkaribishaji wao. Hata hivyo, hilo halimdhuru mkaribishaji kwa kuwa mbilimbibahari anaweza kutengeneza upya tishu zilizoliwa.

Hutumia Mbinu Mbalimbali Anapotishwa

Bila shaka unapaswa kuwatazama kwa makini mbilimbibahari utakapowaona tena unapotembea baharini. Lakini uwe mwangalifu! Wanapotishwa, wasafishaji hao wa baharini wana mbinu nyingi za ajabu za kujikinga. Kwa mfano, wengine hutoa nyuzi nyingi ndefu zenye kunata ambazo huwanasa au kuwakengeusha wavamizi. Nyuzi hizo zenye kunata hukauka na kuwa ngumu haraka, na hilo humlazimisha mtu aliyenaswa kunyoa nywele zozote ambazo zimeguswa na nyuzi hizo.

Mbilimbibahari wengine hutokeza sumu ya aina fulani inayoitwa holothurin. Sumu hiyo huua samaki wa aina nyingi. Ingawa ni hatari kwa macho na huenda ikafanya ngozi iwashe, inaonekana kwamba si hatari kwa wanadamu. Kwa miaka mingi, wakazi wa kisiwani wameitumia kutia sumu, kuua, au kuduwaza samaki ambao wataliwa, na pia inafaa kwa kuwafukuza papa. Utafiti unaonyesha kwamba huenda sumu za mbilimbibahari zikatumiwa kutengeneza dawa ya kutibu kansa na maambukizo. Vitu mbalimbali kutoka kwa mbilimbibahari vimetumiwa na matabibu wanaotumia mbinu zisizo za kawaida kutibu yabisi-kavu, kuunganisha gegedu zilizokatika, na kupunguza shinikizo la damu. Viumbe hao pia hutumiwa kutokeza vitamini na madini.

Lakini mbilimbibahari ana mbinu moja zaidi ambayo yeye hutumia tu katika hali hatari sana, mbinu isiyo ya kawaida ya kujihami. Unapojaribu kumsogeza, mbilimbibahari hupasua mbavu zake na kutoa matumbo. Kwa kushtushwa na jambo hilo, huenda ukajiuliza ulimfanyia nini kiumbe huyo maskini ili afe kwa njia hiyo! Lakini usiwe na wasiwasi. Huenda hukumwua. Badala yake, ulishuhudia mbinu ya ajabu ya kujilinda. Kiumbe huyo sugu atapata viungo vingine vipya baada ya majuma machache!

Bado Anahitajika

Kazi ya kuvua mbilimbibahari ambayo imefanywa kwa miaka mingi, ingali inaendelea katika bahari zenye hali ya joto ya kadiri na za tropiki. Bila shaka, wapiga-mbizi fulani huhatarisha maisha yao ili kuvua mbilimbibahari wengi zaidi. Sehemu kubwa ya bidhaa hizo zitasafirishwa hadi China na sehemu nyingine za Mashariki, jinsi ambavyo imekuwa kwa karne nyingi. Utayarishaji wa mbilimbibahari waliokaushwa hutia ndani kuwachemsha katika maji yenye chumvi na kutoa matumbo, kuwakausha kwa moshi na kwa jua ili wauzwe. Leo, kuna mbilimbibahari ambao huuzwa wakiwa wamegandishwa.

Je, utawahi kula mbilimbibahari? Labda. Baada ya kupikwa, mbilimbibahari huwa kama jeli isiyo na rangi. Hutumiwa kuongeza ladha kwenye mchuzi na kuufanya uwe mzito. Nchini Fiji, aina mbalimbali za kienyeji hutengenezwa kwa kutumia tui ili kutokeza kitoweo kitamu chenye ladha ya samaki, na kinachotafunika.

Hata hivyo, viumbe hao wasioonekana ambao hutimiza mengi bila kelele si chakula kitamu tu. Kwa kweli, tunapaswa kuwashukuru mbilimbibahari kwa sababu ya kazi yao ya usafishaji ambayo hufanya bahari zetu ziwe safi. Wasafishaji hao wa bahari wenye kushangaza humsifu kimyakimya Yule aliyewaumba!—Zaburi 104:24, 25.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 24]

Mambo ya Pekee Kuhusu Mbilimbibahari

Mfumo wa kupumua wa mbilimbibahari hutofautiana sana na mifumo ya kawaida. Maji huvutwa kupitia utumbo, na oksijeni hufyonzwa kupitia kuta zilizo katika njia mbili za mfumo wa kupumua. Jamii fulani zinazoishi kwenye sakafu ya bahari hutumia mwili wao wote kuvuta oksijeni. Nyingine hata hupumua kupitia ngozi ya miguu yao.

▪ Mbilimbibahari wana vitu fulani kama mifupa ambavyo huwafanya waonekane kama tango. Vinapotazamwa katika darubini za elektroni, vitu hivyo vina maumbo ya ajabu ambayo huonekana kama misumari iliyojipinda iliyo kwenye ngozi zao. Kila jamii ya mbilimbibahari ina chembechembe hizo ndogo za kalisi kaboneti za kipekee na zilizo tata ambazo huzitofautisha na jamii nyingine.

▪ Mbilimbibahari hutumia nguvu za maji kusonga. Kiumbe huyo ana mamia ya mirija fulani iliyo kama miguu ambayo huongozwa na mfumo wa mifereji inayofanya mirija hiyo itende kwa upatano. Mifereji hiyo inapopanuka na kujifinya, maji husukumwa kwenye miguu ili kuipanua kwa njia inayofaa na kutokeza mwendo unaohitajika.

▪ Mayai ya mbilimbibahari hutungishwa nje ya mwili, na viinitete hupelekwa na maji hadi kwenye sakafu ya bahari. Hata hivyo, imeonekana kwamba mbilimbibahari wengine hutumia njia fulani zisizo za kawaida. Wao hujipasua kabisa, wakijigawanya katikati, katika sehemu mbili zinazotoshana. Kwa kushangaza, viungo vya mwili vilivyopasuka huanza kukua tena. Njia hiyo ya kujizalisha huhitaji tishu zipangwe kwa uangalifu sana katika kila moja ya sehemu zilizopasuka.

[Hisani]

From top to bottom: Courtesy Bruce Carlson, Georgia Aquarium; courtesy of UC Museum of Paleontology, www.ucmp.berkeley.edu; © Houseman/BIODIDAC; Ocean Sky Diving, Hong Kong

[Picha katika ukurasa wa 23]

Mbilimbibahari akitokeza nyuzi zinazonata ili kujilinda

[Picha katika ukurasa wa 23]

Mbilimbibahari walio na vipele

[Picha katika ukurasa wa 23]

Mbilimbibahari akiwa na mnyiri mmoja mdomoni

[Picha katika ukurasa wa 25]

Mbilimbibahari aliyepikwa kwa njia ya kienyeji kwa tui

[Picha katika ukurasa wa 22 zimeandaliwa na]

http://www.JohnHarveyPhoto.com

[Picha katika ukurasa wa 23 zimeandaliwa na]

Top inset: © David Wrobel/Visuals Unlimited; background: © Phillip Colla/SeaPics.com; bottom left: © Doug Perrine/SeaPics.com