Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Nyanya Hutumiwa Sana

Nyanya Hutumiwa Sana

 Nyanya Hutumiwa Sana

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UINGEREZA

WANAWAKE wa Italia hutumia nyanya sana katika upishi. Wapishi wengi ulimwenguni pote pia huona nyanya kuwa muhimu. Kwa kweli watu wa jamii mbalimbali hutumia nyanya sana. Watu walio na bustani nyumbani hukuza nyanya zaidi ya vyakula vingine. Lakini je, nyanya ni tunda au ni mboga?

Nyanya ni tunda kwani huwa na mbegu ndani yake. Hata hivyo, watu wengi husema kwamba nyanya ni mboga kwa kuwa huliwa pamoja na mlo mkuu. Historia ya nyanya inavutia sana.

Historia Yenye Kupendeza

Waazteki walikuza mnyanya kwa ajili ya chakula huko Mexico. Mashujaa Wahispania walipeleka mnyanya huko Hispania mwanzoni mwa karne ya 16, na waliuita tomate kutokana na neno tomatl la lugha ya Nahuatl. Muda si muda, Wahispania wanaoishi Italia, Afrika Kaskazini, na Mashariki ya Kati walianza kula nyanya.

Katika miaka ya baadaye ya karne hiyo, nyanya zilipelekwa Ulaya Kaskazini. Mwanzoni, watu walifikiri kwamba mnyanya una sumu na waliukuza ili kupamba bustani. Ingawa mnyanya ni wa jamii ya mtunguja, na una majani yaliyo na harufu kali na shina lenye sumu, iligunduliwa kwamba tunda lake halina madhara.

Yaelekea kwamba nyanya zilizopelekwa Ulaya zilikuwa za manjano kwani Waitaliano walipenda kuita nyanya pomodoro (tofaa la dhahabu). Waingereza walitumia jina tomate na baadaye wakaiita tomato, lakini pia walipenda kuita nyanya “tofaa la mapenzi.” Kisha nyanya zikasafirishwa kutoka Ulaya kupitia Bahari ya Atlantiki hadi Amerika Kaskazini, na hatimaye katika karne ya 19 zikawa chakula muhimu cha eneo hilo.

Zinapatikana kwa Wingi Nazo Hupendwa Sana

Mwulize mtu yeyote nyanya zina rangi gani, na kuna uwezekano mkubwa kwamba atakuambia ni “nyekundu.” Lakini je, ulijua kwamba kuna nyanya zenye rangi ya manjano, machungwa, waridi, zambarau, kahawia, nyeupe, kijani, au zenye milia? Nyanya nyingine hazina umbo la duara. Nyingine zina umbo la yai au la pea. Zinaweza kuwa ndogo kama njegere au kubwa kama ngumi.

Nyanya hukuzwa katika sehemu za mbali za kaskazini huko Iceland na sehemu za mbali za kusini huko New Zealand. Nchi zinazokuza nyanya kwa wingi ni Marekani na nchi zilizo kusini mwa Ulaya. Nchi zenye baridi kali hukuza nyanya katika vyumba vya pekee, na katika maeneo yenye ukame nyanya hukuzwa kwenye mchanganyiko wenye rutuba bila kutumia udongo.

Hata watu ambao hawana ustadi wa kutunza bustani hupenda kukuza nyanya. Ni rahisi kukuza nyanya, na mimea michache ya nyanya inatosha kulisha familia ndogo. Ikiwa hakuna nafasi ya kutosha, kuza minyanya inayoweza kupandwa katika vyombo vidogo.

Mapendekezo

Baridi huharibu ladha ya nyanya, kwa hiyo usiziweke ndani ya friji. Ukitaka ziwe mbivu haraka, unaweza kuziweka ndani ya bakuli pamoja na nyanya mbivu au ndizi mbivu, au uzitie ndani ya karatasi ya kahawia iliyofungwa na kuziacha humo kwa siku kadhaa, au unaweza kuziweka kando ya dirisha palipo na mwangaza wa jua.

Nyanya zinaweza kuboresha afya yako. Zina vitamini A, C, na E, kutia ndani potasiamu, kalisi, na madini ya chumvi. Watafiti wamegundua kwamba nyanya zina kiasi kikubwa cha lycopene, na inasemekana kwamba hiyo hupunguza uwezekano wa kupatwa na magonjwa fulani  kama kansa na ugonjwa wa moyo. Asilimia 93 hadi 95 ya nyanya imefanyizwa kwa maji, na hazina kalori nyingi. Hivyo, nyanya haziwezi kumnenepesha mtu.

Nyanya Ni Tamu na Zina Matumizi Mengi

Ukitaka kununua nyanya, utachagua za aina gani? Nyanya nyekundu zinazojulikana sana zinafaa kwa kutengeneza saladi na mchuzi. Huenda ukafurahia kula nyanya ndogo zenye rangi nyekundu, ya machungwa, au ya manjano zikiwa mbichi kwani zina sukari nyingi. Ikiwa unatayarisha piza au spageti, huenda ikafaa kutumia nyanya ngumu zenye umbo la yai. Nyanya fulani kubwa hujazwa ndani ya vyakula kabla ya kupikwa au kuokwa. Nyanya za kijani, ambazo nyakati nyingine huwa na milia, ni tamu zinapoliwa pamoja na chakula. Ladha na rangi ya nyanya huboresha na kufanya mboga, mayai, spageti, nyama, na samaki kuwa tamu. Ikiwa huwezi kupata nyanya zilizotoka tu kuchumwa, basi huenda ukapata nyanya za mkebe dukani.

Kila mpishi ana njia yake ya kutumia nyanya, lakini hapa pana mapendekezo unayoweza kutumia.

1. Katakata nyanya na uziweke juu ya vipande vya jibini na parachichi ili kutengeneza chakula kinachoamsha hamu ya kula. Nyunyiza mafuta ya mzeituni na pilipili manga, na utie majani ya mrehani.

2. Tayarisha saladi ya Kigiriki kwa kuchanganya vipande vikubwa vya nyanya, matango, jibini, zeituni mbivu, na vipande vya vitunguu. Koleza saladi hiyo kwa chumvi na pilipili, kisha uiandae pamoja na mchanganyiko wa mafuta ya mzeituni na maji ya limau.

3. Tayarisha mchuzi wa Kimeksiko kwa kukatakata nyanya, vitunguu, pilipili mbichi, na kitimiri, kisha uzichanganye na maji kidogo ya ndimu.

4. Tayarisha mchuzi wa nyanya ulio mtamu utakaoliwa kwa spageti kwa kutumia nyanya za mkebe zilizokatwa-katwa, sukari kidogo (au rojo ya nyanya), mafuta kidogo ya mzeituni, kitunguu-saumu kilichopondwa, kiasi kidogo cha majani kama vile mrehani, au kiungo kingine kinachofaa. Chemsha mchanganyiko huo kwa dakika 20 hivi mpaka mchuzi uwe mzito. Kisha uutie juu ya spageti zilizopikwa na kukaushwa.

Nyanya ni kati ya vyakula tofauti-tofauti vinavyopendeza vilivyoumbwa kwa ajili yetu.