Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kupata Chanzo cha Nishati Yote

Kupata Chanzo cha Nishati Yote

Kupata Chanzo cha Nishati Yote

JUA ndicho chanzo kikuu cha nishati inayotumiwa duniani. Wanasayansi wengi wanasema kwamba makaa ya mawe na mafuta yametokana na miti na mimea iliyooza ambayo hapo zamani ilipata nishati kutoka kwa jua. * Maji yanayotumiwa katika mabwawa ya kutokeza umeme huvutwa kutoka baharini na joto la jua kisha yanapelekwa juu ya nchi kavu yakiwa mawingu. Miale ya jua husukuma pepo ambazo huendesha jenereta. Hata hivyo, inakadiriwa kwamba nusu ya sehemu ya bilioni ya nishati inayotoka kwa jua ndiyo hufika duniani.

Ijapokuwa jua lina nishati nyingi sana, kuna mabilioni ya vyanzo vingine vikubwa vya nishati katika ulimwengu wote. Nishati yote hiyo hutoka wapi? Mwandikaji wa Biblia, Isaya, anasema hivi kuhusu nyota: “Inueni macho yenu juu, mwone. Ni nani ameviumba vitu hivi? Ni Yeye anayelileta jeshi lake kulingana na hesabu, ambaye zote anaziita kwa jina. Kutokana na wingi wa nguvu zenye msukumo, yeye pia akiwa hodari katika nguvu, hakuna hata moja kati ya hizo inayokosekana.”—Isaya 40:26.

Ijapokuwa sisi hustaajabia nishati nyingi sana ya nyota mbalimbali, sisi hustaajabu hata zaidi tunapomfikiria Muumba wa nyota hizo. Hata hivyo, Biblia hutuhimiza hivi: “Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi.” (Yakobo 4:8) Naam, Muumba wa dunia na vyanzo vingi vya nishati vinavyopatikana duniani, yeye aliyetupa sisi uhai, anaweza kupatikana na wale wanaomtafuta.—Mwanzo 2:7; Zaburi 36:9.

Huenda watu fulani wakashindwa kuamini kwamba Mungu anaijali dunia na wanadamu wanapoona dunia na mali zake za asili zikichafuliwa na kutumiwa kwa ubaguzi. Hata hivyo, Biblia inatuhakikishia kwamba hivi karibuni kutakuwa na badiliko kubwa kuhusu uongozi wa dunia na ugawanyaji wa mali za asili zilizomo duniani. (Danieli 2:44; Mathayo 6:9, 10) Kwa kusimamisha serikali moja ya mbinguni itakayotawala ulimwengu wote chini ya uongozi wa Mwana wake, Kristo Yesu, Yehova Mungu atahakikisha kwamba wanadamu wote wanafaidika na mali za asili zilizomo duniani bila ubaguzi. (Mika 4:2-4) Isitoshe, ‘atawaharibu wale wanaoiharibu dunia,’ yaani, wale wanaochafua mazingira ya dunia katika njia ya kiroho au ya kimwili.—Ufunuo 11:18.

Wakati huo, ahadi hii inayopatikana katika Isaya 40:29-31 itatimia kwa njia ya kiroho na ya kimwili: “Yeye anampa nguvu mtu aliyechoka; naye huzijaza nguvu kamili kwa mtu asiye na nguvu zenye msukumo. Wavulana watachoka na pia kuzimia, na vijana hakika watajikwaa, lakini wale wanaomtumaini Yehova watapata nguvu mpya. Wataruka juu kwa mabawa kama tai. Watakimbia wala hawatazimia; watatembea wala hawatachoka.” Ukijifunza Biblia, wewe pia unaweza kujua mengi zaidi kuhusu Chanzo cha nishati yote na kuhusu suluhisho la matatizo ya nishati yanayoikabili dunia.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 2 Ona sanduku “Mafuta Yalitoka Wapi?” katika gazeti la Amkeni! la Novemba 8, 2003.