Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Nishati Ni Muhimu kwa Uhai

Nishati Ni Muhimu kwa Uhai

Nishati Ni Muhimu kwa Uhai

MICAH alizaliwa mnamo Agosti 2003. Mama yake alipelekwa hospitalini kwa gari linalotumia petroli. Taa za hospitali ambamo alizaliwa ziliwashwa kwa umeme uliotoka kwenye kituo kinachotokeza umeme kwa makaa ya mawe. Mfumo unaotumia gesi ya asili ulitumiwa kupasha joto chumba ambamo alizaliwa. Iwapo mojawapo ya vyanzo hivyo vya nishati havingefanya kazi, uhai wa Micah ungekuwa hatarini.

Ulimwengu wa leo ambamo Micah alizaliwa unategemea vyanzo mbalimbali vya nishati. Kila siku sisi hutegemea vyanzo vya nishati kama vile mafuta, makaa ya mawe, na gesi ya asili kwa ajili ya usafiri tunapokwenda kazini, kupika, kuwasha taa, kupasha joto, na kufanya nyumba iwe baridi. Taasisi ya Mali za Asili za Ulimwengu inasema kwamba vyanzo hivyo vya nishati hutumiwa “kutosheleza asilimia 90 hivi ya mahitaji ya nishati katika biashara mbalimbali ulimwenguni.” Ripoti moja iliyochapishwa na Taasisi hiyo katika mwaka wa 2000 inasema: “Mafuta ndiyo hutosheleza mahitaji makubwa zaidi ya nishati ulimwenguni, yaani asilimia 40, kisha makaa ya mawe hutosheleza asilimia 26 na gesi ya asili hutosheleza asilimia 24 hivi.” *

Kulingana na jarida Bioscience, ‘kwa wastani, kila mwaka Mmarekani mmoja hutumia nishati inayolingana na lita 8000 za mafuta kwa matumizi yake yote yanayotia ndani usafiri na kupasha joto au baridi.’ Zaidi ya asilimia 75 ya nguvu za umeme ambazo hutumiwa huko Afrika Kusini, Australia, China, na Poland hutokezwa na mitambo inayoendeshwa kwa makaa ya mawe. Asilimia 60 ya umeme unaotumiwa nchini India na zaidi ya asilimia 50 ya umeme unaotumiwa huko Marekani na Ujerumani hutokezwa kwa makaa ya mawe.

Mwandishi wa habari anayeitwa Jeremiah Creedon anasema hivi katika makala yenye kichwa, “Jinsi Maisha Yatakavyokuwa Mafuta Yakiisha”: “Ni watu wachache tu wanaofahamu kwamba sasa mazao ya chakula yanayotokezwa ulimwenguni pote hutegemea mafuta. Leo, petroli na gesi ya asili ni muhimu sana katika hatua zote za kilimo, kuanzia hatua ya kutengeneza mbolea hadi ile ya usafirishaji wa mazao.” (Gazeti Utne Reader) Lakini vyanzo vya nishati vinavyoendeleza uhai wa wanadamu vinategemeka kadiri gani? Je, tunaweza kupata njia nyingine za kutokeza nishati bila kuchafua mazingira?

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 3 Ili upate habari zaidi kuhusu uchimbaji wa mafuta, ona gazeti la Amkeni! la Novemba 8, 2003, ukurasa wa 3-12.