Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kifaa cha Kuwafukuza Papa

Watu wengi huogopa kuogelea baharini kwa sababu wanaogopa kukutana na papa. Hata hivyo, kamati inayoshughulika na mambo yanayohusu papa huko Natal, Afrika Kusini, imebuni kifaa kinachowafukuza papa. Kamati hiyo iligundua kwamba “aina fulani ya mawimbi ya umeme huathiri vipokezi vya hisi vilivyo katika pua ya papa,” linaripoti gazeti Weekend Witness la KwaZulu-Natal. Kamati hiyo ilibuni kifaa ambacho humwathiri papa kadiri anavyokikaribia. Anaposhindwa kuvumilia hali hiyo, “papa hugeuka na kuelekea upande mwingine.” Kampuni fulani ya Australia hutengeneza kifaa kama hicho kwa ajili ya waogeleaji na watu wanaoteleza kwenye mawimbi. Mwogeleaji akifunga kifaa hicho kwenye mguu wake kinaweza kumlinda. Hata hivyo, watengenezaji wanasema: “Hatuwezi kuwa na uhakika kabisa kwamba kifaa hiki kitawaathiri papa kila mara.”

Sumu Huhatarisha Hasa Watu Wazima

Debra Kent wa Shirika la Habari Kuhusu Dawa za Kulevya na Sumu la British Columbia anasema kwamba “watu wanaposema kuhusu kuzuia vifo vinavyosababishwa na sumu, wao huwafikiria hasa watoto.” Hata hivyo, Kent anasema kwamba “hasa vijana wanaobalehe na watu wazima ndio hufa kutokana na kunywa sumu kimakosa.” Kulingana na gazeti The Vancouver Sun, watu wazima wengi hunywa sumu kimakosa “kwa sababu sumu hutiwa katika chombo kisichotiwa alama kama vile, chupa ya plastiki ya maji.” Visa vingine vingeepukwa ikiwa watu wangewasha taa na kusoma kilichoandikwa kwenye chombo kabla ya kunywa kilichomo. Kulingana na gazeti Sun, “sumu ndicho kisababishi kikuu cha nne kati ya visababishi 10 vikuu vya vifo miongoni mwa watu wazima.”

Je, Televisheni Inawadhuru Watoto?

Gazeti The Herald la Mexico City liliripoti hivi: “Watoto wachanga sana ambao hutazama televisheni hukabili tatizo kubwa zaidi la kukaza fikira wanapofikia umri wa kwenda shule.” Ripoti hiyo ilizungumzia uchunguzi uliochapwa katika jarida la kitiba Pediatrics kuhusu watoto 1,345, waliogawanywa katika vikundi viwili. Kikundi kimoja kilikuwa na watoto wenye umri wa mwaka mmoja na kile kingine kikiwa na watoto wenye umri wa miaka mitatu. Kulingana na uchunguzi huo, kila saa nzima ambayo mtoto hutumia kutazama televisheni kwa siku huongeza hatari ya kukabili tatizo la kukaza fikira kwa asilimia 10 anapofikia umri wa miaka saba. Watafiti hao wanasema kwamba “picha zinazosonga kwa mwendo wa kasi sana ambazo huonyeshwa katika vipindi vingi vya televisheni, zinaweza kuathiri ukuzi wa kawaida wa ubongo” wa watoto. Dakt. Dimitri Christakis mwanzilishi wa uchunguzi huo alisema hivi: “Ukweli ni kwamba kuna sababu nyingi za kuwazuia watoto kutazama televisheni. Uchunguzi mwingine umeonyesha kwamba [kutazama televisheni] kunawafanya wanenepe kupita kiasi na kuwa wenye jeuri.”

Kucheka Ni Dawa Nzuri

Gazeti UC Berkeley Wellness Letter linaripoti hivi: “Wataalamu wa Chuo Kikuu cha Stanford wanaochunguza mifumo ya neva wamegundua sababu inayofanya tuhisi vizuri tunapocheka. Walichunguza utendaji wa ubongo wa watu wanaopenda kusoma vitabu vya katuni zinazochekesha, nao wakagundua kwamba ucheshi na kucheka huchochea chembe fulani za ubongo,” ambazo pia huchochewa mtu anapotumia madawa fulani ya kulevya. Gazeti hilo linasema kwamba, “kucheka hupunguza mfadhaiko, hutuliza akili, na kumchangamsha mtu.” Kucheka pia hufanya mwili utoe homoni zaidi, hufanya moyo upige kasi zaidi, na huboresha kuzunguka kwa damu na muundo wa misuli. Gazeti hilo linasema: “Kwa kweli kucheka ni aina ya mazoezi. Hata hivyo, huwezi kuwa mwembamba kwa kucheka kupita kiasi kwani hutumii kalori kucheka.”

Mmea Unaofichua Mabomu Yaliyotegwa Ardhini

“Kampuni fulani nchini Denmark inayoshughulikia kubadilisha viungo, imebuni mmea ambao majani yake hubadilika kuwa mekundu unapokua juu ya mabomu yaliyozikwa ardhini,” linaripoti gazeti El País la Hispania. Mmea huo unaoweza kufichua mabomu, ambao unaitwa Arabidopsis thaliana, hubadilika rangi unapopandwa katika eneo lenye nitrojeni-dioksidi, ambayo ni “mojawapo ya kemikali zinazotumiwa zaidi kutengeneza mabomu,” linaeleza gazeti hilo. “Mizizi yake inapofyonza kemikali hiyo, mfululizo wa utendaji wa kemikali huanza na kufanya mmea huo utokeze rangi ya asili inayoitwa anthocyanin.” Simon Oostergaard, msimamizi wa kampuni fulani ya kisayansi anasema kwamba wanapanga “kupeleka mbegu za mmea huo kwenye sehemu zilizo na mabomu hayo, kuzieneza kwenye mashamba, wasubiri kwa majuma matano, halafu wategue mabomu hayo.” Oostergaard anasema kwamba ikiwa mmea huo utaweza kutumiwa katika sehemu nyingi ili kufichua mabomu, basi vifo vingi vitaepukwa kila mwaka. Mabomu milioni 100 hivi ya ardhini yalitegwa na kuachwa katika nchi 75 wakati wa vita vilivyopiganwa katika karne ya 20.

Ustadi wa Mbayuwayu wa Kufahamu Wanakoelekea

Gazeti The Sunday Telegraph la London linasema kwamba “mbayuwayu husafiri kwa zaidi ya kilometa 6,000 kutoka Afrika hadi Uingereza mwishoni mwa Aprili.” Ingawa hawana “mifumo ya kitekinolojia ya hali ya juu, wala vifaa vya kuongoza ndege au marubani,” wakati wa usiku wao husafiri juu kwenye urefu wa meta 3,000 kutoka kwenye ardhi kwa kutumia ustadi wa kujielekeza ulio bora zaidi ya ule wa ndege za kisasa. Ndege hao hubadili-badili wanakoelekea ili waepuke kupeperushwa na upepo. Zamani ilidhaniwa kwamba ndege hao husafiri kwa kutegemea ishara fulani ardhini lakini ikagunduliwa kwamba wao hutegemea upepo. Dakt. Johan Bäckman wa Chuo Kikuu cha Lund, nchini Sweden, ambaye alitumia rada kuwafuata ndege 225, anasema kwamba “hata ndege za kisasa, zilizo na vifaa bora zaidi vya kuziongoza, huenda zisiweze kutambua jinsi upepo unavyoelekea kama ndege hawa.” Inapendeza kwamba uchunguzi fulani umeonyesha kuwa nusu ya ubongo wa ndege hao huacha kufanya kazi wakati wanaporuka usiku. Lakini Graham Madge wa shirika la Royal Society for the Protection of Birds anasema kwamba bado kuna maswali yanayobaki. Kwa mfano, “Ndege hao hula nini wanaporuka?”

Vyoo Visivyovutia

Gazeti la Ufaransa linalochapishwa kila juma, L’Express, linasema kwamba wanafunzi wengi nchini Ufaransa hawatumii vyoo vya shule kwa kuwa “sakafu huwa zimejaa maji, maji ya mfereji huwa baridi sana, havina sabuni,” na vilevile wanafunzi hukosa faragha kwa kuwa “milango haifungiki vizuri” nazo “kuta huwa ndogo sana.” Uchunguzi uliofanywa na Fédération des conseils de parents d’élèves (Shirikisho la Mabaraza ya Wanafunzi na Wazazi), ulifunua kwamba “zaidi ya asilimia 48 ya wanafunzi hawatumii vyoo vya shule.” Hilo huwaletea watoto magonjwa mengi. Kulingana na uchunguzi huo, “robo moja ya wanafunzi wana matatizo ya tumbo na ya kukojoa.” Mtaalamu wa ugonjwa wa mfumo wa mkojo wa watoto, Michel Avérous, anasema: “Watoto wanapaswa kwenda chooni mara tano au sita kila siku. Mtoto asipokojoa mara nyingi inavyohitajiwa anaweza kupatwa na maambukizo yanayoathiri utendaji wa kawaida wa kibofu.”