Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Farasi Wanaocheza Dansi Baharini

Farasi Wanaocheza Dansi Baharini

Farasi Wanaocheza Dansi Baharini

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AUSTRALIA

WENZI wawili wanasalimiana kisha rangi yao inabadilika. Ni kana kwamba mwenzi wa kiume anaonyesha majivuno, huku mwenzi wa kike akimtazama na kumkubali. Wanakaribiana na kugusana kwa wororo, kisha wanakumbatiana kwa shauku. Jua la alfajiri linapowapiga, wao huanza kucheza mojawapo ya dansi za pekee za kiasili—dansi ya farasi-maji.

Dakt. Keith Martin-Smith ambaye ni mtaalamu wa mambo ya baharini anasema: “Farasi-maji wanavutia, ni wa pekee, na ni wenye madaha.” Hata hivyo, zamani watu walishangazwa na viumbe hao. Wataalamu wa maumbile wa kale waliwaita Hippocampus, ambalo pia lilikuwa jina la farasi wenye mikia ya samaki wanaosimuliwa katika hekaya. Inasemekana kwamba farasi hao walivuta gari la Poseidon, mungu wa bahari wa Wagiriki.

Inasemekana kwamba katika Zama za Kati wachuuzi waliwauza farasi-maji huku wakidai kwamba ni drakoni wachanga waliopumua moto. Lakini ukweli ni kwamba farasi-maji ni samaki wenye mifupa mingi ingawa hawafanani wala hawaogelei kama samaki wa kawaida. Kwa kuwa wao huelea majini bila kusonga mbali, imesemwa kwamba wao ni kama farasi waliotengenezwa kwa glasi au vidude vya kuchezea chesi vilivyo hai.

Farasi-maji hupatikana hasa katika maeneo mengi ya pwani yaliyo na maji yenye joto. Farasi-maji wana maumbo na ukubwa mbalimbali. Wataalamu wanakadiria kwamba huenda kuna jamii 33 hadi 70 hivi za farasi-maji. Jamii hizo zinatia ndani farasi-maji wa pygmy ambaye anaweza kutoshea kwenye ukucha wa kidole, na farasi-maji mwenye tumbo kubwa, ambaye anaweza kuwa na urefu wa zaidi ya sentimeta 30.

Hawana Matatizo Licha ya Kutokuwa na Meno na Tumbo!

Umbo la ajabu la farasi-maji huwafanya wasisonge kasi majini kwani wana kichwa kama cha farasi, mwili ulio na mifupa mingi, na mkia kama wa nyani. Wao hutumia muda mrefu wakiwa wamezungusha mikia yao kwenye mmea fulani huku wakila. Wanapotaka kusonga, pezi dogo la mgongoni huwasukuma polepole na mapezi ya kifuani huwaongoza. Kwa kudhibiti kiasi cha hewa kilichomo ndani ya kifuko chao cha hewa, wao hupanda na kushuka kama nyambizi.

Farasi-maji hupenda sana kula, naye hufyonza haraka uduvi au viumbe wengine wenye magamba wanaopita karibu naye kwa mdomo wake wenye mifupa mingi. Kwa kuwa farasi-maji hawana meno wala tumbo la kuwasaidia kumeng’enya chakula, ni lazima wale uduvi 50 hivi kila siku ili waendelee kuishi. Hilo si tatizo kwa wawindaji hao hodari, kwani uwezo wao wa kuona ni mzuri sana. Jicho moja linaweza kutazama mbele kutambua windo huku lile jingine likitazama nyuma. Wanaweza kuona rangi nyingi kuliko wanadamu na kuona vitu vingi zaidi kuliko samaki wengi.

Ni lazima farasi-maji wawe chonjo ili wasiliwe na viumbe wengine. Ili kuwaepuka viumbe wanaowawinda kama vile kaa au kasa, farasi-maji wengi wanaweza kujibadilisha wafanane na majani ya baharini, marijani, au mikoko. Kwa kuwa wana ngozi yenye madoadoa, sehemu za mwili zilizo kama magugu-maji, na uwezo wa kubadili rangi yao kupatana na mazingira, wao huweza kujificha kabisa wasionekane. Rudie Kuiter, ambaye ni mtafiti, anasema: “Wao hujipatanisha vizuri sana na mazingira hivi kwamba ili uwaone unahitaji kuwa makini sana.”

Dansi na Mahaba

Farasi-maji si kama samaki wengine wengi kwani wao huwa na mwenzi mmoja tu maishani na kwa kawaida wao huwa karibu-karibu. Kila asubuhi, wao hucheza dansi ya pekee ili kuimarisha uhusiano wao. Tracy Warland, ambaye hufuga farasi-maji, anasema: “Farasi-maji hucheza dansi kwa njia yenye kuvutia na kwa madaha sana hivi kwamba watu hufurahia kuwatazama.” Baada ya kucheza dansi, farasi-maji hao huenda kula siku nzima kwenye maeneo yao ya kawaida. Wao hucheza dansi ya ajabu zaidi wanapojamiiana. Farasi-maji wa kike anapomkaribia yule wa kiume, farasi-maji wa kiume hufurisha kifuko chake, rangi ya ngozi yake hung’aa, naye husonga huku na huku mbele yake. Wao huzungukana polepole na kushikamanisha mikia yao. Kisha wao huzunguka pamoja na kucheza dansi baharini kama farasi wanaorukaruka. Halafu wao hupanda na kushuka, hujibiringisha na kubadilisha rangi, nao hucheza pamoja kwa karibu nusu saa.

Dansi hiyo ya kujamiiana ndio mwanzo wa kuwa wazazi. Kuiter anasema hivi: “Wakati wa kujamiiana unapokaribia, wao hucheza dansi kwa muda mrefu zaidi na zaidi, nao wanaweza kurudia kufanya hivyo mara nyingi kwa siku. Dansi hiyo inapofikia upeo, wenzi hao wawili huinuka polepole juu ya maji huku mikia yao ikiwa imefungamanishwa na wakiwa wamekaribiana sana. Kisha yule wa kike huyaingiza mayai yake katika kifuko cha uzazi cha farasi-maji wa kiume ambacho kinafanana na cha kangaruu.” Halafu farasi-maji wa kiume hutafuta mahali patulivu baharini ili ayaweke vizuri mayai hayo ndani ya kifuko. Kisha yeye hutungisha mayai hayo na kubeba mimba, jambo linalomfanya kuwa kiumbe wa ajabu sana.

“Ndoto ya Kila Mwanamke”

Mwanamke mmoja alisema: “Inastaajabisha jinsi ambavyo farasi-maji wa kiume hubeba mimba na kuzaa watoto.” Mwanamke mwingine alisema hivi: “Farasi-maji wa kiume ni ndoto ya kila mwanamke.” Katika kipindi cha mwaka mmoja, farasi-maji mmoja wa kiume alibeba mimba saba mfululizo, kila moja ikichukua siku 21!

Farasi-maji wachanga wanapokuwa ndani ya kifuko cha uzazi, wao hupata chakula na hewa kupitia mishipa mingi ya damu. Baada ya muda, chumvi iliyo ndani ya kifuko huongezeka, na hivyo kuwatayarisha kuishi baharini. Wakati wa kujifungua unapofika, farasi-maji wa kiume anaweza kupata maumivu ya kuzaa kwa saa kadhaa au hata kwa siku mbili. Hatimaye, kifuko chake cha uzazi hufunguka na farasi-maji wachanga huzaliwa, mmoja baada ya mwingine. Idadi ya farasi-maji wanaozaliwa hutegemea jamii yao, hata inaweza kufikia 1,500.

Jinsi Wanavyotumiwa

Idadi ya farasi-maji ulimwenguni inapungua ijapokuwa samaki hao huzaana kwa wingi. Inakadiriwa kwamba kila mwaka ulimwenguni pote farasi-maji milioni 30 huvuliwa na kuuzwa. Wengi wao huuzwa huko Asia ili kutengeneza dawa za kienyeji za kutibu magonjwa mbalimbali kama vile pumu, mifupa iliyovunjika, na ugumba.

Kila mwaka, wasanii hutumia farasi-maji milioni moja hivi kutengeneza minyororo ya funguo, vifaa vya kushikilia karatasi, na mapambo. Uvuvi wa kutumia nyavu za kukokota, ulipuaji wa matumbawe kwa baruti, na uchafuzi huathiri maeneo ya pwani ambako farasi-maji huishi. Pia, farasi-maji waliovuliwa baharini huuzwa kwa wafugaji. Lakini wengi wao hufa wanapofugwa kwa sababu wanahitaji chakula cha pekee, nao hupata magonjwa mengi.

Ili kudhibiti uvuvi wa farasi-maji baharini, sheria zimetungwa kuzuia nchi nyingi zinazouza farasi-maji katika nchi nyingine zisiathiri idadi na mazingira yao. Mbinu bora za ufugaji na maendeleo ya kitekinolojia huwezesha wazalishaji fulani wa farasi-maji kuwafuga na kuwauza kwa wafugaji wengine.

Wakati ujao wa farasi-maji unategemea wakati ujao wa bahari. Kuiter analalamika hivi: “Wanadamu wanahatarisha bahari ulimwenguni pote. Tunatoa vitu vingi mno baharini.” Je, viumbe hao wa baharini wanaocheza dansi wataangamizwa na “maendeleo” ya wanadamu? Martin-Smith anasema: “Tunapaswa kutazamia mema. Kuna watu wengi wenye nia njema. Tuna wajibu wa kuwasaidia watu wengi zaidi kuwajali viumbe wa dunia. Hilo likitukia, mambo yatabadilika. Tukifaulu kuwaokoa farasi-maji, huenda tukafaulu kuokoa bahari.” Hata hivyo, kuna mtu mwenye kutegemeka anayetupatia tumaini.—Ufunuo 14:7.

[Picha katika ukurasa wa 15]

Farasi-maji wa “pygmy” (ukubwa kamili)

[Hisani]

© Reinhard Dirscherl/Visuals Unlimited ▼

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Farasi-maji wanaweza kubadili rangi ya ngozi yao kupatana na mazingira

Farasi-maji mwenye kichwa kifupi

Farasi-maji wenye tumbo kubwa

Farasi-maji mwenye milia

[Picha katika ukurasa wa 16]

Farasi-maji wa “high-crown”

[Picha katika ukurasa wa 17]

Farasi-maji wenye kichwa kifupi

[Picha katika ukurasa wa 17]

Farasi-maji wa kiume akizaa

[Picha katika ukurasa wa 17]

Farasi-maji wachanga walio na kichwa kifupi

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]

Lined seahorse: © Ken Lucas/Visuals Unlimited; all other photos: Rudie H Kuiter

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]

All photos: Rudie H Kuiter