Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Dawa ya Meno ya Wamisri wa Kale

Gazeti Electronic Telegraph laripoti hivi: “Maelezo ya kutengeneza dawa ya meno ya kale sana iliyotumiwa zaidi ya miaka 1,500 kabla ya William Colgate kuanza kuuza dawa yake ya kwanza mwaka wa 1873, yamepatikana kwenye mafunjo yenye vumbi katika chumba cha ardhini cha jumba moja la makumbusho huko Vienna. Mwandishi mmoja wa kale wa Misri alisema huo ni ‘unga unaofanya meno yawe meupe na yenye afya.’ Alitumia wino mweusi uliotengenezwa kutokana na masizi na gundi iliyochanganywa na maji kuandika maelezo hayo. Unga huo unapochangamana na mate mdomoni, unafanyiza ‘dawa safi ya meno.’” Maelezo hayo ya karne ya nne W.K., yanasema kwamba dawa hiyo imetengenezwa kwa kupondaponda na kuchanganya chumvi ya mawe, mnanaa, maua yaliyokaushwa ya airisi, na pilipili. Uvumbuzi huo uliwasisimua watu waliohudhuria kongamano la tiba ya meno huko Vienna. Dakt. Heinz Neuman, alionja dawa hiyo na kusema “anahisi mdomo wake ni safi,” na kwamba “hakuna daktari yeyote wa meno aliyefikiri kulikuwa na dawa kama hiyo ya hali ya juu hapo kale.” Makala hiyo inasema kwamba “hivi majuzi madaktari wa meno wametambua faida za ua la airisi ambalo linatibu ugonjwa wa ufizi na linauzwa sasa.”

Kuhifadhi Matunda kwa Muda Mrefu Zaidi

Ripoti ya gazeti New Scientist inasema kwamba “huenda hivi karibuni matunda yatahifadhiwa kwa muda mrefu zaidi kwa sababu ya umajimaji fulani wa divai nyekundu ambao unaboresha afya. Matofaa yalihifadhiwa kwa muda wa miezi mitatu badala ya majuma mawili yalipoingizwa katika umajimaji unaoitwa trans-resveratrol, ambao unapatikana katika zabibu. Zabibu zilizotumbukizwa katika umajimaji huo zilihifadhiwa kwa majuma mawili, mara mbili ya muda wa kawaida.” Watafiti wamegundua kwamba kiasi kidogo cha umajimaji huo ndicho kinachohitajika kuzuia matunda hayo yasiharibike na kuzuia hamira na kuvu ambazo huharibu matunda mengi. Kulingana na gazeti hilo “watafiti hao pia wamehifadhi mazao mengine kama vile nyanya, parachichi, na pilipili mbichi. Sasa wanachunguza mbinu za kutengeneza umajimaji huo ambazo hazigharimu pesa nyingi.”

Hatari za Kiafya za Michezo ya Video

Gazeti El Universal la Mexico City linasema kwamba huenda wazazi hawatambui jinsi michezo ya video inavyoathiri afya ya watoto wao. Kulingana na Antonio González Hermosillo, msimamizi wa Chama cha Mexico cha Ugonjwa wa Moyo, asilimia 40 ya watoto ambao hucheza michezo ya video watapata ugonjwa wa shinikizo la damu. Kwa nini? Kwa sababu mbali na kwamba hawafanyi mazoezi yoyote, watoto hao huwa na mfadhaiko mwingi sana kwa sababu ya kucheza michezo hatari inayohusisha mashambulizi, vita, na mapambano mengine. Kulingana na gazeti hilo, “mtaalamu huyo alionya kwamba magonjwa ya moyo, ambayo ndiyo kisababishi kikuu cha kifo nchini Mexico, yataongezeka sana nchini humo.”

“Kasoro Katika Uongozi”

Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, Dakt. Jacques Diouf, anasema: “Kuna kasoro katika uongozi ulimwenguni.” Alipokuwa akihutubia Shule ya Kennedy ya Usimamizi katika Chuo Kikuu cha Harvard, Marekani, Diouf alisema hivi: “Mojawapo ya mafanikio makubwa katika karne ya ishirini ni ongezeko la uzalishaji wa chakula ambalo lilizidi sana ongezeko kubwa la watu duniani. . . . Tunaweza kuzalisha chakula cha kuwatosha watu wote duniani.” Hata hivyo, watu milioni 800 katika nchi zinazoendelea pekee hawapati chakula cha kutosha, na watoto milioni 6 hivi walio chini ya umri wa miaka mitano hufa kila mwaka kwa sababu ya utapiamlo na njaa. “Wengi wao hufa kutokana na magonjwa kama vile kuharisha, malaria au ukambi, lakini wangepona iwapo wangepata chakula bora,” alisema Diouf. “Ni wazi kwamba tatizo la njaa ulimwenguni linasababishwa na siasa, wala si mbinu za kuzalisha chakula.” Aliongeza hivi: “Serikali zisipochukua hatua, huenda mambo hayatabadilika.”

Wazaliwa Nje ya Ndoa

Gazeti la Hispania La Vanguardia linaripoti kwamba katika Muungano wa Ulaya, “asilimia 25 ya watoto huzaliwa nje ya ndoa.” Maadili ya kawaida yanapobadilika, “idadi ya watoto wanaozaliwa nje ya ndoa inaongezeka kotekote Ulaya.” Kulingana na Idara ya Takwimu ya Jumuiya za Ulaya, nchi za Sweden, Denmark, na Ufaransa zinaongoza kwa asilimia 54, asilimia 46, na asilimia 39. Ufini na Uingereza zinafuata, kila moja ikiwa na asilimia 37 ya watoto wanaozaliwa nje ya ndoa. Hali hiyohiyo inaonekana katika nchi za Mediterania, ambako mila kali za kijamii zilifuatwa zamani. Kwa mfano, takwimu za hivi majuzi zinaonyesha kwamba nchini Hispania, asilimia 19 ya watoto wanazaliwa na wanawake ambao hawajaolewa, na katika maeneo mengine kama vile Catalonia, idadi hiyo ni asilimia 22—ongezeko la asilimia 100 katika muda wa miaka kumi tu.

Nusu ya Dunia Ni Nyika

Kitabu World Watch kinaripoti hivi: “Licha ya hatari za kimazingira kuongezeka katika karne iliyopita, asilimia 46 ya eneo la Dunia ni nyika.” Uchunguzi uliofanywa na wanasayansi 200 ulimwenguni pote “ulionyesha kwamba eneo lenye ukubwa wa [kilometa milioni 68 za mraba] lilihesabiwa kuwa ‘nyika,’ ikimaanisha kwamba lina angalau asilimia 70 ya mimea ya asili, lina watu [5] kwa kila [kilometa ya mraba] katika sehemu za mashambani, na kila nyika ina ukubwa wa [kilometa 10,000 za mraba].” Nyika 37 zina asilimia 2.4 tu ya idadi ya watu duniani, yaani watu milioni 144 bila kuhesabu wakazi wa mjini. Hata hivyo, maeneo hayo ni makubwa kama nchi sita kubwa ulimwenguni zikiunganishwa: Australia, Brazili, China, Kanada, Marekani, na Urusi. Lakini, kitabu hicho kinasema kwamba “zaidi ya thuluthi moja ya nyika ni eneo lenye barafu la Antaktiki au ukanda wa baridi wa Aktiki, na maeneo 5 kati ya 37 ndiyo yanayohitaji kuhifadhiwa kwa sababu kila moja lina zaidi ya aina 1,500 za wanyama na mimea ya asili.”

Nchi Yenye Wafungwa Wengi Zaidi Ulaya Magharibi

“Uingereza ndiyo nchi yenye wafungwa wengi zaidi huko Ulaya Magharibi. Kwa kila wakazi 100,000 wa Uingereza na Wales, kuna wafungwa 139,” lasema gazeti Guardian Weekly. “Idadi ya wafungwa imeongezeka kutoka 42,000 mwaka wa 1991 hadi 72,000.” Mahakama za Uingereza zinawahukumu watu wengi zaidi na kuwapa vifungo virefu zaidi. Mnamo mwaka wa 1992, asilimia 45 ya watu wazima walitiwa gerezani, ikilinganishwa na asilimia 64 mwaka wa 2001. Hata hivyo, idadi ya wafungwa ni kubwa zaidi katika nchi nyingine nje ya Ulaya Magharibi. Kwa kweli, karibu nusu ya wafungwa wapatao milioni 8.75 ulimwenguni pote wako katika nchi tatu tu: Marekani (milioni 1.96), China (milioni 1.4), na Urusi (900,000).

Hatari za Kuwa Mzito Kupita Kiasi

“Watu wazito kupita kiasi wenye umri wa miaka 40 huenda wakafa miaka mitatu kabla ya wale walio wembamba, ikimaanisha kwamba kuwa mnene katika umri wa makamo hupunguza maisha ya mtu kama kuvuta sigara,” laripoti gazeti The New York Times. “Uchunguzi huo unaonyesha kwamba ukiwa mzito kupita kiasi katikati ya umri wa miaka 30 hadi katikati ya umri wa miaka 40, unakabili hatari kubwa ya kufa hata ukipunguza uzito baadaye,” asema Dakt. Serge Jabbour, mkurugenzi wa kliniki ya kupunguza uzito. “Hiyo inamaanisha kwamba unapaswa kuanza kupunguza uzito mapema. Ukingoja sana, itakuwa kuchelewa.” Kupunguza uzito pia huzuia kufa kutokana na kansa. Kulingana na gazeti Times, baada ya kuwachunguza watu 900,000 kwa miaka 16, Chama cha Marekani cha Kansa kilisema kwamba “asilimia 14 ya wanaume na asilimia 20 ya wanawake hufa kutokana na kansa kwa sababu ni wazito kupita kiasi.” Uchunguzi unaonyesha kwamba aina nyingi za kansa husababishwa na kuwa mzito kupita kiasi.