Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mto Ulipogeuza Mkondo

Mto Ulipogeuza Mkondo

Mto Ulipogeuza Mkondo

MTO Mississippi ulio kama mkunjo katika ramani ya Marekani huigawanya nchi hiyo mara mbili. Una upana wa meta tatu mahali unapoanzia huko Minnesota. Lakini mto huo wenye urefu wa kilometa 3,700 unaoelekea kusini hupanuka sana wakati vijito vingi vinapojiunga nao. Karibu na New Orleans, Louisiana, mto huo hufikia kina cha meta 60 na upana wa kilometa moja. Kila sekunde mto huo humwaga lita 15,000,000 katika Ghuba ya Mexico. Wakati wa mafuriko, mto huo humwaga lita 80,000,000 kila sekunde.

Watu wanaoishi kwenye kingo za mto huo wanajua uharibifu unaoweza kusababishwa na maji hayo. Wameona mashamba yakifurika, maboma ya kuzuia maji yakibomolewa, nyumba zikisombwa, na watu wakifa. Lakini watu wengi leo hawawezi kuwazia kile kilichoupata mto huo yapata miaka 200 iliyopita.

Mnamo Desemba 1811, matetemeko yenye nguvu sana yalikumba bonde la kati la Mississippi kwa majuma kadhaa. Matetemeko hayo yaliufanya mto huo usukesuke kama bahari iliyochafuka. Ardhi ilitetemeka sana hivi kwamba mnamo Februari 7, 1812, Mto Mississippi ulielekea kaskazini badala ya kusini, karibu na New Madrid, Missouri.

Siku za Kuogopesha na Kutetemesha

Tukio hilo lilikuwa upeo wa kipindi cha kuogofya kinachoitwa matetemeko ya ardhi ya New Madrid. Mnamo Desemba16, 1811, saa 8:00 usiku, tetemeko la kwanza lilikumba eneo la kusini-mashariki la jimbo la Missouri. Wakulima na wakazi wa mjini waliamka wakati fanicha zilipoanza kutikisika na vitu vya kauri kuvunjika. Nyumba ziling’oka kwenye misingi yake. Watu walikimbia nje na kukaa huko, huku wakitetemeka kwa sababu ya baridi na tetemeko la ardhi. Nyumba zao zilizopaswa kuwakinga zilikuwa hatari.

Ardhi iliendelea kutikisika, lakini kwa kiwango kidogo kabla ya mapambazuko. Tetemeko lingine lilitokea mwendo wa saa 1:00 asubuhi. Halafu, karibu saa 5:00 asubuhi, tetemeko lingine lenye nguvu zaidi likatokea. Ardhi ilipasuka-pasuka. Matope, maji, na makaa ya mawe yalifoka kutoka nyufa hizo zenye kutisha. Gesi za salfa zenye uvundo zilitoka ardhini na kuchafua hewa. Watu walioshuhudia kisa hicho waliona maelfu ya ndege wenye wasiwasi wakipaa kutoka kwenye eneo hilo. Matetemeko hayo yenye fujo yalipokoma, mji wa Little Prairie, Missouri, ulikuwa magofu.

Safari Yenye Msukosuko Mtoni

Wakati huohuo, meli mpya ya mvuke inayoitwa New Orleans ilikuwa ikiabiri kwenye Mto Ohio kuelekea Mississippi na mwishowe ingefika New Orleans, Louisiana. Shangwe ziligeuka kuwa majonzi meli hiyo ilipofika kwenye sehemu iliyoathiriwa na matetemeko. Kingo za mto zilikuwa zikitetemeka na kuporomoka mtoni. Miti iliyokuwa imekaa ndani ya mto kwa muda mrefu ilielea na karibu ivunje meli hiyo. Mawimbi makubwa yaliyumbisha meli huku na huku kama bendera. Ramani za safari hazikusaidia kwa kuwa matetemeko yaligeuza mkondo wa mto. Safari ya kupendeza ikawa yenye kuogopesha.

Mnamo Desemba 19, 1811, meli ya New Orleans ilikaribia New Madrid, ili ichukue bidhaa. Hata hivyo, mji huo ulio karibu na mto, ambao hapo awali ulikuwa na shughuli nyingi, haukukalika. Watu wachache waliokuwa wamebaki waliipungia mkono mashua hiyo ili ije iwaokoe kutoka kwenye magofu ya nyumba na maduka yao.

Hata hivyo, meli hiyo iliendelea na safari yake kwenye Mto Mississippi huku abiria wakitetemeka. Ilipita mji wa Point Pleasant ambao ulikuwa mahame. Meli hiyo ilipaswa kusimama pia huko Little Prairie, lakini haikufanya hivyo kwa kuwa sehemu kubwa ya mji huo ilikuwa magofu na majengo yaliyokuwa yamesalia yalikuwa yameharibiwa sana.

Ilipozidi kusonga kusini, meli hiyo ilipata magogo mengi. Matetemeko ya ardhi yalikuwa yameng’oa miti mingi na kuiangusha mtoni. Baada ya kujitahidi kwa udi na uvumba kupita hapo, mabaharia wa meli ya New Orleans walishusha nanga jioni katika Kisiwa Na. 32, karibu na mji wa kisasa wa Osceola, Arkansas. Karibu saa 10:30 alfajiri mnamo Desemba 21, abiria mmoja alisikia kamba ya nanga ikijikaza isivyo kawaida. Jambo hilo lilibainika asubuhi. Kamba hiyo ilikuwa imevutwa sana. Nanga ilikuwa imeshuka. Kumbe wakati wa usiku sakafu ya mto ilikuwa imezama na Kisiwa Na. 32 kilikuwa kimezama kwa sababu ya matetemeko ya New Madrid.

Meli ya New Orleans ilimaliza safari yake ya kwanza salama salimini na ikawa meli ya kwanza yenye injini ya mvuke kuabiri Mto Mississippi. Labda hata jambo kubwa zaidi ni kwamba ilifaulu kufika.

Matetemeko Zaidi

Matetemeko mengi yaliendelea kutukia hata kufikia Januari 1812. Mnamo Januari 23, mwendo wa saa 3:00 asubuhi, watu walishtushwa sana na tetemeko lingine lenye nguvu. Mji wa Point Pleasant, Missouri, ambao tayari ulikuwa umekumbwa na matetemeko mengine, ulikuwa karibu na kiini cha tetemeko hilo na wakazi wake walitoroka. Wakazi wengine waliporudi mnamo Februari 1812, waligundua kwamba mji ulikuwa umeharibiwa kabisa na mtu hangejua palikuwa na mji zamani. Tetemeko la Januari 23 lilifanya mji wote wa Point Pleasant uporomoke katika Mto Mississippi.

Watu wengi katika eneo hilo waligeukia dini wakihofia kwamba mwisho wa dunia ulikuwa umefika. Makasisi wengine walifurahi sana kwa sababu watu walitubu na kujaza makanisa ambayo kwa muda mrefu hayakuwa na watu. Wengine walishuku nia ya watu wengi waliogeukia dini na kuwaita Wakristo wa tetemeko. Kasisi James B. Finley alitoa hotuba motomoto na akanukuu andiko la Ufunuo 6:17 kutoka Biblia ya King James: “Kwa maana siku iliyo kuu ya hasira yake imekuja; naye ni nani atakayeweza kusimama?” Ingawa ilikuwa vigumu kusimama kiroho, ilikuwa vigumu hata zaidi kusimama kihalisi kwa sababu ya matetemeko ya ardhi.

Tetemeko la Mwisho

Ingawa waumini walisali sana ili kuwe na utulivu, eneo hilo liliendelea kukumbwa na msiba. Kabla ya mapambazuko mnamo Februari 7, 1812, usingizi wa wakazi wa eneo hilo ulikatishwa na tetemeko lingine lenye nguvu. Tetemeko hilo lilikuwa lenye nguvu zaidi ya matetemeko ya awali kwani lilibomoa mabomba ya moshi ya Cincinnati, Ohio, kilometa 650 kutoka eneo hilo. Kengele za kanisa zililia huko Boston, Massachusetts, kilometa 1,600 kutoka hapo. Mbali sana huko Montreal, Kanada, sahani zilichezacheza juu ya meza. Mtu mmoja huko Kentucky, aliyeishi umbali wa kilometa 130 hivi kutoka kwenye kiini cha tetemeko, aliandika hivi katika kitabu chake: “Tusipoondoka hapa, ardhi itatumeza tukiwa hai.” Hata hivyo, tetemeko hilo liliathiri hasa mji wa New Madrid, ulio karibu na mto.

Matetemeko ya mapema yaliharibu kabisa mji wa New Madrid na kuwaua wakazi kadhaa huku wengine wakikimbia. Mnamo Februari 7, tetemeko hilo liliharibu kabisa majengo yaliyosalia. Tetemeko hilo lilipotokea, wakazi waliobaki walikimbia na wakaponea chupuchupu. Mji huo ulikuwa umejengwa kwenye ukingo wa juu wa mto ambao uliporomoka na kuishia kwenye Mto Mississippi. Mto huo ulisomba mbao, matofali, na mawe ya New Madrid. Muda si muda, mji wote ulikuwa umetokomea.

Jinsi Mto Ulivyoathiriwa

Matetemeko ya New Madrid yalisababisha maporomoko ya maji kwenye Mto Mississippi karibu na New Madrid. Mashua nyingi zilipinduliwa na maporomoko hayo. Tetemeko la Februari 7 lilitikisa ardhi na kuizamisha na kugeuza mkondo wa mto. Nyufa kubwa zilitokea kwenye sakafu ya mto na mashua nyingi zikazama humo. Matetemeko hayo yalibadili njia ya mto, na miji na nyumba zikafunikwa. Matetemeko hayo pia yalielekeza maji ya mto kwenye mitaro, na hivyo ndivyo Ziwa Reelfoot lilivyofanyizwa. Ziwa hilo halikuwepo kabla ya mwaka wa 1812. Miti ambayo hapo awali ilikuwa kwenye nchi kavu ingali inasimama katikati ya maji ya Ziwa Reelfoot huko Tennessee.

Ni vigumu kujua vipimo sahihi vya matetemeko hayo kwa sababu vifaa vya kisasa vya kupima matetemeko havikuwepo mwaka wa 1812. Wanasayansi wanakadiria kwamba angalau matetemeko matatu ya New Madrid yalizidi kipimo cha 8.0 kwenye kipimo cha Richter. Hayo ndiyo matetemeko makubwa zaidi kuwahi kutukia nchini Marekani na ni miongoni mwa matetemeko yenye nguvu zaidi kuwahi kutukia duniani. Hata ingawa eneo hilo halikuwa na watu wengi sana, makumi, au hata mamia, ya watu walikufa katika msiba huo.

Leo Mto Mississippi hutiririka katika eneo la kusini-mashariki la Missouri kana kwamba hakuna chochote kilichotukia. Lakini ikiwa mto huo ungeweza kuongea, ungesimulia vile mkondo wake ulivyogeuzwa.

[Ramani katika ukurasa wa 18]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

MISSOURI

Mississippi Mto

New Madrid

[Picha katika ukurasa wa 19]

Meli ya “New Orleans”

[Hisani]

Used by permission, State Historical Society of Missouri, Columbia

[Picha katika ukurasa wa 20]

Matetemeko ya ardhi yalitokeza Ziwa Reelfoot

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 18]

U.S. Fish & Wildlife Service, Washington, D.C./Dave Menke