Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mnyama Mdogo Mwenye Miiba wa Mashambani

Mnyama Mdogo Mwenye Miiba wa Mashambani

Mnyama Mdogo Mwenye Miiba wa Mashambani

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UINGEREZA

UKUNGU ulitanda kwenye bonde la Tyne lililoko kaskazini mwa Uingereza, huku ndege wakubwa weusi wanaofanana na kunguru wakilia na kusikika mbali sana katika hewa iliyotulia wakati wa jioni. Nilikuwa nikitembea kwenye kijia cha msituni wakati niliposikia mchakato wa matawi ya rangi nyekundu, ya kahawia, na ya manjano yaliyokuwa chini. Niliona miguu miwili mifupi myembamba ya nyuma ikisonga kuingia katika pango lililokuwa kwenye ukingo wa kijito kilichokuwa karibu.

Nilipotazama kwa makini, nilimwona nungunungu akitayarisha pango lake ambamo angeishi wakati wa baridi. Tayari alikuwa ameingiza matawi, nyasi kavu, na kangaga. Alikuwa akitandika kitanda chake ambacho angelalia mchana na usiku katika majira yote ya baridi kali.

Mnyama huyu mdogo anayeishi milimani, mashambani, na msituni ni wa kipekee sana. Ana manyoya magumu ya kahawia na meupe kichwani na shingoni, lakini miiba yake yenye ncha za rangi ya manjano ndiyo humtambulisha zaidi. Miiba hiyo yenye urefu wa sentimeta mbili hivi ni mikali na imepangwa katika makundi-makundi. Miiba ya kila kundi hukua kutoka mahali pamoja na kuufunika mwili wake. Kila mwiba umezungukwa na mitaro-mitaro 22 hadi 24 na umejipinda mahali ambapo umeshikamana na ngozi na kufanyiza pembe-mraba. Mwiba huanza kuwa mwembamba na kujipinda unapokaribia kushikana na ngozi. Ndiyo sababu nungunungu hawezi kuchomwa na miiba yake hata akianguka kutoka mahali palipoinuka. Ama kweli, nungunungu ameumbwa kwa njia ya ajabu!

Anaposhtuliwa, nungunungu hujikinga kwa kujikunja kama mpira. Misuli yake yenye nguvu hukaza ngozi yake yenye miiba na kuufunika mwili wake mzima. Ngozi hiyo yenye miiba hufunika kichwa, mkia, miguu, na sehemu zake za chini. Mnyama huyo anaweza kujikunja hivyo kwa muda mrefu.

Nungunungu huona njaa wakati wa jioni. Chakula chake cha jioni huwa wadudu na minyoo, lakini wakati mwingine anaweza kula panya, chura, mjusi, au hata njugu na matunda ya beri. Nungunungu husikia vizuri sana. Pia ana uwezo wa kunusa wenye nguvu, na unaweza kutambua jambo hilo ukiona pua lake refu lenye umajimaji.

Maadui Zake—Wanyama na Wanadamu

Mbali na mbweha na melesi, nungunungu hana maadui wengi mwituni. Melesi aweza kubambua ngozi ya nungunungu kwa kucha zake zenye nguvu bila kuumizwa na miiba. Nimewahi kuona ngozi ya nungunungu mara kadhaa. Huenda ngozi hiyo ikawa imebaki baada ya melesi kumla nungunungu mzima. Kwa upande mwingine, mbweha hawezi kustahimili miiba ya nungunungu, lakini anaweza kujaribu kumviringisha hadi majini, ambapo nungunungu hulazimika kujikunjua la sivyo atakufa maji. Kwa kuwa nungunungu ni mwogeleaji hodari, huenda akafikia mawe au kuingia ndani ya mashimo yaliyo kando ya mto kabla mbweha hajamnyakua na kumfanya kuwa kitoweo chake.

Jamii fulani ya wahamaji na wakazi wengine wa mashambani hula nungunungu waliochomwa katika udongo wa mfinyanzi. Udongo unapopoa, miiba hutoka na kinachobakia ni nyama iliyoiva—“mlo mtamu sana,” kama asemavyo Jean-Paul Clébert kwenye kitabu chake The Gypsies. Inahuzunisha kuona vile nungunungu wengi leo hugongwa na kuuawa na magari. Inaonekana wao hasa hugongwa wanapoamka tu na kuanza kutafuta chakula. Lakini nungunungu wakiponyoka hatari zinazotokana na wanyama hao na wanadamu, wanaweza kuishi kwa miaka sita hivi na kufikia urefu wa sentimeta 25.

Kuzaa, Kulala, na Kulisha

Nungunungu huanza kujamiiana katikati ya miezi ya Mei na Julai, na wanarudia kufanya hivyo kwa mara ya pili katika kipindi hichohicho. Baada ya majuma manne hadi sita, watoto watatu au wanne huzaliwa wakiwa na uzito unaopungua gramu 30. Watoto hao huwa hawaoni wala kusikia wanapozaliwa, hivyo wanaweza kushambuliwa kwa urahisi katika majuma mawili ya kwanza. Kisha miiba humea mahali palipokuwa na manyoya laini. Baadaye wanaweza kujikunja kabisa. Kabla ya kupata uwezo huo, wao huruka juu mara moja na kutoa mlio mkali wa kuchatachata wanaposhtuliwa. Jambo hilo huwashtua maadui zao wengi.

Wakati nungunungu amelala, yeye hutumia mafuta aliyohifadhi mwilini katika miezi ya joto. Wakati huo joto la mwili wake hupungua sana, naye hupumua kidogo sana hivi kwamba si rahisi kutambua kama anapumua. Ana tezi maalumu anayotumia kudhibiti hali ya joto la mwili wake anapolala. Kiasi cha joto kikipungua sana wakati huo, tezi hiyo hutokeza joto zaidi linalomfanya ajue kwamba anapaswa kutafuta makao yenye joto zaidi, yaliyozingirwa zaidi. Hii haimaanishi kwamba wakati wa baridi nungunungu hana habari kuhusu kinachoendelea katika mazingira yake. Anaweza kusikia sauti yoyote iliyo karibu naye, na kumfanya asonge kidogo.

Ukijaribu kumfuga nungunungu, yeye hupanda ukutani, au kwenye bomba la maji na kuponyoka kwani anapenda kulisha katika eneo kubwa. Ndiyo sababu, si rahisi kumfuga au kumfanya awe mnyama kipenzi. Ni vizuri zaidi kwamba hafugwi kwa kuwa yeye hubeba viroboto wengi sana kutoka msituni. Hata hivyo, maisha yake ya kuzurura-zurura katika maeneo ya mashambani ya Uingereza hunivutia sana, nami humshukuru Muumba wetu, Yehova Mungu, kwa jambo hilo.

[Picha katika ukurasa wa 15]

Nungunungu amejikunja kama mpira

[Picha katika ukurasa wa 16]

Mchoro wa nungunungu wa Beatrix Potter katika kitabu chake cha hadithi za watoto, “The Tale of Mrs. Tiggy-Winkle” cha mwaka wa 1905

[Picha katika ukurasa wa 16]

Nungunungu wa kawaida, mwenye umri wa juma moja

[Picha katika ukurasa wa 17]

Aina fulani ya nungunungu kutoka Afrika Kusini