Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Kunenepa Kupita Kiasi Ni Tatizo la Ulimwenguni Pote?

Je, Kunenepa Kupita Kiasi Ni Tatizo la Ulimwenguni Pote?

Je, Kunenepa Kupita Kiasi Ni Tatizo la Ulimwenguni Pote?

JARIDA la kitiba The Lancet la Uingereza linasema hivi: “Kwa muda mrefu kunenepa kupita kiasi kumeonwa kuwa tatizo linalowakumba watu katika nchi tajiri zilizoendelea, lakini sasa tatizo hilo linawakumba watu katika nchi zinazoendelea pia.” Jarida hilo lilisema kuwa wataalamu wa chakula sasa wanasema kwamba kunenepa kupita kiasi kunasababisha magonjwa kama vile shinikizo la damu, ugonjwa wa sukari, kansa, na magonjwa ya moyo na limekuwa “tatizo la ulimwenguni pote.”

Kwa kuwa idadi ya wanaume ambao ni wanene kupita kiasi huko China imeongezeka mara tatu na idadi ya wanawake wanene kupita kiasi imeongezeka mara mbili katika miaka minane iliyopita, idadi ya wanaougua shinikizo la damu nchini humo sasa ni sawa na ile ya Marekani. Zaidi ya nusu ya watu wanaopata ugonjwa wa sukari wanapatikana India na China. Idadi ya watu wanaougua ugonjwa huo nchini Misri ni sawa na ile ya Marekani, na nusu ya wanawake nchini Misri ni wanene kupita kiasi. Huko Mexico, kuna ongezeko kubwa la watu wanene kupita kiasi wanaotoka katika matabaka yote ya jamii na sehemu zote za nchi. Jambo hilo limesababisha ongezeko la wagonjwa wa sukari. Hata katika nchi maskini zilizo kusini mwa jangwa la Sahara, unene wa kupita kiasi umeongezeka na ugonjwa wa sukari vilevile.

Ingawa huenda vyakula vyenye mafuta-mafuta vinavyouzwa mahotelini vikawafanya watu wanenepe kupita kiasi katika nchi fulani, tatizo hilo linasababishwa hasa na watengenezaji wa vyakula ambao wanaviongeza sukari “ili viwe na ladha tamu.” Isitoshe, vyakula vya Kiasia na Kiafrika hutiwa mafuta mengi sana, na hivyo kuongeza mafuta mwilini. Maendeleo ya kitekinolojia viwandani na katika kilimo yamepunguza kazi. Watu hawataki kufanya kazi nyingi bali wanataka kupumzika sana. Sasa kwa kuwa kompyuta na televisheni zimeongezeka sana, wafanyakazi hawafanyi mazoezi mengi, na “utumizi wa barua-pepe umepunguza uhitaji wa kutembea ili kupeleka ujumbe na kuwatembelea wafanyakazi wengine ili kuwasiliana nao.”

Kwa kuwa watoto wengi zaidi wa shule wananenepa kupita kiasi, hasa katika shule ambazo zimepunguza wakati wa kwenda tafrija na kufanya mazoezi, walimu wanapaswa kufahamu kwamba matokeo mazuri shuleni yanategemea ulaji. Gail Harrison, wa Taasisi ya Afya ya Umma katika Chuo Kikuu cha California, anaonya kwamba zaidi ya kuwa na mikakati ya kuzuia tatizo la kunenepa kupita kiasi na magonjwa yanayohusiana nalo, “miradi ya kuzuia tatizo hilo inapaswa kuanzishwa ulimwenguni pote, pamoja na mipango, wafanyakazi, na utaratibu maalumu wa kutimiza miradi hiyo.”