Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuwachora Watu Maarufu na Wahalifu

Kuwachora Watu Maarufu na Wahalifu

Kuwachora Watu Maarufu na Wahalifu

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UINGEREZA

UMEWAHI kuchora uso wa mwanadamu? Hiyo si kazi rahisi. Vipi ikiwa unataka kumchora mtu ambaye umemwona sasa hivi tu na kwa muda mfupi? Ni vigumu hata zaidi ikiwa unamchora ukitegemea tu mambo unayokumbuka kuhusu sura yake. Zaidi ya hayo, mchoro wako unapaswa kukamilika baada ya dakika 30 ili utumiwe na wapiga-picha wa televisheni ambao wanangoja!

Kweli, wengi wetu hatuwezi kuchora haraka hivyo. Lakini nchini Uingereza, kuna watu wachache ambao hufanya kazi hiyo. Wao ni kina nani? Ni wachoraji wa vikao vya mahakamani.

Vizuizi vya Kisheria

Watu huvutiwa sana na vikao vya mahakamani, na katika nchi nyingi si ajabu kuwaona wapiga-picha wa televisheni wakinasa matukio ya vikao hivyo. Lakini katika Uingereza hali ni tofauti. Ni hatia “kujaribu kumchora mtu yeyote” ukiwa mahakamani, iwe ni hakimu, mashahidi au hata washtakiwa na wafungwa. * Ndiyo sababu wachoraji wa vikao vya mahakamani wanahitajiwa ili kuwasaidia waandishi wa habari kunasa matukio ya kesi mbalimbali.

Ili nijifunze mengi zaidi kuhusu taaluma hiyo yenye kupendeza, nilienda kwenye maonyesho ya sanaa huko London. Kwenye kibanda kimoja ambacho kilitembelewa na watu wengi, nilikutana na Beth, mmoja wa wachoraji maarufu wa mahakamani. Swali la kwanza nililomuuliza lilikuwa: “Wewe hutumia muda gani mahakamani ukimtazama mshtakiwa?”

Wakati na Kusudi Langu

“Mshtakiwa husimama kizimbani kwa dakika mbili hivi kesi yake inapotajwa kwa mara ya kwanza, lakini muda huo unatosha,” Beth alisema. “Wakati huo unanitosha kutambua umbo la kichwa chake, mtindo wake wa nywele, umbo la pua, macho, na mdomo. Ni lazima pia nitambue upana wa uso wake, urefu wa kipaji cha uso, ukubwa wa masikio na mambo mengine kama vile ndevu na miwani. Ni lazima nipate habari hizo za msingi ili niweze kumchora mtu kwa usahihi.

“Wakati mwingine kazi yangu huwa ngumu sana. Kwa mfano, katika kesi moja hivi karibuni kulikuwa na wanaume 12 kizimbani! Ingawa walisimama hapo kwa muda wa dakika 15, kusoma sura za watu 12 wakati mmoja kunahitaji mtu awe makini sana. Nina uwezo wa kukumbuka mambo ninayoona, lakini nimehitaji kuuboresha uwezo huo kwa miaka mingi. Nitokapo mahakamani, ninapaswa kukumbuka sura zote nilizoona hata ninapofunga macho.”

Kisha nikamuuliza hivi: “Unatumia muda gani kufanya utafiti kuhusu watu utakaowaona mahakamani?” Jibu lake lilinishangaza.

“Tofauti na waandishi wa habari, mimi sifanyi utafiti wowote. Mimi huenda mahakamani bila kuathiriwa na mawazo yoyote, nikijitahidi kutokata kauli kuhusu watu nitakaowaona. Mimi hurekodi mambo yanayoendelea mahakamani nikikumbuka kwamba sura za watu zinaweza kubadilika siku baada ya siku. Najua mahakimu wanaweza kuiona michoro yangu kwenye televisheni au magazetini, na singependa kumfanya yeyote kati yao aseme, ‘Huyu mshtakiwa anaonekana kuwa mwenye hatia!’ Jambo hilo huufanya uchoraji wa vikao vya mahakamani kuwa tofauti kabisa na uchoraji mwingine.”

“Pindi Muhimu Zaidi”

Nilipomuuliza Beth kuhusu siri ya kufanikiwa katika kazi yake, alinijibu: “Mimi hungojea pindi fulani ambayo hufunua wazi hali ilivyo mahakamani—hiyo ndiyo ‘pindi muhimu zaidi.’ Kwa mfano, mshtakiwa mmoja alipofunika uso wake kwa mikono, hiyo ilionyesha waziwazi kwamba mambo yalikuwa yanamwendea mrama. Kwenye pindi nyingine, mwanamke fulani alipoulizwa kama alikuwa mama mwenye kujali, uso wake ulijibu swali hilo vizuri zaidi kuliko maneno yake. Vivyo hivyo, mtu anapofuta machozi kwa kitambaa, hiyo yaweza kuonyesha waziwazi hisia zake za moyoni.

“Mchoraji wa vikao vya mahakamani pia hunasa mazingara yote ya mahakamani. Yeye huchora mahakimu, mawakili, maafisa wa mahakama, vitabu, kiasi cha mwangaza, na fanicha. Mchoro unaoonyesha vitu vyote hivyo huwavutia watu wengi kwa sababu hawajawahi kuviona vitu hivyo. Mimi huchorea picha zangu wapi? Wakati mwingine katika chumba cha waandishi wa habari mahakamani, lakini mara nyingi nikiwa nimeketi mahali patulivu kwenye ngazi za jengo. Lakini ni lazima nirudi mahakamani ili niongeze mashahidi wengine kwenye mchoro wangu au wakili wa upande wa washtakiwa anapohutubu.” Beth aliongezea kusema hivi akitabasamu: “Naam, michoro yangu mingi imewekwa kwenye ofisi nyingi za mawakili.”

Nilipozitazama picha zenye kupendeza kwenye kibanda chake cha maonyesho, zilinikumbusha kesi zilizohusu watu fulani maarufu na vilevile wahalifu nilizokuwa nimesoma magazetini katika miaka ya majuzi. Baada ya dakika kumi hivi, nilipokuwa nakaribia kuondoka, Beth alinipatia mchoro fulani. Kumbe alikuwa amenichora.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 6 Sheria hiyo haitumiki nchini Scotland.

[Picha katika ukurasa wa 15]

Mchoro wa kikao cha mahakamani na jinsi ulivyoonekana gazetini (kushoto)

[Hisani]

© The Guardian