Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Historia Inayopendeza ya Siria

Historia Inayopendeza ya Siria

Historia Inayopendeza ya Siria

ZAMANI za kale misafara ya ngamia iliyosafiri kutoka Mediterania mpaka China na kutoka Misri mpaka Anatolia ilipitia nchi hii, na vilevile ya majeshi ya Akadi, Babiloni, Misri, Uajemi, Ugiriki, na Roma. Mamia ya miaka baadaye, Waturuki na Wapiganaji wa Vita Vitakatifu waliipitia. Na majeshi ya Ufaransa na Uingereza yameipigania katika siku zetu.

Maelfu ya miaka iliyopita nchi hiyo iliitwa Siria, na sehemu moja ya eneo hilo bado inaitwa hivyo leo. Ijapokuwa eneo hilo limebadilika-badilika, bado kuna vitu vingi huko vinavyotukumbusha matukio ya zama za kale. Wanafunzi wa Biblia hupendezwa hasa na Siria kwa maana nchi hiyo inatajwa katika Biblia.

Jiji la Kale la Damasko

Kwa mfano, jiji kuu la Siria, Damasko, linasemekana kuwa mojawapo ya majiji ya kale duniani ambayo yamekaliwa tangu yalipoanzishwa bila kuwa mahame kamwe. Mto Barada unapita katikati ya jiji hilo lililojengwa chini ya milima ya Anti-Lebanon, ukingoni mwa jangwa kubwa la Siria. Kwa mamia ya miaka jiji hilo lenye maji lilikuwa kituo kilichotazamiwa kwa hamu na misafara ya ngamia. Yaelekea Abrahamu alipita mji huo aliposafiri kuelekea kusini kwenda Kanaani. Naye alimchukua “Mdameski,” Eliezeri, awe mtumishi wake.—Mwanzo 15:2.

Karibu miaka elfu moja baadaye, wafalme wa Siria wa eneo la Soba walipigana na Sauli, mfalme wa kwanza wa Israeli. (1 Samweli 14:47) Daudi, mfalme wa pili wa Israeli, alipigana pia na wafalme wa Aramu (jina la Kiebrania la Siria), naye akawashinda, na “akaweka ngome katika Shamu ya Dameski.” (2 Samweli 8:3-8) Ndipo uadui ulioendelea kwa muda mrefu kati ya Waisraeli na Wasiria ulipoanza.—1 Wafalme 11:23-25.

Yaelekea uadui huo kati ya Wasiria na Wayahudi ulikuwa umepoa katika karne ya kwanza W.K. Hata kulikuwa na masinagogi kadhaa ya Wayahudi huko Damasko wakati huo. Huenda ukakumbuka kwamba Sauli wa Tarso (aliyeitwa Paulo baadaye) alikuwa njiani kwenda Damasko kutoka Yerusalemu alipogeuzwa imani akawa Mkristo.—Matendo 9:1-8.

Katika jiji la kisasa la Damasko hakuna uthibitisho wowote wa kuonyesha kwamba Abrahamu alipita huko wala wa ushindi wa Daudi. Lakini kuna mabaki ya jiji kale la Waroma na vilevile barabara moja ya jiji hilo la kale inapita mahali ambapo barabara ya Waroma iliyoitwa Via Recta (Barabara Nyoofu) ilipita. Sauli aligeuzwa imani kimwujiza nje tu ya Damasko na ilikuwa katika nyumba moja kando ya barabara hiyo ambamo Anania alimpata baada ya yeye kuwa Mkristo. (Matendo 9:10-19) Barabara ya leo haifanani hata kidogo na barabara iliyokuwapo nyakati za Waroma. Hata hivyo, hapo ndipo mtume Paulo alipoanza utumishi wake wa kipekee. Barabara Nyoofu inafika hadi lango la Kirumi liitwalo Bab-Sharqi. Kuta za jiji zilizo na nyumba juu zinatusaidia kuelewa jinsi Paulo alivyoweza kutoroka kwa kushushwa katika kikapu kupitia tundu ukutani.—Matendo 9:23-25; 2 Wakorintho 11:32, 33.

Jiji la Jangwani la Palmyra

Inachukua saa tatu kufikia jiji la kale la Palmyra kwa gari, lililoko kaskazini-mashariki ya Damasko. Jiji hilo linaitwa Tadmori katika Biblia. (2 Mambo ya Nyakati 8:4) Jiji hilo lilikuwa katikati ya Bahari ya Mediterania na Mto Eufrati na linapata maji kutoka chemchemi za chini ya ardhi zinazobubujika hapo, ambazo zinatoka kwenye milima iliyo upande wa kaskazini. Wanabiashara wa kale waliosafiri kati ya Mesopotamia na nchi za magharibi walipitia eneo la Fertile Crescent upande wa kaskazini, mbali sana na Palmyra. Hata hivyo, katika karne ya kwanza K.W.K., kulikuwa na mgogoro wa kisiasa huko kaskazini hivyo wanabiashara wakaanza kutumia njia nyingine fupi upande wa kusini. Wakati huo Palmyra likaanza kusitawi.

Kwa kuwa jiji la Palmyra lilitumiwa na Waroma kukinga eneo la mashariki la milki hiyo, likaunganishwa na Siria iliyotawaliwa na Roma, lakini hatimaye lilipata uhuru. Kandokando ya barabara kuu ya fahari yenye nguzo kulikuwa na mahekalu makubwa, tao, vyumba vya kuogea, na jumba la michezo. Njia za miguu pande zote za barabara hiyo zilifunikwa kwa mawe, lakini sehemu ya katikati iliachwa ili ngamia watembee kwa starehe. Misafara ya ngamia iliyosafiri kati ya India na China upande wa Mashariki na Ugiriki na Roma upande wa Magharibi ilitua Palmyra. Hapo walitozwa kodi za vitambaa vya hariri, vikolezo, na bidhaa nyingine walizosafirisha.

Jiji la Palmyra lilisitawi sana katika karne ya tatu W.K., nalo lilikuwa na wakazi 200,000 hivi wakati huo. Ndipo Malkia Zenobia mwenye kutaka makuu alipopigana na Roma na hatimaye akashindwa mwaka 272 W.K. Hivyo, bila kujua Zenobia alitimiza sehemu ya unabii ulioandikwa na nabii Danieli miaka 800 mapema. * (Danieli, sura ya 11) Baada ya Zenobia kushindwa, Palmyra liliendelea kuwa jiji muhimu katika Milki ya Roma kwa muda, lakini halikuwa na fahari na nguvu kama awali.

Kuelekea Mto Eufrati

Baada ya kusafiri jangwani kwa muda wa saa tatu kuelekea kaskazini-mashariki, tunawasili kwenye mji wa Dayr az Zawr, ambapo mto mkubwa wa Eufrati unapita. Chanzo cha mto huo kiko katika milima iliyo katika sehemu ya mashariki ya Anatolia (sehemu ya Uturuki iliyomo Asia), kisha mto huo unaingia Siria, kaskazini tu ya Karkemishi, na kuelekea kusini-mashariki kupitia Siria hadi Iraki. Kuna mabaki ya majiji mawili ya Siria karibu na mpaka wa Iraki.

Umbali wa kilometa 100 kuelekea kusini-mashariki kutoka Palmyra, mahali ambapo Mto Eufrati unajipinda, kuna magofu ya jiji la kale la Dura-Europos lenye ngome. Jiji la kale la Mari lilikuwa umbali wa kilometa 25 kuelekea kusini-mashariki kutoka Dura-Europos. Jiji hilo lililokuwa tajiri kibiashara liliharibiwa na Mfalme Hammurabi wa Babiloni katika karne ya 18 K.W.K. Mabamba zaidi ya 15,000 ya udongo yenye maandishi yamepatikana katika jumba la mfalme la jiji hilo. Hayo yanaeleza mengi kuhusu maisha ya wakati huo.

Majeshi ya Hammurabi walipoharibu jiji hilo, walibomoa kuta za juu na kujaza vyumba vya chini kwa matofali na udongo. Kwa hiyo, michoro ya kuta, sanamu, vyombo vya udongo, na vitu vingine vingi vilihifadhiwa hadi wanaakiolojia Wafaransa walipogundua jiji hilo mwaka wa 1933. Vitu hivyo vimo katika majumba ya makumbusho huko Damasko na Aleppo, na vilevile huko Louvre, Paris.

Majiji ya Kale Huko Kaskazini-Magharibi mwa Siria

Ukifuata Mto Eufrati kuelekea kaskazini-magharibi utafika Aleppo (Haleb). Aleppo, sawa na Damasko, ni mojawapo ya majiji ya kale duniani ambayo bado yanakaliwa na ambayo hayajawa mahame kamwe. Masoko ya Aleppo ni miongoni mwa masoko yanayopendeza zaidi huko Mashariki ya Kati.

Kusini kidogo ya Aleppo kuna eneo la Tell Mardikh, jiji la kale la Ebla lililokuwa na utawala wake. Ebla lilikuwa jiji kuu la biashara kaskazini mwa Siria kuanzia mwaka wa 2,600 K.W.K. hadi 2,240 K.W.K. hivi. Mabaki ya hekalu la Ishtar, mungu wa kike wa Babiloni, yamefukuliwa hapo. Mabamba ya udongo 17,000 yalipatikana wakati jumba la mfalme lilipofukuliwa. Vitu vilivyopatikana Ebla vimo katika jumba la makumbusho la Idlib, mji mdogo ulio umbali wa kilometa 25 kutoka eneo hilo.

Ukielekea kusini kwenye barabara ya Damasko utafika kwenye jiji la Hama, ambalo liliitwa Hamathi nyakati za Biblia. (Hesabu 13:21) Mto Orontes unapita Hama kwa kupinda-pinda, kwa hiyo jiji hilo ni mojawapo ya majiji ya Siria yenye kuvutia zaidi. Kisha unafika Ras Shamra, ambapo jiji la kale la Ugarit lilikuwa. Ugarit lilikuwa bandari ya biashara iliyositawi sana kuanzia mwaka wa 1400 hadi 1200 K.W.K. hivi, na wakazi wengi waliabudu Baali na Dagoni. Tangu mwaka wa 1929, wanaakiolojia Wafaransa wamefukua mabamba mengi ya udongo na sanamu za shaba ambazo zinafunua mengi juu ya ibada ya Baali iliyopotoka. Jambo hilo linatusaidia kuelewa vizuri ni kwa nini Mungu aliagiza Wakanaani walioabudu Baali waangamizwe.—Kumbukumbu la Torati 7:1-4.

Ndiyo, huko Siria ya sasa bado kuna mabaki yanayofunua mengi kuhusu historia yake yenye kupendeza.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 12 Ona makala “Bibi Mwenye Nywele Nyeusi wa Jangwa la Siria,” katika gazeti la Mnara wa Mlinzi la Januari 15, 1999, lililochapishwa na Mashahidi wa Yehova.

[Ramani katika kurasa za 24, 25]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

BAHARI YA MEDITERANIA

‐‐ Mipaka inayobishaniwa

MISRI

ISRAELI

YORDANI

LEBANONI

SIRIA

DAMASKO

Barada

Orontes

Hama (Hamathi)

Ugarit (Ras Shamra)

Ebla (Tell Mardikh)

Aleppo (Haleb)

Karkemishi (Jerablus)

Eufrati

Zenobia

Dayr az Zawr

Dura-Europos

Mari

Palmyra (Tadmori)

IRAKI

UTURUKI

[Picha katika ukurasa wa 24]

Damasko (chini) na Barabara Nyoofu (juu)

[Picha katika ukurasa wa 25]

Nyumba za matope huko Sirouj

[Picha katika ukurasa wa 25]

Ugarit

[Picha katika ukurasa wa 25]

Hama

[Picha katika ukurasa wa 26]

Mari

[Picha katika ukurasa wa 26]

Aleppo

[Hisani]

© Jean-Leo Dugast/Panos Pictures

[Picha katika ukurasa wa 26]

Jumba la mfalme huko Ebla

[Picha katika ukurasa wa 26]

Wachungaji huko Zenobia

[Picha katika ukurasa wa 26]

Palmyra

[Picha katika ukurasa wa 26]

Eufrati unapita Dura Europos

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]

Children: © Jean-Leo Dugast/Panos Pictures; beehive homes: © Nik Wheeler