Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuzoa Chumvi Baharini kwa Kutumia Jua na Upepo

Kuzoa Chumvi Baharini kwa Kutumia Jua na Upepo

Kuzoa Chumvi Baharini kwa Kutumia Jua na Upepo

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UFARANSA

KWENYE ufuo wa bahari, vidimbwi vingi vinang’aa vikibadilika rangi kulingana na tofauti za hali ya anga. Mwanamume mmoja anasimama kando ya vidimbwi hivyo vyenye umbo la mstatili na kukusanya chumvi nyingi kutoka baharini na kuiweka kwenye marundo madogo meupe yanayometameta kwenye mwangaza wa jua. Katika eneo hili la Guérande na kwenye visiwa vya Noirmoutier na Ré, katika Pwani ya Atlantiki, mbinu za kale za kuzoa chumvi zingali zinatumiwa.

“Dhahabu Nyeupe”

Kuzoa chumvi katika mashimo ya Pwani ya Atlantiki kulianza karibu miaka ya 200 W.K. Lakini uzoaji huo ulianza kupamba moto mwishoni mwa miaka ya 1400. Ongezeko la idadi ya watu huko Ulaya wakati huo lilifanya kuwe na uhitaji mkubwa wa chumvi, kwa kuwa ilitumiwa kuhifadhi nyama na samaki. Kwa mfano, tani nne za samaki aina ya heringi zilihifadhiwa kwa kutumia tani moja ya chumvi. Watu wa kawaida hawangeweza kununua nyama, hivyo samaki waliohifadhiwa kwa chumvi waliliwa kwa ukawaida. Kwa hiyo, meli kutoka sehemu zote za kaskazini mwa Ulaya zilikuja kwenye ufuo wa Brittany kununua chumvi nyingi ambayo wavuvi walihitaji ili kuhifadhi samaki.

Kiasi kikubwa cha pesa kilichotokana na ‘dhahabu hiyo nyeupe’ hakikukosa kujulikana na wafalme wa Ufaransa. Mnamo mwaka wa 1340, ushuru wa chumvi ulioitwa kwa Kiarabu gabelle, ulianzishwa. Ushuru huo haukupendwa na wengi, hivyo mapigano mengi yenye umwagaji wa damu yalizuka. Mgogoro ulitokea kwa sababu wanunuzi walilazimika kununua kiasi kidogo kilichoamuliwa cha chumvi kwa bei ghali bila kujali mahitaji yao. Pia, watu wenye mapendeleo ya pekee, kama wale wenye vyeo na viongozi wa dini, walisamehewa kulipa kodi hiyo. Mikoa mingine, kutia ndani Brittany, haikuhitajika kulipa kodi, na mingine ililipa tu robo ya kiasi kilichotakiwa. Jambo hilo lilileta tofauti kubwa katika bei za chumvi, huku mikoa fulani ikilipa mara 40 zaidi ya mingine.

Haishangazi kwamba katika hali hizo magendo ya chumvi yaliongezeka. Hata hivyo, waliokamatwa wakifanya magendo hayo waliadhibiwa vikali. Wangetiwa alama kwa chuma chenye moto, kutumiwa katika meli za watumwa, au hata kuhukumiwa kifo. Mwanzoni mwa miaka ya 1700, karibu robo ya wafungwa waliokuwa katika meli za watumwa walishikwa kwa sababu ya kufanya magendo ya chumvi. Wengine walikuwa wahalifu wa kawaida, wanajeshi watoro, au Waprotestanti waliokuwa wakinyanyaswa baada ya kufutiliwa mbali kwa Amri ya Nantes. * Mageuzi ya mwaka wa 1789 yalipoenea nchini Ufaransa, mojawapo ya madai ya kwanza lilikuwa kuondolewa kwa ushuru wa chumvi ambao ulichukiwa sana.

Kuzoa Chumvi kwa Kutumia Jua

Kwa muda wa karne nyingi, mbinu ya kuzoa chumvi katika Pwani ya Atlantiki ya Ufaransa haijabadilika sana. Chumvi huzolewaje? Katika miezi ya baridi, wazoaji hurekebisha mahandaki ya udongo wa mfinyanzi na mitaro katika ufuo wenye mchanganyiko mzito wa chumvi na kutayarisha mashimo ambamo chumvi huzolewa. Wakati wa joto, mchanganyiko huo hukaushwa kwa jua, upepo na upeo wa maji kwenye ufuo. Maji ya bahari huingia katika dimbwi la kwanza yanapojaa ufuoni, maji hayo hutulia na kuanza kukauka. Halafu maji huelekezwa polepole kwenye vidimbwi mbalimbali ambamo huendelea kukauka. Maji yanapozidi kupungua, na chumvi kukolea zaidi na zaidi, mimea midogo ya mwani hunawiri na kuyafanya maji hayo yawe mekundu kwa muda mfupi. Mimea hiyo inapokauka chumvi huwa na harufu ndogo nzuri ya maua ya urujuani. Maji huwa yamekolea chumvi sana yanapoingia katika shimo la chumvi, hufikia kiasi cha gramu 260 za chumvi kwa lita moja kutoka gramu 35 kwa lita moja.

Kwa kuwa mchanganyiko huo unaweza kuharibika kwa urahisi, haiwezekani kuzoa chumvi kwa kutumia mashine, kama inavyofanywa huko Salin-de-Giraud na Aigues-Mortes, katika pwani ya Mediterania. Mzoaji hutumia kifaa chenye mkono mrefu kinachofanana na reki kuzoa chumvi, naye huwa mwangalifu asizoe pia udongo wa mfinyanzi ulio chini ya shimo hilo lenye kina kifupi. Chumvi hiyo yenye rangi ya kijivu-nyeupe kwa sababu ya udongo wa mfinyanzi, huachwa ikauke. Kwa wastani, mzoaji mmoja anaweza kuzoa karibu mashimo 60 kwa mwaka, na kila moja ya mashimo hayo hutoa karibu tani moja na nusu ya chumvi kwa mwaka.

Chini ya hali fulani, chumvi laini hujikusanya juu ya maji kama vipande vya barafu. Aina hiyo ya chumvi si nyingi kama chumvi inayotoka baharini kila mwaka, lakini inatumiwa sana katika mapishi ya Kifaransa.

Bila shaka, mambo yote hayo hutegemea mabadiliko ya hali ya hewa. Mtu mmoja aliyefanya biashara ya chumvi hapo awali alisema: “Sisi huathiriwa na hali mbaya ya hewa. Kwa mfano, katika mwaka wa 1950, mvua ilinyesha sana katika msimu wa joto. Tulipata kiasi kidogo sana cha chumvi.” Pascal, mzoaji kutoka Guérande, anasema: “Mnamo mwaka wa 1997, nilizoa tani 180 za chumvi ya mawe na tani 11 za chumvi laini. Mwaka huu [1999], hali ya hewa haikuwa nzuri. Nilipata tani 82 tu.” Kwa kushangaza, matokeo hayawi mazuri wakati wa joto kali sana, kwa kuwa maji ya chumvi huwa moto sana na fuwele hazitokei.

Uhaba na Wingi

Katika miaka ya 1800, maendeleo ya viwanda yalipunguza uhitaji wa chumvi ya Pwani ya Atlantiki. Chumvi ya Mediterania yenye bei nafuu ilijaa kwenye masoko kwa sababu usafiri uliimarika. Zaidi ya hilo, hewa ya Mediterania huruhusu uzoaji ufanywe mwaka mzima ambapo zaidi ya tani milioni moja na nusu huzolewa kwa mwaka. Pamoja na hayo, kufikia miaka ya 1970, chumvi kidogo sana ilipatikana katika Pwani ya Atlantiki na uzoaji ulielekea kukoma kabisa.

Lakini katika miaka ya majuzi, “dhahabu nyeupe” imeanza tena kuwa maarufu kama awali. Mambo yamebadilika kadiri watu wanavyozidi kufahamu umuhimu wa kuhifadhi mazingira na umuhimu wa kiuchumi wa fuo zenye chumvi. Mimea aina mbalimbali na ndege-wahamaji hupatikana katika maeneo hayo salama ambayo sasa yametambuliwa na kulindwa.

Isitoshe, fuo hizo zenye shughuli za kikale ambazo hazijaathiriwa na mvurugo wa kisasa huwavutia watalii wanaotafuta utulivu usio na hekaheka za maisha. Pia tunaishi kipindi cha wakati ambacho watu wanahangaikia uchafuzi wa mazingira na ubora wa chakula. Wanapenda chakula cha kiasili ambacho hakijatiwa kemikali au kutengenezwa viwandani. Ingawa ulimwengu umeunganishwa kwa njia za mawasiliano na kuna mashindano makali ya kibiashara, bado wazoaji-chumvi wa Ufaransa wanahitajiwa, pamoja na kazi ya kuzoa chumvi ambayo imedumu kwa miaka mingi.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 7 Ona toleo la Agosti 15, 1998, la Mnara wa Mlinzi, ukurasa wa 25-29, lililochapishwa na Mashahidi wa Yehova.

[Sanduku katika ukurasa wa 22]

CHUMVI NA AFYA YAKO

Imedaiwa kwamba kula chakula chenye chumvi nyingi husababisha kupanda kwa shinikizo la damu, ambalo huchangia ugonjwa wa moyo. Kwa hiyo, wataalamu wa tiba hupendekeza kiasi kisichozidi gramu sita kwa siku.

Hata hivyo, uchunguzi wa hivi majuzi umeonyesha kwamba kupunguza kiasi cha chumvi hakuelekei kupunguza kupanda kwa shinikizo la damu na hakuathiri sana watu wenye shinikizo la kawaida la damu. Uchunguzi uliochapishwa katika gazeti la Lancet, la Machi 14, 1998, ulionyesha kwamba watu wanaokula chakula chenye chumvi yenye sodiamu kidogo hupata ugonjwa wa moyo mara nyingi zaidi kuliko wale wanaotumia kiasi cha kawaida cha sodiamu. Uchunguzi huo ulimalizia kwa kusema kwamba “wale wanaokula chakula chenye sodiamu kidogo hupata madhara zaidi kuliko faida.” Makala katika gazeti Canadian Medical Association Journal (CMAJ) la Mei 4, 1999, ilisema kwamba “watu wenye shinikizo la kawaida la damu hawapaswi kuzuiwa kutumia chumvi sasa, kwa sababu hakuna ushuhuda wa kutosha unaoonyesha kwamba jambo hilo linapungunza ugonjwa wa moyo.”

Je, hilo linamaanisha kwamba mtu hapaswi kuhangaikia kiasi cha chumvi ambacho anatumia? Kama ilivyo na masuala yote yanayohusu chakula, jambo muhimu zaidi ni kuwa na kiasi. Makala iliyotajwa hapa juu CMAJ inapendekeza kwamba watu wasitumie chumvi nyingi sana, wasitie chakula chumvi nyingi jikoni na wajaribu kuepuka kuongeza chumvi mezani. Hata hivyo, ikiwa una shinikizo la juu la damu au matatizo ya moyo, fuata maagizo ya daktari wako.

[Ramani katika ukurasa wa 21]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Guérande

ÎLE DE NOIRMOUTIER

ÎLE DE RÉ

[Picha katika ukurasa wa 22]

“Fleur de sel”

[Picha katika ukurasa wa 22]

Mji wa Île de Ré

[Picha katika ukurasa wa 23]

Kuzoa chumvi laini

[Picha katika ukurasa wa 23]

Fuo zenye chumvi na viwekeo vyake

[Picha katika ukurasa wa 23]

Mzoaji wa chumvi huko Noirmoutier

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 21]

© Cliché Bibliothèque nationale de France, Paris

[Picha katika ukurasa wa 23]

Juu: Index Stock Photography Inc./Diaphor Agency; kushoto: © V. Sarazin/CDT44; katikati na kulia: © Aquasel, Noirmoutier