Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Yurumí anastaajabisha

Yurumí anastaajabisha

Yurumí anastaajabisha

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI ARGENTINA

KUNA giza katika makao yao ya chini ya ardhi, na jamii hiyo inajitahidi kufa na kupona kujiokoa kutokana na shambulizi. Maaskari walinzi wanakimbia kwenye eneo la hatari wakiwa wamejihami kwa silaha, zijapokuwa duni. Kufumba na kufumbua, sehemu kubwa ya ngome yao yaanguka, na wakazi wengi wanapondwa na vifusi. Mvamizi aingia kupitia ufa uliofanyizwa ngomeni huku mwangaza mkali ukipenya.

Je, maelezo hayo yanafafanua shambulizi dhidi ya jiji fulani katika siku za Waroma? Au, je, yanafafanua onyesho fulani katika sinema ya kusisimua? Hata kidogo! Badala yake, yanafafanua shambulizi la yurumí, na hivyo ndivyo wadudu wanavyoliona. Hata hivyo, yurumí, au mnyama huyo anayekula mchwa, anafanya tu ziara zake za kawaida za kuvamia vichuguu vya mchwa.

Maumbile ya Yurumí

Ijapokuwa kuna aina mbalimbali za walaji hao wa mchwa, tutazungumzia hasa mnyama mmoja ambaye katika lugha nyingine huitwa pia dubu anayekula mchwa. Ama kwa hakika, mnyama huyo si dubu hata kidogo, lakini huenda alipewa jina hilo kwa sababu ya mtindo wake wa kutembea kwa kujikokota na vilevile jinsi anavyosimama wima anapolazimika kujilinda. Pia, yeye “humkumbatia” mvamizi kwa miguu yake ya mbele yenye nguvu, kama dubu afanyavyo.

Huko kaskazini-mashariki mwa Argentina na katika nchi jirani, mnyama huyo huitwa yurumí, jina la Kiguarani linalomaanisha “mwenye mdomo mdogo.” Jina hilo lafaa kwani mdomo wake ni mdogo sana hata ingawa utaya wake ni mrefu sana. Mdomo wake ambao ni kama mrija ni mojawapo ya viungo vyake vinavyotambulika kwa urahisi. Pia, yurumí ana mkia mrefu wenye manyoya mengi, naye huusimamisha wima nyakati nyingine. Manyoya yaliyo kwenye mkia wake huwa marefu zaidi, na hivyo kumfanya aonekane mzito sana na kumbe sivyo. Japo ana umbo la kustaajabisha, mnyama huyo ni mkubwa tu kama mbwa wa aina fulani. Yurumí aliyekomaa kabisa anaweza kuwa na uzani wa kilogramu 25. Lakini mnyama huyo anaweza kukua kufikia urefu wa meta 1.8 au zaidi kutoka mdomoni hadi kwenye ncha ya mkia wake.

Mnyama huyo huishi peke yake, akitangatanga hasa katika maeneo yenye vinamasi huko Amerika Kusini. Mara nyingi watu huhusianisha bara hilo na mimea mingi na vilevile misitu ya mvua yenye miti mingi. Lakini eneo hilo pia lina sehemu kubwa kavu zenye nyasi na zilizo tambarare na vilevile mitende na vichaka vya miti yenye miiba hapa na pale. Udongo wa eneo hilo una mbolea nyingi za mimea na unawafaa kabisa mchwa. Wadudu hao hutengeneza vichuguu vyao kwa udongo na mate—mchanganyiko unaofanya jengo hilo liwe thabiti sana. Vichuguu hivyo vikubwa vinaweza kufikia zaidi ya meta 1.8 kwenda juu.

Yurumí huishi mahali penye wadudu hao wengi, naye hupenda kuwala. Hivyo, jina la kisayansi la mnyama huyo Myrmecophaga tridactyla linaonyesha kwanza zoea lake la kula mchwa, na pili, linaonyesha muundo wa vidole vyake vya miguu kwani vidole vitatu kati ya vidole vyake vinne vya kila mguu wa mbele vina kucha kali zilizojipinda. Kichapo Enciclopedia Salvat de la fauna chasema hivi: “Kucha hizo ni za kuwinda na kujilinda: Anapovamiwa, mnyama anayekula mchwa huzitumia kama visu vikali, huku akijinyanyua kwa miguu yake ya nyuma kwa ustadi sana hivi kwamba zinaweza kusababisha majeraha makubwa na hata kuwatimua mbio wanyama aina ya jaguar.”

Yurumí Hulaje?

Yurumí hana meno. Hata hivyo, hilo halimzuii, kwani ana maumbile ya kustaajabisha sana yanayomwezesha kupata mlo. Kwanza, ana uwezo mkali wa kunusa—unaozidi ule wa wanadamu kwa mara 40—naye huutumia kutafuta chakula. Kisha yeye hutumia nyayo zake za mbele, ambazo zina kucha zenye urefu wa sentimeta 10, kuchimba vichuguu akitafuta wadudu, mabuu, au mayai. Akiisha kufanya hivyo, yeye huingiza ulimi wake mwembamba wenye urefu wa sentimeta 45 katika vijia vilivyo ndani ya vichuguu hivyo.

Mnyama huyo ana tezi kubwa za mate ambazo hufanyiza mate yanayonata na kuufanya ulimi wake uwe majimaji na wenye kunata. Sisimizi au mchwa hukwama kwenye ulimi na kutumbukizwa mdomoni mwake. Lakini kuwameza wadudu hao hakutoshi. Ni lazima wadudu hao wameng’enywe. Jambo la kustaajabisha ni kuwa misuli ya tumbo ya mnyama huyo ina nguvu sana hivi kwamba inaweza kuwasaga wadudu hao.

Ni Nini Kitakachompata Yurumí?

Ijapokuwa wanyama hao wanapatikana katika sehemu nyingi za Amerika ya Kati na ya Kusini, wao si wengi sana. Yaonekana hawazai sana. Yurumí wa kike huzaa mtoto mmoja tu baada ya kubeba mimba kwa siku 190 hivi. Mtoto anapozaliwa, mamake humbeba mgongoni kwa mwaka mmoja. Mtaalamu mmoja wa viumbe huko Argentina anasema jambo fulani la kupendeza kuhusiana na hilo: “Nilikutana na mama mmoja na mtoto wake aliyezaliwa juzijuzi. Haikuwa rahisi kumwona mtoto huyo mdogo aliyebebwa mgongoni, na niligundua kwamba hakuonekana kwa urahisi kwa sababu alibebwa mahali pa pekee ambapo mstari mweusi mgongoni mwake ulipita barabara juu ya mstari mweusi ulio mgongoni mwa mamake. Hivyo, ndege wanaowinda hawangeweza kumwona kwa urahisi.”

Yurumí ni muhimu sana katika mazingira anamoishi. Yurumí mmoja hula makumi ya maelfu ya sisimizi au mchwa. Kama yurumí hangekuwapo, je, inawezekana kwamba wadudu hao wangeongezeka na kusababisha maafa? Iwe ndivyo ama sivyo, ukweli ni kwamba hali hiyo inabadilika. Kwa nini?

Kwa kusikitisha, mnyama huyo ameanza kutoweka pole kwa pole kwa sababu ya shughuli za wanadamu. Watu wengine huwawinda ovyoovyo; wengine huwaua eti kwa sababu wanafikiri kwamba wanaashiria mabaya. Isitoshe, wengine huwakamata ili kuwauzia watu wanaokusanya viumbe wasiopatikana kwa urahisi, na wanyama hao huishia kufungiwa vizimbani au kwenye majumba ya ukumbusho—wakiwa wamekaushwa. Je, yurumí ataangamia kabisa? Tunasubiri kuona yatakayotukia. Kwa sasa jitihada zinafanywa ili kulinda kiumbe huyo mwenye thamani.

[Picha katika ukurasa wa 15]

Anatafuta mchwa

[Picha katika ukurasa wa 15]

“Yurumí” mchanga anabebwa mgongoni na mamake

[Picha katika ukurasa wa 15]

Ulimi wenye kustaajabisha wa “yurumí” wenye urefu wa sentimeta 45

[Hisani]

Kenneth W. Fink/Bruce Coleman Inc.