Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Meli Zenye Nguvu Zinazotoa Msaada

Meli Zenye Nguvu Zinazotoa Msaada

Meli Zenye Nguvu Zinazotoa Msaada

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI FINLAND

NDEGE wanaoitwa shakwe wanaruka katika anga jangavu. Jua limewaka kwelikweli. Mbegu za kahawa zanukia. Kisha, milango inafungwa, ving’ora vinalia, na meli iliyojaa mizigo yaanza safari polepole. Shehena ya mbegu za kahawa inasafirishwa kwenda Finland, nchi yenye watu wanaopenda sana kahawa. Hata hivyo, majuma machache baadaye, wakati wa majira ya baridi kali, meli hiyo iliyobeba magunia ya mbegu za kahawa inaelekea kukwama kwenye barafu katika Bahari ya Baltiki. Ni hatua gani inayoweza kuchukuliwa? Hakuna haja ya kubabaika kwani msaada upo. Meli nyingine yenye nguvu yaonekana ikija—ni meli ya kuvunja barafu.

Kuvunja Barafu

Mizigo mingi ulimwenguni husafirishwa kupitia bahari. Kwa kawaida, hilo si tatizo. Lakini meli zinawezaje kufika bandarini kunapokuwa na barafu baharini? Hilo ni tatizo kubwa hasa katika Bahari ya Baltiki yenye utendaji mwingi, kwani nchi nyingi huitumia kama njia ya kufika kwenye bahari kuu. Kwa mfano, wakati wa baridi kali sana, bandari nyingi za Finland haziwezi kufikika kwa sababu ya barafu, na bandari zilizo kaskazini kabisa zinaweza kuzungukwa na barafu kwa muda wa miezi sita. Hilo limesababisha vifo.

Mnamo 1867, mavuno yalikuwa haba kaskazini na katikati mwa Ulaya. Kwa sababu ya barafu, haingewezekana kufika Finland kupitia baharini hadi mwezi wa Mei. Hivyo, misaada haingeweza kupelekwa huko hadi wakati ambapo barafu ingeyeyuka. Katika kitabu Through Ice and Snow, nahodha Seppo Laurell anasema hivi: “Kufikia wakati huo, watu wapatao 110,000, au zaidi ya asilimia tano ya idadi ya watu [huko Finland], walikuwa wamekufa njaa.”

Barafu huzuia usafirishaji wa mizigo katika sehemu nyinginezo pia. Katika Amerika Kaskazini tatizo hilo hutokea mara nyingi katika yale Maziwa Makuu, Mto St. Lawrence, na karibu na pwani ya Kanada. Ni vigumu hata zaidi kusafiri katika bahari za Aktiki na Antaktiki kunapokuwa na barafu wakati wa baridi kali. Huko, barafu hufikia kina cha meta mbili hadi tatu kwa wastani.

Jinsi Barafu Ilivyovunjwa Hapo Kale ili Kupata Njia

Wakati meli zilipoendeshwa kwa tanga, bahari yenye barafu ilitokeza tatizo kubwa sana. Meli za chuma zilizoendeshwa kwa mvuke zilipotokea, hali ikawa afadhali. Iwapo meli ya kubeba mizigo ingekuwa yenye nguvu vya kutosha, ingeweza kupita palipo na tabaka jembamba la barafu. Lakini, meli hizo hazingeweza kupita katika sehemu fulani, licha ya kwamba nyingine zilikuwa zimeundwa kwa njia ya pekee kukabili barafu.

Meli za kuvunja barafu zilipoundwa, tatizo hilo lilisuluhishwa. Inasemekana kwamba meli ya kwanza ya kuvunja barafu iliitwa City Ice Boat I, iliyoundwa huko Marekani mwaka 1837. Meli kama hiyo iliundwa pia huko Ulaya mwaka 1871 katika mji wa Hamburg, Ujerumani, nayo iliitwa Eisbrecher. Baada ya muda, ilibainika wazi ni meli zipi ambazo zingeweza kukabiliana vema na barafu. Basi, karne ya 20 ilipoanza, miundo fulani maalumu ndiyo iliyokuwa ikitumiwa. *

Meli Kubwa za Chuma

Inakuwaje meli inapokwama kwenye barafu? Baharia mmoja anaeleza hivi: “Meli hutetemeka kama mtu aliye na homa kali.” Kiunzi cha meli ya kuvunja barafu hushinikizwa mara nyingi zaidi kuliko kiunzi cha meli ya kusafirisha bidhaa. Mtu mmoja anayefanya kazi ya kuvunja barafu anasema hivi: “Kugonga barafu ni kama kugonga ufuo wa bahari kwa motaboti.” Mabamba ya chuma yaliyo kwenye sehemu ya mbele ya meli hizo yanaweza kuwa na upana wa zaidi ya milimeta 30—na kwenye meli za kuvunja barafu katika maeneo yenye baridi sana yanaweza hata kuwa na upana wa milimeta 50—na mbali na mataruma ya kawaida, mengine yameongezwa katika sehemu ya katikati ili kukabili barafu. Meli hizo zina nguvu kadiri gani? Wakati wa Vita ya Pili ya Ulimwengu, meli ya kuvunja barafu inayoitwa Tarmo iligongwa kwa bomu lililoharibu sitaha na vyumba vingi vya meli hiyo, lakini kiunzi cha meli hiyo hakikupata ufa wowote.

Kiunzi cha meli hizo kinapasa kuwa na umbo linalofaa. Mara nyingi kazi ngumu zaidi si kuvunja barafu bali ni kuondoa njiani vipande vya barafu vilivyovunjika. Sehemu ya mbele ya meli nyingi za kuvunja barafu huwa na umbo la kijiko, bila ncha kali. Kwa kutumia uzito wa kiunzi, meli hizo huvunja barafu na kusukuma vipande vya barafu kando na chini. Umbo la kiunzi hutengenezwa ipasavyo ili kupunguza msuguano kati ya meli na barafu. Isitoshe, kiunzi hicho hufunikwa kwa chuma cha pua au rangi fulani iliyo laini sana na yenye kudumu.

Meli hizo kubwa huendeshwaje? Siku hizi watu hawahitaji kuwasha makaa ili kuendesha injini. Meli za kisasa za kuvunja barafu hutumia dizeli, na nishati inayoendesha rafadha zake ni sawa na ile ya meli za wastani za kubebea mafuta. Nyingine huendeshwa kwa mitambo ya nyuklia ambayo huziwezesha zitumiwe katika maeneo yenye baridi sana bila wasiwasi wa kuishiwa mafuta.

Muundo wa Kipekee

Mtumbwi wa makasia unapokwama matopeni, huenda mpiga makasia akautikisa huku na huku ili usonge mbele. Kanuni hiyohiyo hutumiwa katika meli za kuvunja barafu. Hata hivyo, meli hizo haziwezi kutikisika hata kikosi chote cha mabaharia wapatao 30 wakijaribu kuzitikisa. Meli hizo hutikiswa kwa kuzifanya ziegemee upande mmoja—maji husukumwa huku na huku katika matangi mawili makubwa, tangi moja likiwa upande mmoja wa kiunzi na tangi jingine upande mwingine. Kwa kushangaza, kazi hiyo yaweza kuchukua sekunde 15 tu! Mtu ambaye hajazoea kusafiri baharini anaweza kuwa na wasiwasi mwingi anapowazia jinsi ambavyo meli huyumbayumba. Ama kweli, mabaharia ni watu waye ustadi.

Kufikia mwishoni mwa karne ya 19, mtu fulani alifikiria kuweka rafadha katika sehemu ya mbele. Rafadha iliposonga, maji yalipunguza msuguano na kuondoa barafu njiani. Baadhi ya meli za kisasa za kuvunja barafu zina rafadha mbili nyuma, na rafadha moja au mbili mbele. Hata hivyo, meli nyingi za kuvunja barafu hutumia mfumo ambao unatokeza mapovu kwa kushinikiza hewa. Mifereji iliyowekwa chini ya kiunzi huingiza hewa nyingi iliyoshinikizwa ndani ya maji yaliyo chini ya barafu. Hivyo, mapovu mengi hufanyizwa na kupunguza msuguano.

Kutazama Mbali

Ijapokuwa meli tisa kubwa za kuvunja barafu nchini Finland hushindwa kuvunja barafu kwenye bandari zote, jua linalochomoza wakati wa majira ya kuchipua huondoa barafu kabisa hata kwenye bandari zilizo kaskazini kabisa mwa nchi hiyo. Meli hizo hurudishwa bandarini, na mabaharia wanaoziendesha hupumzika wakati wa kiangazi. Meli hizo za bei ghali na za kipekee hazitumiwi kwa miezi kadhaa kwa sababu hazikuundwa zitumiwe wakati ambapo hakuna barafu.

Hata hivyo, kuna meli nyingine mpya za kuvunja barafu. Meli hizo hutumiwa kuvunja barafu wakati wa baridi kali kisha wakati ambapo hakuna barafu, zinaweza kutumiwa kuweka nyaya kwenye sakafu ya bahari, kufanya utafiti, na kurekebisha visima vya mafuta vilivyo baharini. Meli moja ya aina hiyo, inayoitwa Botnica, iliundwa mnamo 1998 ili itumiwe na Idara ya Usimamizi wa Bahari ya Finland nayo ina rafadha mbili zinazozunguka kikamili. Hivyo, rafadha hizo hutumiwa pia kama rada. Rafadha hizo huwezesha meli hizo ziendeshwe kwa urahisi sana. Muundo huo umetumiwa pia katika meli za kisasa za abiria.

Kutokana na maendeleo ya mbinu za kuvunja barafu, meli mpya ya kubeba mizigo inabuniwa. Meli hiyo itakapokuwa ikisonga mbele, itakata mawimbi kama kawaida. Hata hivyo, sehemu ya nyuma itatumiwa kuvunja barafu. Meli hiyo mpya itakuwa yenye faida kubwa katika maeneo yenye baridi sana, ambako mara nyingi meli za kuvunja barafu hazipatikani kwa urahisi. Meli hiyo itaweza kupita barafuni kwa kusonga kinyumenyume.

Kwa sasa, ile meli iliyokuwa imebeba kahawa inangojewa kwa hamu huko Finland. Meli ya kuvunja barafu iliyotajwa katika fungu la kwanza la makala hii imeondoa barafu njiani na sasa inavuta meli iliyokuwa imekwama. Nahodha wa meli ya kuvunja barafu aegemea kwenye chuma kilicho kwenye sitaha bila wasiwasi wowote. Kisha anaelekea jukwaa ya kuendeshea meli. Ni wakati wa kunywa kahawa moto.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 10 Meli za kuvunja barafu hutofautiana kwa ukubwa na muundo, ikitegemea mahali ambapo zinatumiwa—iwe ni bandarini, katika bahari kuu, au katika maeneo yenye baridi sana. Makala hii inazungumzia hasa meli zinazotumiwa katika bahari kuu.

[Picha katika ukurasa wa 25]

Meli ya kuvunja barafu inayoitwa “Otso” inaondoa barafu njiani

[Hisani]

Idara ya Usimamizi wa Bahari ya Finland

[Picha katika ukurasa wa 25]

Meli ya mvuke ilikwama barafuni—wapata mwaka wa 1890

[Hisani]

Museovirasto

[Picha katika ukurasa wa 26]

Meli ya Urusi inayoitwa “Taymyr” inayoendeshwa kwa mitambo ya nyuklia

[Hisani]

Kværner Masa-Yards

[Picha katika ukurasa wa 26]

Meli za kisasa za kuvunja barafu zinaweza pia kutumiwa kuweka nyaya na mabomba kwenye sakafu ya bahari

[Hisani]

Idara ya Usimamizi wa Bahari ya Finland

[Picha katika ukurasa wa 26]

Meli ya “Botnica”

[Hisani]

Idara ya Usimamizi wa Bahari ya Finland