Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Tazama! Gwaride la Pengwini Wadogo

Tazama! Gwaride la Pengwini Wadogo

Tazama! Gwaride la Pengwini Wadogo

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AUSTRALIA

UMATI umenyamaza kimya ukiwa na matarajio makubwa. Wote wanakodoa macho ili waone watumbuizaji hodari wakiingia. Ghafla huku taa zikimulika, kiumbe mdogo anaonekana akitoka majini. Watu wanashangilia kiumbe wa pili na wa tatu watokeapo. Tamasha hiyo ya usiku imeanza. Tazama! Gwaride la Pengwini wadogo katika Kisiwa cha Phillip. *

Pengwini walianza kujulikana ulimwenguni kote wakati wavumbuzi maarufu Vasco da Gama na Ferdinand Magellan walipovuka bahari kuu za kusini katika miaka ya 1500. Mwanzoni wanadamu hawakujua pengwini angekuwa katika kikundi gani cha viumbe. Alikuwa na manyoya kama ndege; aliogelea kama samaki, na kutembea katika nchi kavu kama mnyama. Manyoya ndiyo yaliyowasaidia kusuluhisha suala hilo. Ni ndege tu walio na manyoya, hivyo iliamuliwa kuwa pengwini ni ndege. Kuna aina 18 za ndege hao wasioruka kutia ndani stately emperor, Adélie wa Antaktika, na Galápagos wa maeneo ya Ikweta.

Je, ungependa kutembelea makao ya kiasili ya pengwini? Hebu tembelea Kisiwa cha Phillip, kilichoko kilometa 140 kusini-mashariki mwa jiji la kisasa la Melbourne, Australia. Watu wapatao 500,000 hutembelea kisiwa hicho kila mwaka ili waone viumbe hao wadogo wa ajabu. Ni nini ambacho huwafanya pengwini wa Kisiwa cha Phillip wavutie sana?

“Maridadi, na Wenye Nguvu”

Mtu yeyote huvutiwa na pengwini wadogo wenye manyoya ya rangi nyeupe na nyeusi. Pengwini hao ndio wadogo zaidi ulimwenguni wakiwa na urefu wa sentimeta 33 na uzito wa kilogramu moja. Lakini, usipumbazwe na udogo wao! Pengwini hao ni jasiri na wavumilivu sana.

“Pengwini wadogo ni maridadi na wenye nguvu,” aeleza Profesa Mike Cullen, aliyewachunguza pengwini wa Kisiwa cha Phillip kwa zaidi ya miaka 20. Pengwini hao wadogo ndio wenye kelele zaidi. Wakiwa katika makao yao usiku, pengwini hao hunguruma, hulia, huwika, na kutoa sauti ya mkwaruzo ili kulinda viota vyao kutokana na uvamizi wa wale wanaoingilia makao yao, kutafuta wenzi, au kufurahia kuimba pamoja.

Pengwini wadogo walipotambuliwa kwa mara ya kwanza katika mwaka wa 1780, waliitwa kwa Kigiriki Eudyptula minor, maana yake “mpiga-mbizi mdogo mzuri.” Kwa kuwa wana umbo la ndege inayobeba abiria, manyoya laini yasiyopenya maji na mabawa yanayowawezesha kuogelea kwa haraka, wao huonekana kama wanaruka juu ya maji.

Kinga Nzuri ya Ndani

Pengwini wanaweza kuogelea kilometa 100 kwa siku wakitafuta chakula, na kukaa baharini kwa siku kadhaa au majuma kadhaa ikihitajika. Wao hulalaje baharini? Manyoya yao ya ajabu ndiyo ambayo huwawezesha kufanya hivyo. Pengwini wana manyoya mengi yanayoangalia chini na yaliyoshikamana. Manyoya hayo yanazidi uzito wa ndege warukao mara tatu au mara nne. Kama vazi ambalo huvaliwa ili kumzuia mtu asizame na kufa maji, hewa ambayo hubanwa ndani ya manyoya hayo humzuia asizame. Kwa hiyo, pengwini aweza kulala baharini, akielea juu ya maji kama kitu chepesi, huku mikono yake ikinyooshwa ili awe thabiti, na mdomo wake ukibaki salama juu ya maji.

Bila shaka, kama manyoya ya pengwini yangelowa maji, angezama katika maji baridi ya bahari anapotafuta chakula. Pengwini hutatua tatizo hilo kwa kutoa umajimaji wenye nta kutoka kwa tezi ya kipekee iliyo chini ya mkia wake. Yeye hutumia mdomo wake kuipaka nta hiyo katika mabawa yake na hivyo kuyasafisha, kuzuia maji yasipenye, na kuyadumisha katika hali nzuri. Hakuna mpiga-mbizi mwenye mavazi mazuri kama hayo ya kumwezesha akabiliane na hali za baharini.

Je, kiumbe huyu anayeishi baharini hutatizwa na maji ya chumvi? Tezi zake mbili zenye muundo wa pekee juu ya kila jicho, hutoa chumvi kutoka kwa maji. Kwa kutikisa mdomo wake tu, pengwini huondoa chumvi hiyo kupitia pua lake.

Isitoshe, macho ya pengwini humwezesha kuona vizuri akiwa ndani ya maji kama akiwa katika nchi kavu. Ni wazi kwamba kiumbe huyo ana vifaa vinavyomwezesha kuishi majini. Hata hivyo, tunafurahi kwamba pengwini wadogo hawakai majini nyakati zote.

Kuishi Katika Nchi Kavu

Ufuo wa Kisiwa cha Phillip na nchi iliyo karibu si laini, na una mchanga uliofunikwa na nyasi na majani mengi. Hayo ni makao mazuri kwa pengwini wadogo 26,000. Wazazi wa pengwini huchimba mashimo katika mchanga huo wa pwani. Yai lililotagwa karibuni huachwa kwa muda mfupi, lakini likiwa salama, kabla ya wazazi wote wawili kuanza kulilalia kwa zamu. Ndege anayelalia yai hutokeza uvimbe chini ya tumbo lake, wenye mishipa mingi ya damu. Anapolalia yai, uvimbe huwa mkubwa na kupasha joto yai ili lianguliwe. Wakati ndege mmoja halalii yai, uvimbe wake hupungua ili kumruhusu kutia nta katika manyoya yake na kutafuta chakula baharini.

Baada ya kuanguliwa, kifaranga hukua haraka sana. Kwa majuma manane hadi kumi tu, pengwini mchanga huwa mkubwa kama pengwini wengine waliokomaa na huwa tayari kwenda baharini. Kitabu Little Penguin—Fairy Penguins in Australia chasema: “Jambo la ajabu ni kwamba utendaji katika mwili wa pengwini wachanga . . . pamoja na silika zao nyingi huwasaidia kuishi baharini kwa muda mrefu.”

Kwa muda wa mwaka mmoja hadi mitatu baadaye, pengwini hao wachanga wanaweza kusafiri maelfu ya kilometa, wakitumia wakati mwingi baharini. Mara nyingi wale ambao huhimili hurudi nyumbani—angalau umbali wa meta 500 kutoka mahali wao wenyewe walipozaliwa. Wao hujuaje njia ya kurudi nyumbani? Watu fulani husema kwamba pengwini wana saa ya asili ambayo huenda sawia na jua. Wengine wanaamini kwamba pengwini hutambua ishara fulani njiani mwao. Vyovyote vile, kuwatazama ndege hao wakirudi katika nchi kavu baada ya safari yao ndefu au baada ya kazi ngumu ya uvuvi ni jambo ambalo huwavutia watu wengi katika Kisiwa cha Phillip.

Gwaride Linaanza!

Baada tu ya jua kutua, mamia ya wageni wenye furaha wanaketi ili watazame gwaride la pengwini. Pengwini tayari wamejipanga karibu na ufuo wa bahari katika vikundi vikubwa vyenye mamia ya ndege. Taa nyingi zinamulika ufuoni. Upepo mwanana unavuma, na mawimbi madogo yanapiga ufuo. Watazamaji wanaanza kuwa na wasiwasi. Pengwini wako wapi? Je, watakuja kweli? Ghafula, pengwini wachache wanatokea wakipigapiga maji kwa woga ukingoni. Wanashtuka ghafula na kurudi majini. Wanatahadhari sana wasionekane na maadui, kama tai. Muda si muda wanatokea tena na pole kwa pole wanakuwa jasiri. Mwishowe, ndege mmoja jasiri anatoka majini kwa ukakamavu na kuelekea katika mapango yao. Wengine katika kikundi wanamfuata haraka. Wote wanaelekea ufuoni, kana kwamba wanapanga gwaride, bila kujali mwangaza wala watazamaji.

Baada ya kufika katika eneo la usalama kwenye mashimo, pengwini wanastarehe na kukusanyika katika vikundi vikubwa zaidi na kuanza kupaka manyoya yao nta. Kikundi kimoja baada ya kingine kinafuata mtindo huo, huku pengwini wakisimama ili “kuzungumza” na majirani kabla ya kuingia mapangoni. Wengine hutembea, na kupanda miamba yenye urefu wa meta 50 kabla ya kufika makwao.

Pengwini Wadogo —Masuala Makubwa

Kama wanyama wengine, pengwini wadogo wanakabili matatizo mbalimbali, na mengi yameletwa na binadamu. Hayo ni pamoja na mafuta yanayomwagwa baharini na meli zinazopita, upungufu wa maeneo ya kuishi kwa sababu ya shughuli za binadamu, na maadui ambao wameletwa kutoka mbali, kama mbweha na wanyama wengine wa kufugwa.

Jitihada zimefanywa ili kusuluhisha matatizo hayo. Katika miaka ya hivi majuzi, pengwini wadogo katika Hifadhi ya Pengwini ya Kisiwa cha Phillip wameongezeka. “Tunatatua tatizo hilo . . . ingawa polepole,” anaeleza Profesa Cullen. Anaongeza kusema: “Tatizo kubwa zaidi tunalokabili sasa ni kupata chakula cha pengwini wadogo . . . , na hilo linategemea bahari na binadamu kwa ujumla.” Ongezeko la joto duniani na badiliko la hali ya hewa, kama vile mkondo wa El Nino, huathiri kiasi cha chakula baharini na kutokeza matatizo makubwa ambayo watafiti wanachunguza kwa makini sana.

Bila shaka, matokeo ya uchunguzi huo yataongeza uthamini wetu kwa sayari yetu tata na yenye unamna-namna wa viumbe. Kutokana na jitihada za kuwatunza wanyama katika Kisiwa cha Phillip, huenda siku moja uwe pia miongoni mwa watazamaji wanaosema kwa sauti za chini, “Tazama! Gwaride la pengwini wadogo.”

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 3 Mara nyingi pengwini wadogo huitwa pengwini wadogo wa bluu.

[Ramani katika ukurasa wa 15]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

KISIWA CHA PHILLIP

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Watazamaji, viti, na taa—kila kitu kiko tayari kwa ajili ya gwaride la pengwini

[Picha katika ukurasa wa 17]

Kinda huwa amekua kabisa baada ya majuma kumi tu

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]

Photo: Photography Scancolor Australia

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]

Photos on pages 16 and 17: Photography Scancolor Australia