Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

“Ndoto za Kutajirika”

Matangazo motomoto ya kibiashara yamewapotosha watu wengi maskini kuamini kwamba wanaweza kuwa matajiri wakicheza kamari, ingawa uwezekano wa kushinda donge nono la pesa ni mdogo sana, laripoti gazeti la Times of Zambia. Gazeti hilo lilisema kwamba “matangazo ya kamari huwafanya watu wawe na ndoto za kutajirika, kuishi maisha ya anasa na yasiyo na matatizo,” hata hivyo “hayataji uwezekano mkubwa wa kutoshinda.” Gazeti hilo lamalizia hivi: “Hata mtu asemeje, kucheza kamari ni wizi wa wazi na unapaswa kupigwa marufuku katika jamii yoyote yenye maadili.”

Wanaogopa Giza

Ripoti moja katika gazeti la The Times la London inasema kwamba “watoto huogopa giza zaidi ya jinsi wazazi wao walivyoliogopa walipokuwa watoto kwa sababu wamezoea taa na mara nyingi hawajikuti katika giza tititi.” Mwandishi na mtaalamu wa akili, Aric Sigman, alichanganua utafiti unaoonyesha kwamba thuluthi mbili hivi ya watoto wenye umri usiozidi miaka 10 husisitiza kulala taa ikiwa imewaka. Anadai kwamba kutozoea giza kunadhoofisha uwezo wa watoto wa kufikiri—hata wanapokuwa kitandani usiku. “Uwezo wa watoto wa kufikiri unapaswa kusitawishwa,” yasema ripoti hiyo. “Watoto wanaweza kusisimuka sana wakicheza gizani, kwa sababu watawazia mambo ya pekee sana.” Lakini leo, “mambo ambayo yametia mizizi kwenye akili za watoto kutoka kwenye televisheni, sinema na michezo ya kompyuta” yanawatisha. Dakt. Sigman anasema hivi: “Kuwaambia watoto waache kutazama televisheni kwa muda mrefu na badala yake wasome sana ni kama kutoa shauri la kizamani, lakini tunahitaji kulirudia-rudia.”

Mwamba wa Barafu wa Antaktika Wavunjika

Kwa siku 35, kuanzia mwishoni mwa Januari 2002, kipande cha mwamba wa barafu wa Larsen B chenye ukubwa wa kilometa 3,250 ambacho kiko upande wa mashariki wa Rasi ya Antaktika, kilivunjika na kusambaza maelfu ya miamba ya barafu baharini, charipoti Kituo cha Kitaifa cha Kuhifadhi Habari za Theluji na Barafu Kwenye Chuo Kikuu cha Colorado. Sehemu kubwa ya Antaktika imezungukwa na miamba mikubwa ya barafu, lakini miamba iliyo kwenye rasi imekuwa ikiyeyuka kwa sababu ya kuongezeka kwa joto tangu mwishoni mwa miaka ya 1940. Kuvunjika kwa mwamba huo hakutazidisha maji baharini kwa sababu miamba hiyo ya barafu inaelea. Hata hivyo, ripoti hiyo yasema kwamba “miamba ya barafu huzuia barafu kubwa inayoteleza kutoka milimani. Miamba hiyo inapoondolewa, huenda barafu hiyo . . . ikajaa baharini badala ya kufanyiza theluji.” Bado haijulikani ni nini kinachosababisha kuongezeka kwa joto, na habari hiyo inaweza kutatanisha. Gazeti la The New York Times linasema kwamba “hakuna dalili zinazoonyesha kwamba sehemu nyinginezo za Antaktika zimeathiriwa na joto” isipokuwa rasi hiyo. Hata utafiti fulani unaonyesha kwamba huenda kipimo cha joto kwenye bara hilo lote kilipungua katika muda wa miaka 35 iliyopita.

Mradi wa China wa Kupeleka Vyombo Angani

Mnamo Aprili 1, 2002, chombo cha angani cha China kisichoendeshwa na mtu kiitwacho Shenzhou III, kilitua katika eneo la Inner Mongolia baada ya kukaa angani kwa juma moja, laripoti Shirika la Utangazaji la BBC. Chombo hicho kilikuwa na “sanamu ya mwanadamu”—iliyokuwa na vifaa vya kupima oksijeni na hali ya joto katika majaribio ya kuona iwapo wanadamu wataweza kuishi katika mazingira hayo wakati ujao wanaposafiri angani. Wataalamu wa mambo ya angani huko China wametangaza kwamba wana mradi wa kumsafirisha mwanadamu angani angalau kufikia mwaka wa 2005. Ripoti hiyo yasema kwamba “shirika la China la vyombo vya angani limejiwekea mradi wa kumsafirisha mwanadamu kwenye Mwezi kufikia mwaka wa 2010.”

Chiriku wa Manjano Huvutiwa na Rangi Nyangavu

Chiriku wa manjano au kasuku mdogo humchaguaje mwenzi? Huenda anavutiwa na rangi nyangavu ya manyoya yake. Manyoya ya chiriku hao huwa na kemikali fulani ambayo hufyonza miale ya jua na kufanya manyoya hayo yenye rangi manjano-nyekundu yang’ae sana. Dakt. Justin Marshall wa Chuo Kikuu cha Queensland, Australia, pamoja na wafanyakazi wenzake waliwapaka chiriku wa porini mafuta ya kuzuia miale ya jua kupenya manyoya yao na kuyafanya yasing’ae. Gazeti la The Sydney Morning Herald laripoti kwamba “ndege wenye manyoya yasiyong’aa hawakuwavutia wale wa jinsia tofauti.” Marshall alisema kwamba labda ndege wanaong’aa sana wana afya bora. Ingawa miili ya viumbe wengine inaweza kuwa na kemikali zinazofanya wawe na rangi nyangavu, Marshall alisema kwamba hilo ndilo “jaribio la kwanza la kuchunguza umuhimu wa viumbe kuwa na rangi nyangavu,” lasema gazeti la Herald.

Simba Wamo Hatarini

Gazeti la New Scientist linaripoti kwamba “huenda simba wakatoweka hivi karibuni katika sehemu nyingi za Afrika.” Simba 500 hadi 1,000 wanahitajiwa ili kupata wenzi 100 hivi wanaoweza kuzaana—na kuepuka simba wa ukoo mmoja wasizalishane. Shirika la Kuhifadhi Viumbe Ulimwenguni linasema kwamba idadi ya simba katika Afrika Magharibi na ya Kati haifikii idadi hizo. “Hiyo ni hali mbaya sana,” asema Hans Bauer wa Chuo Kikuu cha Leiden huko Uholanzi. “Hakuna jamii ya simba tunayoweza kuwa na hakika kwamba itaendelea kuwapo.” Idadi ya simba imepungua hasa kwa sababu wanadamu wameingilia mazingira yao. Simba huhitaji maeneo makubwa sana ya kuwinda—dume mmoja anahitaji eneo lenye ukubwa wa kilometa 200 za mraba. “Simba ni mnyama muhimu sana,” aonya Bauer. “Kuhatarishwa kwa simba sasa kunaonyesha kwamba huenda wanyama wengine watakuwa katika hatari ya kutoweka baada ya miaka 20 hadi 30.”

Kitanda Kinachotoa Miale ya Jua Ni Hatari

Gazeti The Guardian la London linaripoti kwamba “uwezekano wa watu wanaotumia kitanda kinachotoa miale ya jua kupata kansa ya ngozi ni mara mbili zaidi ya wale wasiokitumia, na vijana ndio wanaokabili hatari kubwa zaidi.” Profesa Margaret Karagas, wa Chuo cha Kitiba cha Dartmouth, New Hampshire, Marekani, aliwahoji watu 1,500 wenye umri wa miaka 25 hadi 74, na zaidi ya nusu ya watu hao walikuwa na kansa ya ngozi. Uwezekano wa kupata kansa uliongezeka “kufikia asilimia 20 kwa kila miaka kumi ambayo mtu alitumia kitanda kinachotoa miale ya jua kabla ya umri wa miaka 50,” lasema gazeti la The Times of London. Profesa Karagas anasema: “Taa zinazogeuza rangi ya ngozi nyeupe hutoa mwangaza kama wa jua lakini [wenye] miale mikali sana ya mnururisho.” Hivi sasa idadi ya watu wanaokufa kutokana na kansa ya ngozi nchini Uingereza ni mara tatu zaidi ya ilivyokuwa miaka ya 1960, na idadi ya wanaokufa nchini Scotland imeongezeka mara nne. Wataalamu wanasema kwamba watu hao walikufa kwa sababu ya miale hiyo yenye mnururisho kutoka kwa jua au taa zenye miale ya mnururisho. “Huwezi kugeuza rangi ya ngozi yako kwa miale ya jua bila madhara,” akasema msemaji wa Kituo cha Utafiti wa Kansa nchini Uingereza. “Ngozi hubadilika rangi hasa kwa sababu ya kuharibika kwa chembe za DNA.”

“Minara ya Maji” Imo Hatarini

Asilimia 50 ya watu ulimwenguni hutegemea maji safi kutoka milimani, lasema gazeti la The Toronto Star la Kanada. Milima hiyo ambayo inaitwa “minara ya maji ulimwenguni” katika ripoti ya Umoja wa Mataifa ya kuadhimisha Mwaka wa Milima wa UM, imo hatarini. Gazeti la Star linasema kwamba uharibifu huo unasababishwa na “mabadiliko ya hali ya hewa, uchafuzi, vita, ongezeko la watu, ukataji wa misitu kwa ajili ya shughuli za kilimo, uchimbaji wa madini, na utalii.” Kulingana na gazeti hilo, ripoti hiyo inaonya kwamba “uharibifu huo utasababisha mafuriko zaidi, maporomoko ya ardhi na njaa.”

Walevi wa Kupindukia

Gazeti la The Independent la London, linasema kwamba mtu mmoja kati ya watu 13 nchini Uingereza ni mlevi wa kupindukia, hivyo unywaji wa kupindukia wa pombe “umeenea maradufu zaidi ya utumiaji sugu wa dawa za kulevya na dawa za kitiba.” Kuanzia mwaka wa 1994 hadi 1999, watu waliokufa kwa sababu ya kuwa walevi wa kupindukia—kutia ndani wale waliokufa kutokana na ugonjwa wa moyo, uvimbe wa ini, na sumu inayosababishwa na pombe—waliongezeka kwa karibu asilimia 43. Misiba ya barabarani iliyosababishwa na madereva walevi iliongezeka kutoka 10,100 mwaka wa 1998 hadi 11,780 mwaka wa 2000, na ilisababisha kifo cha mtu 1 kati ya vifo 7 vilivyotokea barabarani. Asilimia 60 ya waajiri wanasumbuliwa na wafanyakazi walevi, na asilimia 40 ya wahalifu wajeuri huwa walevi. Eric Appleby, mkurugenzi wa Taasisi Inayoshughulikia Masuala ya Vileo Nchini Uingereza, alisema hivi: “Matatizo hayo yanaathiri sana afya ya watu, mahusiano na hali ya kiuchumi, na vilevile huduma za jamii, . . . hivyo kuna uhitaji wa kuungana bila kukawia ili kupambana nayo.”