Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Kuna Matumaini Yoyote ya Kupata Amani?

Je, Kuna Matumaini Yoyote ya Kupata Amani?

Je, Kuna Matumaini Yoyote ya Kupata Amani?

“Leo ni kama tunaishi . . . katika kimbunga, katika dhiki kubwa sana.”—Gazeti “La Repubblica” la Roma, Italia.

BAADA ya mashambulizi ya kigaidi huko New York City na Washington, D.C. mwaka uliopita, watu wengi hawana uhakika kuhusu wakati ujao wa wanadamu. Picha za televisheni zinazoonyesha yale Majengo Mawili yakiporomoka na kuteketea—na hali ya kukata tamaa ya waokokaji—zimeonyeshwa mara nyingi. Picha hizo zimewahuzunisha sana watu duniani pote. Zaidi ya hilo, inadhaniwa kuwa hali ulimwenguni zimebadilika sana. Je, ni kweli?

Vita ilizuka punde tu baada ya Septemba 11, 2001. Mataifa yaliyokuwa na uadui hapo awali yalianza kushirikiana ili kukomesha ugaidi. Watu wengi wamekufa na mali nyingi zimeharibiwa. Lakini, huenda tatizo kubwa linalowakabili watu wengi duniani pote ni kujihisi hawako salama haidhuru wanaishi wapi.

Viongozi ulimwenguni wanakabiliana na matatizo makubwa. Waandishi na wachanganuzi wa habari hawaoni kukiwa na njia yoyote ya kuzuia ugaidi unaoenea haraka, kwa sababu inaonekana kwamba unasababishwa na umaskini na ushupavu—matatizo ambayo inaonekana hakuna mtu anayeweza kuyatatua. Ukosefu wa haki umeenea sana ulimwenguni hivi kwamba unaweza kusababisha maafa makubwa. Watu wa jamii zote wanajiuliza kama maovu ya kijamii yatakwisha. Je, vita—inayosababisha mateso, kifo, na uharibifu—itakoma?

Mamilioni ya watu sasa wanageukia dini mbalimbali ili kupata majibu ya maswali hayo. Wengine hawajui la kufanya. Namna gani wewe? Je, unafikiri viongozi wa kidini wanaweza kujibu maswali hayo? Je, maombi yao yataleta amani?