Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Balolo—“Chakula Kitamu cha Pasifiki”

Balolo—“Chakula Kitamu cha Pasifiki”

Balolo—“Chakula Kitamu cha Pasifiki”

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI FIJI

JE, UNAPENDA vyakula vya baharini? Ikiwa ndivyo, jiunge nasi tunapotembelea kijiji kimoja kilicho kwenye mojawapo ya visiwa vya nchi ya kitropiki ya Fiji, ambako tutafurahia karamu ya kipekee. Tunasikia mawimbi yakipigapiga mitumbwi, na tunaona joko la chini ya ardhi, linaloitwa lovo, ambalo limechimbwa karibu na ufuo. Moto umewashwa ili kupasha joto mawe maalumu yaliyoteuliwa, na chakula kikuu kitapikiwa hapo.

Lakini ni nani atakayeleta chakula hicho? Hakitaletwa na mtu fulani! Badala yake, chakula hicho kitajileta. Iwapo tayari umegundua kwamba chakula hicho ni cha kiajabu, basi hujakosea. Chakula hicho tunachotarajia kwa hamu ni minyoo yenye ladha tamu! Minyoo hiyo ya baharini yenye rangi nyekundu-kahawia (minyoo ya kiume) na rangi ya bluu-kijani (minyoo ya kike) imeitwa chakula kitamu cha Pasifiki. Huku katika Visiwa vya Fiji, chakula hicho cha kipekee na kitamu huitwa balolo. *

Mara moja au mbili kwa mwaka, mwezi unapoanza awamu ya tatu ya kuzunguka dunia, minyoo mingi sana ya balolo huelea baharini kwa jioni moja au tatu. * Haieleweki kikamili jinsi ambavyo minyoo hiyo huzaana kwa wingi kwa wakati barabara hivyo, lakini wanasayansi wanaamini kwamba huenda tukio hilo linahusiana na halijoto za bahari zinazoongezeka, sura za mwezi, kujaa na kupwa kwa maji, au urefu wa mchana. Dalili za wakati barabara wa tukio hilo zaweza kuonekana kwa kuchunguza hali ya hewa, mimea fulani inapochanua maua, na hali mbalimbali za bahari. Hivi karibuni, wanabiolojia wa mambo ya bahari wametabiri wakati barabara ambapo minyoo hiyo itazaana kwa kutegemea sura za mwezi na ule mzunguko unaochukua muda wa miaka 19.

Kule kijijini, nyimbo zinazoimbwa kwa kufuatana na ala ya ukulele na gitaa, zinakatizwa na tangazo la kwamba minyoo imeanza kuelea baharini. Hebu tujiunge na wanaume, wanawake, na watoto wanaokwenda kwenye miamba ya bahari. Baadhi yao wamevaa vazi la isulu lenye rangi nyangavu (shuka la kufungwa kiunoni ambalo huvaliwa na wanaume na wanawake) na shada la maua maridadi lenye manukato linaloitwa salusalu. Watu hao wamevalia maridadi hata ingawa wataingia baharini.

Baadhi yao wanaamua kushiriki katika tukio hilo wakiwa ndani ya mtumbwi, lakini sisi tunaamua kujiunga na kikundi cha watu wanaoogelea kutoka ufuoni. Muda si muda, maji hayo ya kitropiki yenye joto yanatufika viunoni. Kwa ghafula, tunazungukwa na maelfu kwa maelfu ya minyoo!

Sasa tunasisimuliwa na tukio ambalo limeitwa “mojawapo ya matukio ya asili yenye kustaajabisha zaidi Kusini mwa Pasifiki.” Viumbe hao wanaojinyonga-nyonga mwili wanakamatwa kwa njia yoyote ile wanapoelea baharini—kwa ndoo, nyavu ndogo, vyandarua, vikapu vilivyofumwa kwa majani ya minazi, na hata mikono mitupu. Mgeni mmoja alimwona mwanamume Mfiji mwenye nywele matimutimu akiingiza kichwa chake ndani ya maji kisha akakitikisa-tikisa ndani ya mashua ili kuondoa minyoo iliyoshika nywele zake! Washiriki wengine wenye bidii wanatafuna-tafuna minyoo hiyo bila huruma wanapoendelea kuikusanya.

Muda unayoyoma na tukio hilo la kustaajabisha linamalizika—hadi mwaka mwingine tena. Badala ya kula minyoo mibichi, tunaamua kujiunga na rafiki zetu walio ufuoni ili tuonje ‘chakula hicho kitamu cha Pasifiki’ baada ya kutayarishwa ndani ya joko la chini ya ardhi. Chakula hicho kina vitamini na madini tele, nacho chaweza kuchemshwa, kuokwa, au kukaangwa. Kikiisha pikwa, chakula hicho chaweza kukaa kwa juma moja au zaidi bila kuharibika. Hata hivyo, tunatambua kwamba watu wengine hawatafurahia ladha yake ya samaki.

Ni wakati wa kuondoka, nasi tunawashukuru wanakijiji kwa sababu ya kutukaribisha kwa uchangamfu kisiwani. Tunapofikiria tena jinsi ambavyo minyoo ya balolo huelea baharini kwa wakati barabara, na jinsi ambavyo viumbe wote katika miamba hiyo ya bahari hutegemeana, tunastaajabishwa na Muumba wa taratibu hizo tofauti-tofauti za uhai.—Ufunuo 4:11.

Iwapo unapanga kutembelea Visiwa vya Fiji, huenda ungependa kuonja chakula kitamu kilichotayarishwa kutokana na minyoo hiyo. Kwa upande mwingine, huenda ukapenda kula vyakula vya kwenu! Vyovyote iwavyo, uwe na hakika kwamba wakati minyoo ya balolo inapotokea, wakazi hao wa kisiwani watakuwa wakisubiri kuibuka kwa ‘chakula hicho kitamu cha Pasifiki.’

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 4 Katika lugha nyingine, kutia ndani Kiingereza, chakula hicho huitwa jina la Kisamoa palolo.

^ fu. 5 Tukio kama hilo hutukia pia katika sehemu nyinginezo katika maeneo ya kusini na magharibi mwa Pasifiki, kutia ndani Visiwa vya Cook, Samoa, Visiwa vya Solomon, Tonga, na Vanuatu. Zaidi ya hayo, inaripotiwa kwamba minyoo mingine ya jamii hiyohiyo huibuka kwa wingi katika sehemu nyingine za ulimwengu, kutia ndani kwenye Visiwa vya Malay, Ghuba ya Mexico, Karibea, na Japan.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 11]

Je, Kweli Wanakula Minyoo?

Huenda ukashangaa na kustarehe kujua kwamba harakati hiyo ya kuvua haitukii kama inavyodhaniwa. Hebu ona sababu zinazoeleza jambo hilo.

Mkia wa mnyoo wa balolo hubadilika na kukua haraka kuwa viungo vya uzazi vinavyoitwa epitoke. Viungo hivyo vina chembe za uzazi zinazoitwa gameti. Mkia wa mnyoo, ambao una macho na miguu, hujitenganisha na mnyoo na kuelea baharini. Mikia hiyo isipovuliwa na mtu mwenye njaa au kuliwa na kiumbe mwingine wa baharini, itapasuka na kutoa mayai na shahawa, kisha vitu hivyo vitakutana “ghafula” kwa njia ya kustaajabisha. Mikia hiyo huwa mingi sana na hilo huwezesha minyoo mingi kuzalishwa hata ingawa inavuliwa na wanadamu na kuliwa na wanyama. Mikia inayosalia ikiwa mabuu huogelea hadi kwenye matumbawe ambako inaanza mzunguko wa maisha.

Hivyo, tunapokula balolo, sisi hula tu mikia ya minyoo ambayo inaishi kwenye matumbawe.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 10]

Juu: Sekove Bigitibau; kushoto, katikati, na kwenye ukurasa wa 11: Paul Geraghty