Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

“Aliye Mdogo Zaidi Ulimwenguni”

“Mjusi aliye mdogo zaidi ulimwenguni,” mwenye urefu wa sentimeta mbili tu, amegunduliwa katika mapango ya Mbuga ya Kitaifa ya Jaragua huko Jamhuri ya Dominika. “Hatari kubwa inayomkabili ni kuishiwa maji kwa sababu sehemu yake ya juu ni kubwa sana ukilinganisha na uzani wake,” laripoti gazeti The Times la London. “Mnyama huyo si mjusi mdogo tu bali pia ni mdogo zaidi kati ya aina 23,000 za wanyama wanaotia ndani wanyama wanaonyonyesha watoto, ndege, na wanyama watambaazi.” Mnyama wa pili kwa udogo ni mjusi mwenzake kutoka Visiwa vya Virgin vya Uingereza vilivyo karibu na Jamhuri ya Dominika. Gazeti hilo laongeza: “Visiwa hivyo vya Karibea pia vina ndege mdogo zaidi ulimwenguni, Ndege-Mvumaji, mwenye urefu wa sentimeta 5, na nyoka mwembamba zaidi aina ya Lesser Antillean Threadsnake, anayeweza kuingia katika tundu la kalamu iwapo risasi ya kuandikia ingeondolewa.”

Matabiri Yasiyotimia Kamwe

“Watabiri, wanajimu, na wabashiri walishindwa kabisa tena mwaka wa 2001,” lasema gazeti Süddeutsche Zeitung la Ujerumani. Wataalamu katika taasisi moja ya Ujerumani walifikia mkataa huo walipochunguza matokeo ya matabiri ya mwaka huo. Kwanza, hakuna mtabiri hata mmoja aliyetabiri mashambulizi ya Septemba 11 au vita huko Afghanistan. Pia, hawakutabiri kuzorota kwa uchumi huko Ujerumani, badala yake walikuwa na matumaini makubwa kuhusu wakati ujao. Mtabiri mmoja alisema kijasiri kwamba katika mwaka wa 2001, ulimwengu ungeingia katika “kipindi cha amani.” Ingawa mara chache matabiri ya binadamu hutimia, hakuna awezaye kusema kwa usahihi ni yapi yatakayotimia, lasema gazeti hilo likiongeza: “Hata hivyo, kuna uthibitisho wa kutosha kwamba wanadamu huelekea kukosea mara nyingi.”

Ujinga Mkubwa Sana wa Kutega Mabomu ya Ardhini

“Ulimwenguni kote kuna mabomu yaliyofukiwa ardhini [milioni] 110. Kuyategua mabomu hayo kutagharimu dola [bilioni] 33 za Marekani na kuchukua miaka 1,100 iwapo jitihada ya sasa itaendelea,” lasema gazeti The Guardian la Uingereza. “Mabomu hayo yanategwa kwa haraka sana, mara 25 kuliko yanavyoweza kuteguliwa,” na tangu mwaka wa 1975, zaidi ya watu milioni moja wameuawa au kulemazwa nayo—kutia ndani watoto 300,000. Nusu ya watu wazima na zaidi ya nusu ya watoto wanaokanyaga mabomu hayo hufa kabla ya kufikishwa hospitalini. “Mara nyingi wanajeshi hawarekodi mahali ambapo mabomu yametegwa au hawaweki rekodi za mabomu hayo,” laongeza gazeti hilo, na mabomu mengi “hupelekwa na maji kutoka mahali yalipotegwa hadi mahali pengine ambapo hapakuwa na mabomu.” Ingawa biashara ya kimataifa ya mabomu ya ardhini inakaribia kukoma, bado mabomu milioni 230 hadi milioni 245 yamehifadhiwa duniani kote. Kulingana na Kampeni ya Kimataifa ya Kupiga Marufuku Mabomu ya Ardhini, serikali 15 na mashirika ya magaidi na makundi ya wapiganaji wa kuvizia 30 bado wanatumia mabomu hayo.

Vipepeo-Maliki Taabani

Dhoruba kubwa ya mvua ya Januari, iliyofuatwa na hali ya hewa baridi sana, imeharibu vikundi viwili vikubwa zaidi vya vipepeo-maliki huko Mexico. Kama ilivyoripotiwa katika gazeti The New York Times, watafiti walikadiria kuwa “asilimia 74 ya vipepeo hao wa kikundi cha Sierra Chincua na asilimia 80 wa kikundi cha Rosario walikufa. Vipepeo wa vikundi hivyo pamoja na vingine vidogo vichache, . . . ndio wanaozaa huko Marekani na Kanada.” Vipepeo milioni 220 hadi milioni 270 waliganda na kuanguka kutoka mitini na kufunika ardhi hadi kina cha zaidi ya sentimeta 30 katika sehemu fulani. Ingawa watu wengine wanaona kwamba vifo hivyo havitishii kumaliza viumbe hao, watafiti hao walisema kwamba upungufu huo utawafanya vipepeo hao waathiriwe zaidi wakati ujao na hali mbaya ya hewa na magonjwa. Vipepeo hao wanajulikana sana kwa msafara wao wenye kuvutia kutoka Mexico kuelekea kaskazini kila majira ya kuchipua. Wao hutaga mayai kusini mwa Marekani, ambayo huangua vipepeo zaidi na kuendeleza msafara huo, hadi Kanada wakati wa kiangazi.

“Sahihi na ya Kishairi”

Biblia ni ya “kweli na sahihi zaidi kuliko ilivyodhaniwa,” lasema gazeti la Ufaransa la mambo ya kiasili Terre sauvage. Wataalamu wa mambo ya kiasili waliona kuwa, ingawa Biblia ni kitabu cha kidini, ina “maelezo sahihi kuhusu wanyama.” Makala hiyo ilisema kwamba vitabu vya “Zaburi na Mithali vina habari muhimu” kwa wataalamu wa mambo ya kiasili, na kuongeza kwamba: “Kitabu cha Ayubu . . . kinaeleza kwa njia sahihi na ya kishairi kuhusu maisha ya mbuzi-mwitu na makao ya punda-mwitu na kiboko.”

“Wenzi Wasiofaana”

“Uhusiano wowote kati ya simba-jike na choroa ungetarajiwa kuwa mfupi, na choroa angeliwa na simba,” lasema gazeti The Economist. Hata hivyo, picha iliyoandamana na makala hiyo ilionyesha simba-jike na choroa mchanga wamelala pamoja kwa amani. Makala hiyo iliendelea: “Wenzi hawa wasiofaana walionwa katika mbuga ya Samburu nchini Kenya mnamo Desemba 21, na wakafuatiliwa na kupigwa picha na . . . wapiga-picha wawili, hadi simba mwingine alipomuua choroa huyo Januari 6.” Nyakati nyingine mnyama wa kike aliyezaa majuzi anaweza kumkubali mtoto wa mnyama mwingine ili kumnyonyesha na kumlea. Je, hivyo ndivyo ilivyokuwa katika kisa hicho? Haionekani kuwa hivyo, lasema gazeti hilo. “Kinacholifanya tukio hilo liwe tofauti ni kwamba mamake choroa huyo alikuwa bado hai na alinyonyesha, naye simba-jike alikuwa mchanga na hakuwa na dalili zozote za kuwahi kuzaa.” Zaidi ya hiyo, “simba-jike ndiye aliyemfuata choroa huyo mdogo (kwa mfano alipoenda kunyonya mamake), wala choroa hakumfuata simba-jike.” Makala hiyo ilimalizia kusema: ‘Sababu alitaka kumlea mnyama aliyepaswa kumla ni fumbo.’

Wanyama-Vipenzi Walioachwa

“Australia ina wanyama-vipenzi wengi kwa kila mtu nchini kuliko nchi nyingine ulimwenguni,” anasema Hugh Wirth, msimamizi wa kitaifa wa Shirika la Kitaifa la Kuzuia Ujeuri Dhidi ya Wanyama. Hata hivyo, gazeti The Australian linaripoti kuwa “wanyama-vipenzi 135,000 waliachwa katika mwaka wa kifedha wa 2000-2001,” na kwamba “karibu asilimia 60 ya wanyama hao waliuawa.” Kwa nini wanyama wengi hivyo waliachwa? Sababu moja ilikuwa ni kutochagua wanyama-vipenzi vizuri. Mara nyingi wazazi huwanunulia watoto wao mbwa wanaohitaji kufundishwa, kuzoezwa, na kuhudumiwa sana. Pia, mbwa hao ndio huwauma watu mara nyingi. Gazeti The Australian lasema hivi kuhusu kuchagua mnyama-kipenzi: “Usimnunue kwa kusukumwa na hisia tu. Fikiria nafasi, hali za familia yako na hali yako ya kifedha. Usikawie kumzoeza mbwa kutii. Kadiri unavyokawia kumzoeza, ndivyo anavyoendelea kuwa mtundu. Kumbuka kwamba kuwa na mbwa ni mradi wa muda mrefu.”

Maradhi Yanayotokana na Gari Jipya

“Uchunguzi . . . umeonyesha kuwa hewa ndani ya magari mapya yaliyonunuliwa miezi sita iliyopita ina sumu nyingi,” lasema Shirika la Utafiti wa Sayansi na Viwanda la Australia (CSIRO). Hewa hiyo ina benzene, acetone, ethylbenzene, n-hexane, toluene, na xylene isomer—ambazo ni hatari kwa binadamu. Waendeshaji wanaovuta hewa hiyo huumwa na kichwa, husinzia, huchanganyikiwa, na macho, pua, na koo zao huwasha. Kulingana na Dakt. Steve Brown, msimamizi wa utafiti kuhusu ubora wa hewa wa CSIRO, “ndani ya gari unaweza kuvuta hewa yenye sumu nyingi zaidi ya vipimo vilivyoruhusiwa na Baraza la Australia la Kitaifa la Utafiti kuhusu Afya na Tiba.” Ili kupunguza hatari, Brown anapendekeza kwamba ikiwezekana waendeshaji wa magari mapya “wahakikishe kuna hewa ya kutosha kutoka nje inayoingia garini wanapoendesha, kwa angalau miezi sita baada ya gari kununuliwa.”