Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Nywele Zako Zinakuhangaisha?

Je, Nywele Zako Zinakuhangaisha?

Je, Nywele Zako Zinakuhangaisha?

HUENDA wewe kama watu wengine wengi husimama mbele ya kioo kila siku ukichunguza nywele zako. Wanaume na wanawake hupendezwa na nywele zao, lakini nyakati nyingine zinaweza kuwahangaisha.

Jifunze Juu ya Nywele Zako

Unajua una nywele ngapi kichwani mwako? Kwa wastani 100,000. Kila unywele huendelea kukua kwa miaka miwili hadi miaka sita tu. Kisha unywele huo hutoka, na baada ya muda unywele mwingine unaanza kukua katika kitundu hichohicho. Mfuatano huo hujirudia tena na tena. (Ona sanduku kwenye ukurasa wa 27.) Kwa sababu ya mfuatano huo, nywele 70 hadi 100 huanguka kwa ukawaida kila siku, hata mtu asipokuwa na tatizo la nywele.

Kwa nini kuna rangi mbalimbali za nywele? Kitabu The World Book Encyclopedia kinasema hivi: “Rangi ya nywele inatokana hasa na rangi ya asili ya kahawia-nyeusi inayoitwa melanin.” Rangi hiyo iko katika nywele, ngozi, na macho. Kiwango cha rangi hiyo ndicho kinachoamua rangi ya nywele. Ikiwa rangi hiyo ni nyingi nywele zitakuwa nyeusi zaidi. Na kwa kupatana na kiwango cha rangi hiyo nywele zinaweza kuwa nyeusi, kahawia, nyekundu, au manjano. Ikiwa nywele hazina rangi yoyote ya melanin, zitakuwa nyeupe kabisa.

Mbali na mba, yaani, vipande vidogo-vidogo vya ngozi vinavyobambuka kichwani, watu wengi huhangaishwa na kutokwa kwa nywele au mvi.

Je, Una Mvi?

Nywele za kijivu-jivu huonwa mara nyingi kuwa dalili ya kuzeeka. Na kwa kawaida nywele nyeupe huonwa kuwa za wazee. Ni kweli kwamba nywele huzidi kuwa nyeupe mtu anapozeeka. Hata hivyo, mbali na kuzeeka, mambo mengine, kama vile kujinyima chakula ili kupunguza unene, yanaweza kusababisha mvi. Wanaume na wanawake huota mvi nazo hutokea katika nywele za kila rangi ijapokuwa zinaonekana wazi zaidi katika nywele nyeusi.

Nyakati nyingine watu wengine wenye mvi huonwa kuwa wazee ijapokuwa hawana umri mkubwa sana na jambo hilo linawahangaisha. Kwa upande mwingine, baadhi ya watu wasio na mvi huhangaishwa kwa sababu wengine hawatambui umri wao mkubwa.

Kuota mvi hakumaanishi kwamba nywele zimekufa. Kwa kweli, sehemu inayoonekana ya nywele zote imekwisha kufa. Kila unywele una sehemu iliyo chini ya ngozi. Ukuzi huendelea kwenye sehemu hiyo. Sehemu hiyo ni kama kiwanda ambapo nywele zinatengenezwa. Ukuzi wa nywele hutokea wakati chembe zinapojigawanya kwa haraka katika sehemu hiyo. Na nywele zinapoendelea kukua hufyonza rangi. Rangi hiyo inafanyizwa na chembe za rangi. Kwa sababu hiyo, iwapo chembe za rangi zingekoma kutengeneza rangi hiyo kwa sababu fulani, nywele zitakuwa nyeupe.

Haijulikani ni kwa nini chembe za rangi hukoma nyakati nyingine kwa ghafula kutengeneza rangi hiyo. Kwa hiyo njia za kuzuia mvi hazijagunduliwa bado. Inajulikana pia kwamba chembe za rangi ambazo zimekoma kufanya kazi zinaweza kuanza kufanya kazi tena. Jambo la kupendeza ni kwamba Biblia inataja nywele mara nyingi, na mfano mmoja wa Yesu hutaja nywele nyeupe. Alisema hivi: “Huwezi kugeuza unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi.” (Mathayo 5:36) Maneno hayo yanaonyesha kwamba tangu zamani wanadamu wametambua kwamba hawawezi kuzuia mvi zisitokee na kurudisha rangi ya awali ya nywele baada ya mvi kutokea.

Baadhi ya watu hujaribu njia mpya kama vile kudungwa sindano yenye rangi ya asili ya nywele. Wengine hutia nywele zao rangi, jambo ambalo si jipya. Wagiriki na Waroma wa kale walitia nywele zao rangi. Na Wamisri wa kale walitumia damu ya mafahali ili kutia nywele zao rangi. Imesemekana kwamba Herode Mkuu, aliyeishi wakati wa Yesu Kristo, alitia nywele zake rangi ili umri wake usitambuliwe.

Hata hivyo, kutia nywele rangi kwa ukawaida ni kazi nyingi na huchukua muda, na wengine wanaweza kuathiriwa na rangi hiyo au kupata matatizo ya ngozi. Huenda ukaamua kutia rangi nywele zako kwa sababu ya mvi. Lakini huenda ikawa siku moja utaamua kuacha kuzitia rangi na wakati huo utakuwa na nywele zenye rangi mbili kwa muda fulani wakati nywele mpya zisizotiwa rangi zitakapoanza kutokea. Kwa upande mwingine, mvi zinaweza kuwa maridadi na kukufanya uwe na heshima ambayo hukuwa nayo hapo awali. Biblia inasema hivi: “Kichwa chenye mvi ni taji ya utukufu, kama kikionekana katika njia ya haki.”—Mithali 16:31.

Upara na Kupungua kwa Nywele

Matatizo mengine ya kawaida ni upara na kupungua kwa nywele. Matatizo hayo pia yamekuwapo tangu zamani za kale. Dawa ya upara huko Misri ya kale ilitia ndani mafuta ya simba, kiboko, mamba, paka, nyoka, na bata-bukini. Siku hizi kuna dawa nyingi za nywele na za ngozi ya kichwa zinazodaiwa kufanya kazi, na kila mwaka watu hutumia pesa nyingi sana kuzinunua.

Upara hutokea wakati ukuzi wa nywele unapobadilika. Ukuzi wa nywele unaweza kuathiriwa na afya mbaya kama vile utapiamlo, homa inayoendelea, au magonjwa ya ngozi. Mimba na kujifungua kunaweza pia kuathiri ukuzi wa nywele na kufanya nywele nyingi zitoke. Hata hivyo, visababishi hivyo vinapokwisha, nywele hazitoki tena na ukuzi huendelea kama kawaida.

Sababu nyingine ya kutoka kwa nywele ni ugonjwa unaoitwa alopecia. * Mara nyingi, ugonjwa huo hufanya nywele zitoke kwenye sehemu ndogondogo kichwani. Utafiti wa kitiba wa karibuni unaonyesha kwamba hali hiyo inaweza kusababishwa na hitilafu katika mfumo wa kinga.

Upara wa wanaume ni tatizo la kawaida zaidi la nywele. Tatizo hilo huwakumba wanaume. Nywele huanza kutoka hatua kwa hatua upande wa mbele kichwani au katikati. Ukuzi wa nywele hubadilika katika sehemu inayoathiriwa na hatimaye hukoma kabisa. Kitabu The Encyclopædia Britannica kinaeleza hivi: ‘Nywele nyororo zinaanza kukua mahali ambapo nywele za awali zimetoka zilizokuwa ndefu, nene, na zenye rangi ya asili.’ Kwa hiyo, hatua kwa hatua ni nywele chache tu zinazobaki ambazo hukua kwa muda mfupi tu, kisha kutoka, na hatimaye zitakoma kutokea. Hali hiyo hurithiwa na husababishwa na homoni za wanaume.

Upara wa wanaume unaweza kuanza kijana anapoanza kubalehe, lakini kwa kawaida hutokea mwanamume anapokuwa mwishoni mwa miaka yake ya 30 na katika miaka yake ya 40. Ijapokuwa upara huo huwaathiri wanaume wengi, wanaume wa rangi mbalimbali huathiriwa kwa viwango tofauti-tofauti. Jambo la kusikitisha ni kwamba ugonjwa huo hauna dawa kufikia sasa. Baadhi ya wanaume wameamua kutumia nywele bandia au kufanyiwa upasuaji ili kuwekewa nywele za mtu mwingine. Wengi wameweza kuzuia nywele zinazobaki zisitoke sana kwa kuzitunza vizuri.

Nyakati nyingine inaonekana kama nywele zinapungua ijapokuwa hazitoki. Hilo linaweza kutokea wakati unene wa unywele mmoja-mmoja hupungua. Unywele mmoja ni mnene kadiri gani? Kulingana na uchunguzi mmoja, nywele za watu fulani zinaweza kuwa zenye unene wa mikroni 50 ijapokuwa nywele za wengine zinaweza kuwa zenye unene wa mikroni 100. * Unene wa nywele hupungua mtu anapozeeka. Huenda mtu akadhani kwamba kupungua kwa unene wa nywele kwa mikroni chache tu hakuwezi kutambuliwa. Lakini, kumbuka kwamba kuna nywele 100,000 kichwani. Kwa hiyo, ijapokuwa kila unywele hupungua unene kidogo sana inaonekana kama mtu amepoteza nywele nyingi.

Tunza Nywele Zako

Nywele hukua zaidi ya sentimeta moja kila mwezi, na ni mojawapo ya sehemu za mwili zinazokua haraka sana. Kama ukuzi wa nywele zote ungejumlishwa katika unywele mmoja, huo ungekua zaidi ya meta 20 kwa siku!

Ijapokuwa dawa ya mvi na upara haijapatikana bado, tunaweza kufanya mengi ili kutunza nywele tulizo nazo. Ni muhimu kula chakula chenye lishe ya kutosha na kuboresha mzunguko wa damu kwenye ngozi ya kichwa. Kujinyima chakula ili kupunguza unene au kula vyakula visivyo na lishe kunaweza kufanya mvi na upara kutokea mapema. Wataalamu wanadokeza kuosha nywele kwa ukawaida na kusugua ngozi ya kichwa, na kuepuka kukwaruza ngozi ya kichwa kwa kucha. Jambo hilo huboresha mzunguko wa damu kichwani. Baada ya kuosha nywele kwa kutumia sabuni ya nywele, tumia maji safi ili kuondoa sabuni kabisa.

Usichane nywele kwa nguvu. Ukiwa na nywele ndefu, ni afadhali uanze kuchana sehemu ya mwisho ya nywele. Baadaye sehemu ya katikati. Kisha chana nywele zote ukianzia juu.

Huenda ukahangaishwa ukiona mvi na nywele nyingi zikitoka. Hata hivyo, kumbuka kwamba kwa kawaida wengine hawaangalii nywele zako kwa makini kama wewe. Wewe ndiwe utaamua ukitaka kutia nywele zako rangi au la, kutumia nywele bandia au la, au kujaribu njia nyingine. Vyovyote iwavyo, ni muhimu kuziweka nywele zikiwa safi na nadhifu, hata uwe na nywele nyingi au rangi yake iweje.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 17 Ona toleo la Amkeni! la Kiingereza la Aprili 22, 1991, ukurasa wa 12.

^ fu. 20 Mikroni moja ni milimeta 0.001.

[Sanduku/Mchoro katika ukurasa wa 27]

UKUZI WA NYWELE

Nywele hukua hatua kwa hatua. Hatua hizo ni hatua ya kukua, hatua fupi ya kubadilika kwa unywele, na ya kutokua. Kitabu The World Book Encyclopedia kinaeleza hivi: ‘Unywele huacha kukua kila unapofikia hatua ya kutokua. Unywele hubaki katika kitundu cha kutokua hadi hatua inayofuata ya ukuzi. Unywele hutoka unapokuwa katika hatua ya kutokua, wakati unywele mpya unapoanza kukua na kuusukuma nje ya kitundu.’ Asilimia 85 hadi 90 ya nywele huwa katika hatua ya kukua kwa wakati mmoja, asilimia 10 hadi 15 huwa katika hatua ya kutokua na asilimia 1 katika hatua ya kubadilika kwa unywele.

[Mchoro]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Ukuzi wa mapema

Unywele unaokua

kitundu

mishipa ya damu

tezi ya mafuta

unywele

Hatua ya kutoka

Hatua ya kutokua

Unywele mpya unakua

[Picha ya ukurasa mzima katika ukurasa wa 24]