Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kukosa Usingizi Katika Safari ya Anga

Baada ya kusafiri angani kwa muda wa miezi mitano katika chombo cha angani cha Urusi kiitwacho Mir mwaka wa 1997, mwana-anga Jerry Linenger alitambua kwamba mchana uligeuka kuwa usiku kila wakati Mir ilipozunguka dunia kwa dakika 90. Jambo hilo lilivuruga kabisa usingizi wake. Kwa nini? Ili kuhifadhi nishati iliyotumika katika chombo hicho cha angani, ilibidi kutumia mwangaza wa jua, ulioingia kupitia dirishani. Kwa hiyo, “mchana, usiku, mchana, usiku, mara 15 kwa siku unakuvuruga kabisa,” akasema Linenger. Alisema hivi kuhusu jinsi usingizi wa wana-anga wenzake wawili ulivyovurugika: “Wanaanza kusinzia na kuelea.” Kulingana na gazeti la New Scientist, ili “kufanikisha safari ndefu za angani wakati ujao” itahitaji kutafuta njia za kuwasaidia wanaanga kudumisha kawaida zao za kulala. Iwapo hakuna suluhisho, “kuwasaidia wanaanga wasisinzie wanapokuwa katika safari za mbali angani kunaweza kuwa tatizo kubwa.”

Nzi Alivumbua Injini Kwanza

Kutengeneza injini inayochanganya kiasi kinachofaa cha mafuta na oksijeni ili kufanya gari liweze kusafiri kwa miendo mbalimbali na bado lisitoe moshi usio mchafu, si kazi rahisi. Gazeti la The New York Times linasema kwamba watengenezaji wa magari walihitaji kutumia “mfumo wa vali zinazoweza kubadili kiasi cha mafuta na hewa inayopita mara tu badiliko la mwendo linapohitajika.” Hata hivyo, watafiti waliochunguza nzi-tunda katika Chuo Kikuu cha Würzburg, Ujerumani, hivi majuzi waligundua kwamba nzi-tunda hao wametumia njia inayofanana sana na hiyo ya kutumia kiasi kinachofaa cha oksijeni na kutoa kaboni dayoksaidi, bila kupoteza mvuke mwingi. Nzi-tunda hutumia mashimo madogo yaliyo kifuani na tumboni ili kudhibiti “kiasi kinachofaa cha gesi zinazoingia ndani yake au kutoka, na wakati huohuo kuzuia maji mengi yasipotee,” gazeti hilo lilisema. Liliongezea kusema kwamba “mashimo hayo yanaweza kufunguka na kujifunga kabisa, au kujifungua kwa kadiri tofauti-tofauti kwa sekunde chache tu.”

Upendo Unaopumbaza

Watu wengi hupumbazwa na upendo na kuhisi wakiwa na furaha nyingi, laripoti gazeti El Universal la Mexico City. Jambo hilo huongeza vipitisha-habari kama dopamine katika ubongo. Mwanasaikolojia mmoja Giuseppe Amara anaonelea kwamba watu fulani huanzisha urafiki na mtu mmoja baada ya mwingine bila kutaka uhusiano wa kudumu kwa sababu hawataki kupoteza hisia hiyo ya kupumbazika. Hisia hiyo ya kupumbazika yaweza kudumu kwa miezi mingi hata kufikia miaka miwili. Halafu hisi hiyo huanza kupoa, na mtu huingia katika hatua inayofuata, ambapo homoni iitwayo oxytocin huongezeka, na kuleta hisi nzuri na ya upendo wa ndani sana. Amara anasema kwamba ingawa ule upendo wa kupumbaza unafurahisha sana, unaweza kuharibu uwezo wa mtu wa kutumia busara anapofanya maamuzi, ukimzuia kuona udhaifu wa mwenzake. Kwa hiyo, gazeti la El Universal linasema, wataalamu wanapendekeza kwamba watu wasioane hadi wawe “wamejuana vizuri ili waweze kudumisha uhusiano mzuri.”

Kutengana na Talaka Zaongezeka Sana Hispania

“Si lazima tubaki katika ndoa moja maishani,” anasema mtaalamu mmoja wa mambo ya jamii na mwandishi Inés Alberdi katika kitabu chake La nueva familia española (Familia Mpya ya Kihispania). Kulingana na gazeti El País, inaonekana wenzi wengi wa ndoa huko Hispania wana maoni ayo hayo. Uchunguzi uliofanywa hivi majuzi na Wizara ya Sheria unaonyesha kwamba kati ya kila ndoa mbili zinazofungwa nchini Hispania, moja huishia talaka au kutengana. Wataalamu wanatabiri kwamba ndoa zitazidi kuvunjika kwa sababu ya maoni yanayobadilika kuhusu ndoa na wanawake kuwa na uwezo zaidi wa kifedha. “Wenzi wa ndoa hawataki kujidhabihu sana, [na] vijana hawataki kuvumilia hata kidogo,” anasema Luis Zarraluqui, msimamizi wa Chama cha Mawakili wa Masuala ya Kifamilia cha Hispania. “Ndoa zinazidi kuvunjika [hata] miongoni mwa wazee, hasa wanapofikia umri wa kustaafu.” Desturi za kidini zimeshindwa kukomesha mwelekeo huo. Ingawa asilimia 85 ya Wahispania wanadai kuwa Wakatoliki, kutengana na talaka zimeongezeka mara 5 katika miaka 20 iliyopita.

Hatari za Kutoboa Mwili

Watu wengi, hasa vijana, wanapenda sana kutoboa sehemu mbalimbali za mwili ili kuvaa vipuli. “Kwa kusikitisha, hawaoni hatari za tabia hiyo,” lasema gazeti Świat Kobiety la Poland. “Kipindi cha uasi wa vijana kinapopita, sehemu ya juu ya jicho iliyojaa vipuli sasa haionwi kuwa urembo.” Na hata kama vipuli hivyo vitatolewa, bado alama zinabaki. Zaidi ya hilo, kutoboa ngozi ya uso kunaweza kuharibu mishipa ya neva na ya damu na kusababisha “hali ya kutoweza kuhisi chochote” na “maambukizo na vidonda ambavyo huchukua muda mrefu kupona.” Bakteria husitawi sana katika “sehemu zenye umajimaji na joto” za mdomo, hivyo kutoboa sehemu hizo husababisha maambukizo na kuoza kwa meno. Vivimbe vigumu vyenye mafuta vinaweza kutokea katika sehemu zilizo na mafuta mengi kama vile kitovuni na masikioni. Gazeti hilo lilionya kwamba “mara nyingi vipuli vya chuma vimechanganywa na nikeli. Watu ambao huathiriwa na nikeli wanaweza kupata uvimbe au vidonda vidogo vinavyowasha.”

“Upasuaji Wenye Kasoro wa Kubadili Maumbile”

Katika miaka kumi iliyopita, kesi zilizohusu makosa yaliyofanywa katika upasuaji wa kubadili maumbile ziliongezeka kwa asilimia 117 katika Ufaransa, na kesi 1 kati ya 3 ilihusu upasuaji wa matiti, lasema gazeti Le Point. Kulingana na wataalamu, asilimia 30 ya upasuaji uliofanywa ilihitaji kufanyiwa marekebisho, na wengine hata wamekufa kutokana na matatizo yaliyotokana na upasuaji waliofanyiwa. Akilaumu kile alichokiita “upasuaji wenye kasoro wa kubadili maumbile,” Dakt. Pierre Nahon, aliye mpasuaji wa kubadili maumbile alisema hivi: “Kwa dakika 20, sote tunaweza kufanya upasuaji ambao kwa kawaida huchukua muda wa saa mbili. Lakini matokeo yatakuwa tofauti.” Kulingana na gazeti Le Point, “Hospitali fulani huwa makini zaidi zinapochagua mawakili kuliko zinapochagua madaktari.”

Mahangaiko Kuhusu Afya Barani Ulaya

Watu zaidi na zaidi katika mataifa fulani barani Ulaya hawaridhishwi na huduma za afya. Takwimu za Tume ya Ulaya zinaonyesha kwamba watu wengi katika Ureno, Ugiriki, na Italia wanahisi hawapati huduma nzuri ya afya. Ni kweli kwamba huduma za afya katika Ulaya zimebanwa sana. Wazee wanapozidi kuongezeka, wale wanaougua maradhi kama ya Alzheimer nao wanaongezeka. Kwa upande mwingine, maofisa wa afya wanaonelea kwamba watu wanapaswa kutunza afya zao zaidi. Kulingana na gazeti EUR-OP News, “tabia za kupima ulaji, kukaa kitako, na kula nyama zenye mafuta mengi, zimeonekana kuwa hatari,” na “idadi ya wanaume wanene na wanawake waliokonda . . . inaongezeka.”

Ujeuri Dhidi ya Makasisi

“Waenda-kanisani wenye hasira huwatukana na kuwashambulia makasisi wakati wa mabishano makali kuhusu arusi na ubatizo wa watoto,” laripoti The Sunday Telegraph la London. Uchunguzi uliohusu makasisi 1,300 wa kusini-mashariki mwa Uingereza ulionyesha kwamba kwa zaidi ya kipindi cha miaka miwili, zaidi ya asilimia 70 ya makasisi walitukanwa, asilimia 12 wakashambuliwa, na asilimia 22 wakatishwa kupigwa. Dakt. Jonathan Gabe, aliyeongoza uchunguzi huo katika Taasisi ya Holloway ya Chuo Kikuu cha London, alilaumu “waenda-kanisani wenye kutukana ikiwa mambo hayaendi jinsi wanavyotaka.” Pia alitaja visababishi vya ujeuri kuwa “tabia ya kudai mno kutimiziwa haki na mapendezi yao na kukosa kuheshimu umma na kutokuwa na imani na watumishi wa umma.” Ili kukabili hali hiyo dayosisi nyingine zinawafundisha makasisi mbinu za kupigana ili waweze kukabiliana na waenda-kanisani wenye ujeuri kwa kuwapa mazoezi ya kujikinga.