Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Fahary ya Mapango ya Carlsbad

Fahary ya Mapango ya Carlsbad

Fahary ya Mapango ya Carlsbad

Kuna giza totoro na kumenyamaza kimya. Hivyo ndivyo tunavyoona tunapotembelea mapango makubwa kwenye Mbuga ya Wanyama ya Mapango ya Carlsbad huko New Mexico, Marekani. Tulipokuwa tukiingia mapangoni tulijiuliza: ‘Haya mapango yalitokeaje? Ni makubwa kadiri gani? Ni mambo gani yasiyo ya kawaida yaliyomo? Je, ni salama kutembea ndani ya hayo mapango?’

KABLA ya kuyatembelea mapango, kikundi chetu kilifurahia kupiga kambi na vilevile kupanda milima kwenye Mbuga ya Wanyama ya Milima ya Guadalupe, kusini-magharibi mwa Texas. Tulipokuwa tukipanda Kilele cha Guadalupe chenye urefu wa meta 2,666, tuliona visukuku kwenye miamba iliyokuwa njiani. Hiyo ndiyo sehemu ya Texas iliyo na kimo cha juu zaidi. Kulingana na wanajiolojia, visukuku hivyo huonyesha jinsi Mapango ya Carlsbad yalivyotokea. Jinsi gani?

Hapo zamani, yamkini sehemu hiyo ilikuwa na mwani, sifongo, na moluska. Sehemu yote ilifunikwa kwa maji yenye joto ya bahari. Matumbawe, yanayofanyiza miamba mingi leo, hayakupatikana kwa wingi katika sehemu hiyo. Kati ya viumbe wa baharini waliopatikana ni kutia ndani jamii za athropodi zilizotokomea. Baadhi ya viumbe hao waliishi katika magamba makubwa yaliyojikunja, yenye sehemu mbalimbali. Magamba hayo yanafanana na yale ya wanyama wa baharini wanaoitwa nautilus. Tulifurahi sana kuona gamba kama hilo kwenye mwamba uliokuwa njiani!

Yamkini miamba ya chokaa ilitokea wakati visukuku vya viumbe vya baharini na chembe nyingine ziliporundikana na kuunganishwa pamoja. Kwa kuwa sakafu ya bahari ilizama, miamba hiyo iliongezeka kimo kufikia meta 500. Hatimaye, maji ya bahari yalipopanda, miamba hiyo ilifunikwa kwa masimbi ya bahari. Muda mrefu baadaye, ardhi iliinuka, masimbi yakamomonyoka na ile miamba ikawa milima. Hata hivyo, huko kuinuka kwa ardhi kulitokezaje Mapango ya Carlsbad?

Gesi, Maji, Hewa, na Asidi

Maji ya mvua yanapopita hewani na kwenye udongo, hupata kiasi kidogo cha asidi-kabonia. Yamkini asidi hiyo dhaifu ndiyo hufanyiza mapango mengi ya chokaa ulimwenguni. Hata hivyo, kulingana na mwanajiolojia Carol Hill, mapango yaliyo kwenye Milima ya Guadalupe yalifanyizwa kwa asidi kali zaidi.

Hill adokeza kwamba gesi yenye salfa nyingi ilifanyizwa katika sehemu zenye mafuta, chini ya mawe yaliyo chini ya miamba ya chokaa. Mawe hayo yalipoinuka, gesi hiyo iliingia kwenye miamba na kuchangamana na hewa na maji yenye oksijeni yaliyo chini ya ardhi na kufanyiza asidi-sulfuriki. Hiyo asidi kali iliyeyusha sehemu kubwa ya miamba ya chokaa.

Milima ilipoinuka na tabaka la maji ya chini ya ardhi kushuka chini, asidi iliyapanua hayo mapango pole kwa pole. Kwenye Mapango ya Carlsbad, nyufa na mapengo yaliungana na kufanyiza njia yenye mizingile mingi. Ramani ya vijia vyenye urefu wa kilometa 37 imechorwa. Licha ya Mapango ya Carlsbad, kuna mamia ya mapango mengine kwenye milima hiyo. Pango kubwa zaidi linaitwa Pango la Lechuguilla. Kuna ramani ya vijia vya pango hilo vyenye urefu wa kilometa 160.

Mapambo Mapangoni

Tulipoingia Mapango ya Carlsbad kwa mara ya kwanza tuliteremka meta 225 kwa kutumia kambarau iliyotufikisha karibu na chumba kikubwa (Big Room). Kina ukubwa wa ekari 14. Katika sehemu nyingine, paa za chumba hicho zimeinuka meta 30 juu ya sakafu ya pango. Lakini kilichotupendeza zaidi ni mapambo mengi ya asili yaliyo mapangoni, yanayomulikwa kwa taa zisizoonekana.

Mapambo hayo husitawi mahali ambapo maji yanayoingia mapangoni yanapovukizwa, na kusababisha chokaa iliyo majini kurundamana. Kwenye sehemu za paa ambapo maji yamedondoka kwa kuendelea, kuna mirija inayositawi ikielekea meta kadhaa chini. Mirija hiyo huitwa eti “mirija ya kunywa soda.” Hatimaye mirija hiyo huzibwa, na kuwa mawe ya chokaa yanayoning’inia juu ya pango yanayoitwa stalaktiti. Pia, stalaktiti zenye kujipinda-pinda huning’inia juu ya paa zilizoinama na kurembesha vyumba fulani mapangoni vinavyofanana na vyumba vya maonyesho.

Maji yanapodondoka sakafuni, mawe yaweza kusitawi pangoni na kuelekea juu. Baadaye, mawe hayo yanayoitwa stalagmiti yaweza kufika kwenye paa, yaungane na stalaktiti, na kufanyiza nguzo. Baadhi ya stalagmiti katika chumba kinachoitwa Jumba la Majitu (Hall of Giants) yamesitawi kufikia kimo cha zaidi ya meta 18! Maji yanayodondoka na kuingia kwenye mashimo madogo, yanaweza kufanyiza mawe madogo yaliyopakwa chokaa laini na kufanyiza lulu za mapangoni zinazong’aa. Hata mapambo yasiyo ya kawaida yametokea. Hayo yatia ndani makundi ya fuwele zenye ncha kali, na mirija iliyojipinda-pinda inayoitwa helictites, inayositawi ikielekea pande mbalimbali.

Tulipotazama stalaktiti kubwa nyingi zilizo juu yetu, tulihofu kuwa labda zaweza kuporomoka. Mtembezaji wetu alituhakikishia kuwa ni vigumu sana kwa mapambo hayo kuporomoka. Tulitumai hayangeanguka!

Mazingira ya Mapango

Baada ya kufurahia mlo nje ya mapango hayo, tuliteremka tena mapangoni kupitia mlango mpana. Michoro ya Wahindi wa Amerika hupamba kuta za mapango.

Tulipokuwa tukiingia, kulikuwa na uvundo wa kinyesi cha popo. Tulijifunza kwamba karne moja hivi iliyopita, kinyesi hicho kilikuwa kikikusanywa na kutumiwa kama mbolea. Ndoo iliyofungwa kwa kamba ngumu ilitumiwa kupandisha kinyesi hicho na baadaye mfumo huohuo ukatumiwa kuwa kambarau ya kuwateremsha na kuwapandisha watalii kutoka mapangoni. Kinyesi hicho hupatikana kwenye kijia kilicho kando kinachoitwa Pango la Popo (Bat Cave)—makao ya mamilioni ya popo wakati wa kiangazi. Kunapokuwa usiku, popo hao hutoka nje ya pango katika vikundi vikubwa.

Wasimamizi wa mbuga hiyo walitueleza kwamba mapango hayo yanaweza kuharibika kwa urahisi. Watu wanaotembelea mapango hayo wanaweza kuyaharibu na kuyachafua kwa urahisi. Kwa mfano, mapambo yaliyo mapangoni yanapoguswa tu, yaweza kuchafuliwa na mafuta yanayoweza kuzuia yasisitawi au kuyageuza rangi. Kwa hiyo, tuliamua kutembea kwenye vijia vilivyoteuliwa na tukaepuka kuyagusa mawe yaliyo mapangoni.

Tulipokuwa tukiondoka kwenye mandhari hayo mazuri, tulifikiria kurudi wakati mwingine kuona vitu vingine vilivyo mapangoni. Tungependa kuona popo wanaporuka. Popo hao wametembelea mapango hayo kwa muda mrefu zaidi ya wanadamu. Hata hivyo, ni wanadamu wala si popo wanaoondoka mapangoni wakiwa wamevutiwa sana.—Imechangwa.

[Picha katika ukurasa wa 26]

Juu: Stalaktiti zilizo kama taa maridadi zinazoning’inia

[Picha katika ukurasa wa 26]

Chini: Kutembelea kile chumba kikubwa (Big Room)

[Hisani]

© Russ Finley/Finley-Holiday Films

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]

© Russ Finley/Finley-Holiday Films

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 26]

© Russ Finley/Finley-Holiday Films