Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mbinu Mpya za Ugaidi

Mbinu Mpya za Ugaidi

Mbinu Mpya za Ugaidi

Mara ya mwisho tulipozungumzia ugaidi katika gazeti la “Amkeni!” tulitumia picha inayofahamika kwenye jalada —picha ya wauaji wenye bunduki waliofunika nyuso zao huku kukiwa na mlipuko mkubwa nyuma yao. Lakini siku hizi hali imebadilika.

MSAFARA wa malori yasiyopambwa wapita taratibu kwenye maeneo ya makazi katika mwanga hafifu wa machweo. Malori hayo yasimama karibu na shule moja. Punde si punde, kikosi maalumu cha wanaume waliovalia vinyago vya kujikinga gesi na mavazi ya kujikinga dhidi ya kemikali, chaibuka na kuingia vichakani. Wanajua tu kwamba kombora dogo lililipuka wakati wa tamasha ya michezo shuleni humo. Gesi kali ya kombora hilo ilisambaa na kuwadhuru watazamaji wengi. Wanaume wanne wanakagua eneo hilo kwa uangalifu huku wakishirikiana na kikosi cha hali ya dharura cha mji huo ili kujua kilichotukia. Kombora hilo lilikuwa na gesi gani? Je, ni gesi yenye viini vya maradhi ya wanyama (anthrax) yanayoambukiza wanadamu? Je, ni gesi inayodhuru neva?

Wanaume hao wanatembea taratibu kuelekea uwanjani, huku wakiwa wamebeba vifaa mbalimbali vya kuchunguza kemikali. Wanaingia kwenye chumba kidogo wanamopata vipande vya kombora hilo. Wanahitaji kuwa waangalifu sana, kwa kuwa wanatumia vifaa vidogo vya kupimia na pia wanahitaji kusogeza vitu vizito.

Muda si muda jasho lawatiririka. Kazi hiyo inachosha sana, hata kwa watu waliozoezwa. Wanagundua gesi hiyo baada ya muda usiozidi dakika 10. Mtaalamu wa kemikali anayeambatana nao asema hivi: “Bila shaka ni gesi yenye viini vya maradhi ya wanyama yanayoambukiza wanadamu.”

Mbinu Mpya za Ugaidi

Tukio hilo halikuwa halisi. Hayo yalikuwa mazoezi ya kujaribu itikio la kikosi hicho kwa shambulizi bandia la gesi ya sumu. Mazoezi hayo yalifanywa katika jimbo moja kaskazini mwa New York. Kikosi hicho ni mojawapo ya Vikosi vya Kulinda Umma Kutokana na Silaha Hatari (Weapons of Mass Destruction Civil Support Teams). Vikosi hivyo vinachunguza uwezo na athari ya mbinu mpya zinazotumiwa na magaidi. Vinapima viini hatari, kemikali, au vifaa vyenye mnururisho.

Kikosi hicho ni mojawapo ya vikosi vingi ambavyo vimebuniwa ulimwenguni pote ili kupambana na mbinu mpya na matatizo mapya ya ugaidi. * Visa vilivyotukia miaka ya majuzi vyaonyesha kwamba matendo ya kigaidi yanayofanywa na vikundi mbalimbali au na watu wenye siasa kali yanaongezeka. Ijapokuwa magaidi wengi bado hushambulia vituo vya kijeshi na makao ya kibalozi, baadhi yao wameanza pia kushambulia zile zinazoitwa eti shabaha rahisi, kama vile mifumo ya usafiri wa umma, tamasha za michezo, sehemu za miji zenye watu wengi, mahoteli, na vituo vya watalii.

Porter Goss, mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi ya Bunge la Wawakilishi la Marekani, alikiri magaidi wanatumia mbinu mpya aliposema hivi: “Ni lazima tubadili maoni yetu ya kale kuhusu magaidi wanaodhaminiwa na serikali na kutambua mbinu mpya za ugaidi. Matendo ya kigaidi yanayoongezeka sasa ni yale yanayofanywa na magaidi wenye lengo hususa.”

Mbinu mpya za ugaidi zatia ndani matendo na harakati ambazo haziwezi kuzuiwa au kukomeshwa kwa urahisi. Magaidi wengi zaidi wanatumia tekinolojia mpya na wanajitafutia msaada wa kifedha. Gazeti la USA Today laripoti hivi: “Ni vigumu sana kukomesha ugaidi kwa sababu magaidi wanatumia tekinolojia mpya ya kompyuta na ya mawasiliano na wanashirikiana na makundi ya siri ya ujambazi.” Siku hizi magaidi wana shabaha mpya. Jambo hilo limewafanya waandishi na wachanganuzi wa habari wabuni semi mpya kama vile “ugaidi wa Internet,” “ugaidi wa viini hatari,” na “ugaidi wa kimazingira.”

Mbinu hizo mpya za ugaidi ni hatari kadiri gani? Je, uhai wako umo hatarini? Je, tatizo la kuenea kwa ugaidi ulimwenguni pote laweza kutatuliwa? Makala zifuatazo zitajibu maswali hayo.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 8 Watu wana maoni mbalimbali kuhusu ugaidi. Kwa mfano, katika nchi zilizoharibiwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe, matendo ya kijeuri kati ya vikundi vinavyozozana yanaweza kuonwa kuwa matendo halali ya kivita au kama ugaidi, ikitegemea yule anayehojiwa. Katika mfululizo huu wa makala, neno “ugaidi” kwa ujumla linamaanisha kuwashurutisha watu kwa kutumia jeuri.

[Sanduku/Ramani katika ukurasa wa 4, 5]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Mwongo wa UGAIDI

1. Buenos Aires, Argentina

Machi 17, 1992

Bomu lililotegwa katika gari lalipua Ubalozi wa Israeli. Waliouawa: 29. Waliojeruhiwa: 242

2. Algiers, Algeria

Agosti 26, 1992

Bomu lalipuka kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa. Waliouawa: 12. Waliojeruhiwa: angalau 128

3. New York City, Marekani

Februari 26, 1993

Wanadini wenye siasa kali walipua bomu lenye nguvu sana chini ya jengo la World Trade Center. Waliouawa: 6. Waliojeruhiwa: 1,000 hivi

4. Matsumoto, Japani

Juni 27, 1994

Wafuasi wa madhehebu ya Aum Shinrikyo wasambaza gesi ya sarin kwenye eneo la makazi. Waliouawa: 7. Waliojeruhiwa: 270

5. Tokyo, Japani

Machi 20, 1995

Wafuasi wa madhehebu ya Aum Shinrikyo waweka makopo sita ya gesi ya sarin kwenye magari ya moshi ya chini ya ardhi huko Tokyo. Makopo hayo yaeneza gesi yenye sumu ya sarin. Waliouawa: 12. Waliojeruhiwa: zaidi ya 5,000

6. Oklahoma City, Marekani

Aprili 19, 1995

Bomu lililotegwa katika lori lalipuka karibu na jengo la serikali. Magaidi wenye siasa kali walaumiwa. Waliouawa: 168. Waliojeruhiwa: zaidi ya 500

7. Colombo, Sri Lanka

Januari 31, 1996

Magaidi wa kikabila wagongesha lori lililojaa makombora kwenye benki. Waliouawa: 90. Waliojeruhiwa: zaidi ya 1,400

8. London, Uingereza

Februari 9, 1996

Magaidi wa kutoka Ireland walipua bomu kwenye maegesho. Waliouawa: 2. Waliojeruhiwa: zaidi ya 100

9. Jerusalem, Israel

Februari 25, 1996

Mpiganaji wa kujitolea kufa alipua basi kwa bomu. Yasemekana kwamba wanadini wenye siasa kali ndio waliofanya hivyo. Waliouawa: 26. Waliojeruhiwa: 80

10. Dhahran, Saudi Arabia

Juni 25, 1996

Lori la mafuta lenye bomu lalipuka nje ya makazi ya kijeshi ya Marekani. Waliouawa: 19. Waliojeruhiwa: 515

11. Phnom Penh, Kambodia

Machi 30, 1997

Magaidi warushia waandamanaji makombora manne. Waliouawa: 16 hivi. Waliojeruhiwa: zaidi ya 100

12. Coimbatore, India

Februari 14, 1998

Mabomu kadhaa yalipuliwa na wapiganaji wa kidini wenye siasa kali. Waliouawa: 43. Waliojeruhiwa: 200

13. Nairobi, Kenya, na Dar es Salaam, Tanzania

Agosti 7, 1998

Majengo ya Ubalozi wa Marekani yalipuliwa kwa bomu. Waliouawa: 250. Waliojeruhiwa: zaidi ya 5,500

14. Kolombia

Oktoba 18 na Novemba 3, 1998

Shambulizi moja la mabomu na jingine la makombora. Bomba la mafuta lalipuliwa kwa mabomu. Waliouawa: 209. Waliojeruhiwa: zaidi ya 130

15. Moscow, Urusi

Septemba 9 na 13, 1999

Milipuko miwili mikubwa yabomoa majengo mawili ya makazi. Waliouawa: 212. Waliojeruhiwa: zaidi ya 300

[Hisani]

Chanzo cha habari: The Interdisciplinary Center, Herzliya, Israel

Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.

Victor Grubicy/Sipa Press

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 6]

Kompyuta Zavamiwa

Machi 1999: Ripoti zaonyesha kwamba kompyuta za Makao Makuu ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) zimekuwa zikivamiwa “kisirisiri, na kwa mpango” na watu wasiojulikana. Wataalamu wa kompyuta huvamia mifumo ya kompyuta ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani mara 60 hadi 80 kila siku.

Katikati ya Mwaka wa 1999: Katika kipindi cha miezi mitatu tu, wataalamu wa kompyuta wanaopinga serikali walivamia vituo vya Internet vya Bunge la Marekani, Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI), Jeshi la Marekani, Ikulu ya White House, na wizara kadhaa za serikali ya Marekani.

Januari 2000: Inaripotiwa kwamba biashara ulimwenguni pote zilitumia dola bilioni 12.1 za Marekani katika kupambana na “ugaidi wa kiuchumi” uliosababishwa na programu hatari zinazoharibu mifumo ya kompyuta.

Agosti 2000: Mtaalamu wa kompyuta avamia vituo vya Internet vya shirika la serikali na vya halmashauri ya mitaa katika Muungano wa Uingereza na Ireland.