Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ugaidi Utakoma Karibuni!

Ugaidi Utakoma Karibuni!

Ugaidi Utakoma Karibuni!

MAGAIDI wanaweza kushambulia basi huko Jerusalem, jengo la serikali huko Oklahoma City, au jengo la makazi huko Moscow. Ijapokuwa magaidi hukusudia kuwasilisha ujumbe muhimu kwa wanasiasa, wakuu wa kijeshi, au wasimamizi wa mambo ya kiuchumi, mara nyingi wanashambulia watu wasiohusika. Katika visa vingi wao hushambulia watu wa kawaida—watu ambao hawahusiki hata kidogo na makusudi ya magaidi hao. Basi, mbona watu wenye siasa kali hutenda matendo ya kigaidi?

Mbona Kuna Ugaidi?

Matendo ya kigaidi huwa yamepangwa kimbele na kudhamiriwa. Lengo kuu si kuua na kujeruhi watu wengi. Mauaji hayo huwasaidia kutimiza lengo lao. Magaidi huzusha hali ya wasiwasi na hofu ili kudunisha wenye mamlaka. Wao hutaka kusikilizwa na kutimiziwa mahitaji yao hususa. Fikiria baadhi ya sababu zinazofanya magaidi watende kwa ujeuri.

Chuki. “Ugaidi . . . huchochewa na chuki,” asema Louis J. Freeh, mkurugenzi wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI). “Wale walio na chuki hiyo huchochewa na watu wenye chuki, hila, na ujinga.”

Uonevu. “Hatuna budi kukubali kwamba viongozi wa makundi na wa nchi fulani wana kusudi ovu la kuangamiza watu wa tamaduni nyingine,” aandika Stephen Bowman katika kitabu chake When the Eagle Screams. “Lakini ni wazi pia kwamba visa vingi vya kigaidi hufanywa na watu waliokata tamaa.”

Kukata tamaa. “Mara nyingi . . . magaidi wengi hutenda hivyo kwa sababu ya kukatishwa tamaa na hali ngumu za kisiasa, kijamii, na kiuchumi,” asema mhariri wa kitabu Urban Terrorism.

Ukosefu wa haki. “Ugaidi husababishwa na tatizo jingine,” asema Michael Shimoff katika makala yake yenye kichwa “Sera ya Ugaidi.” Aendelea kusema hivi: “Mradi wetu wapasa kuwa kukomesha hali za kijamii na za kisiasa zinazosababisha ugaidi. . . . Mbali na kupambana na ugaidi, ni sharti tujitahidi kwa udi na uvumba kudumisha uhuru, staha, haki, na heshima ya binadamu. Hatutaweza kukomesha ugaidi tusipojitahidi kudumisha mambo hayo.”

Visababishi na historia ya ugaidi imethibitisha ukweli huu wa Biblia: “Mtu mmoja anayo mamlaka juu ya mwenziwe kwa hasara yake.” (Mhubiri 8:9, Chapa ya 1989) Biblia ilitabiri pia sifa ambazo zimesitawisha ugaidi. Yasema hivi: “Katika siku za mwisho nyakati za hatari zilizo ngumu kushughulika nazo zitakuwa hapa. Kwa maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, . . . wasio na shauku ya kiasili, wasiotaka upatano wowote, wachongezi, wasio na hali ya kujidhibiti, wakali, wasio na upendo wa wema, wasaliti, wenye vichwa vigumu, wenye kututumuka kwa kiburi.”—2 Timotheo 3:1-4.

Ukweli ni kwamba jitihada za wanadamu za kukomesha ugaidi, hata ziwe za moyo mweupe jinsi gani, haziwezi kutatua matatizo yanayosababisha ugaidi. Biblia yasema hivi waziwazi: “Njia ya mwanadamu haimo katika nafsi yake; kuelekeza hatua zake si katika uwezo wa mwanadamu.” (Yeremia 10:23) Hata hivyo, Mungu anaweza kutatua tatizo la ugaidi, yeye si kama wanadamu wasiokuwa na uwezo.

Utatuzi

Wale ambao wamekata tamaa sana kwa sababu ya kudhulumiwa au kuonewa wanaweza kufarijiwa na ahadi hii hakika ya Biblia: “Maana wanyofu watakaa katika nchi, na wakamilifu watadumu ndani yake. Bali waovu watatengwa na nchi, nao wafanyao hila watang’olewa.”—Mithali 2:21, 22.

Ahadi hiyo ya Mungu itatimizwa hivi karibuni. Mtawala Wake, Mfalme Yesu Kristo anayemiliki atahakikisha imetimizwa. Unabii wa Biblia wasema hivi kumhusu Kristo: “Hatahukumu kwa kuyafuata ayaonayo kwa macho yake, wala hataonya kwa kuyafuata ayasikiayo kwa masikio yake; bali kwa haki atawahukumu maskini, naye atawaonya wanyenyekevu wa dunia kwa adili.”—Isaya 11:3, 4.

Naam, hivi karibuni Mwana wa Mungu, Yesu Kristo, atakomesha ukosefu wote wa haki pamoja na wote wanaousababisha. Katika mfumo mpya wa Mungu wa uadilifu, ugaidi na jeuri ya kila namna zitatokomea kabisa. Halafu kila mtu duniani ataishi kwa usalama, hatahofu madhara yoyote.—Ufunuo 21:3, 4.

[Picha katika ukurasa wa 12]

Biblia inaahidi kwamba hivi karibuni Mungu atakomesha uonevu wote na ukosefu wa haki