Je, Magereza Yanaendeleza Uhalifu?
Je, Magereza Yanaendeleza Uhalifu?
“Kuwashushia heshima na kuwavunja moyo wafungwa ndiyo njia mbaya zaidi ya kuwarekebisha wafungwa.”—SAFU YA MHARIRI KATIKA GAZETI THE ATLANTA CONSTITUTION.
MARA nyingi magereza huzuia uhalifu kwa muda mfupi tu. Je, kweli mfungwa anapoachiliwa huru huwa amelipia hasara iliyosababishwa na uhalifu aliotenda? Vipi wahasiriwa au wapendwa wao? “Mtoto wangu aliuawa,” akasihi Rita wakati mtu aliyemwua mwanawe mwenye umri
wa miaka 16 alipoachiliwa huru baada ya kufungwa gerezani kwa miaka mitatu tu. “Hebu tua kidogo na ufikirie jambo hilo. Ni vigumu sana kuwazia jinsi ninavyohisi.” Kama kisa cha Rita kinavyoonyesha, watu waliotendewa uhalifu huendelea kuteseka baada ya wahalifu hao kuhukumiwa na hata baada ya habari hizo kusahaulika.Hili ni suala linalowahangaisha wale waliotendewa uhalifu na watu wengineo wote. Kwa kuwa, utulivu wako na labda usalama wako unahusika iwe wafungwa walioachiliwa huru wamerekebishwa au wamekuwa wabaya zaidi baada ya kukaa gerezani.
Wahalifu Hujifunza Mbinu Mpya za Uhalifu Gerezani
Baadhi ya wahalifu huendelea na uhalifu baada ya kutoka gerezani. “Pesa nyingi zinapotumiwa kujenga magereza zaidi badala ya kuwarekebisha wahalifu, kwa kawaida hilo huongoza kwa uhalifu mbaya zaidi,” aandika Jill Smolowe kwenye gazeti Time. Maelezo ya Peter, * ambaye amekuwa gerezani kwa miaka 14 yapatana na maoni hayo. “Wafungwa wenzangu wengi waliiba vitu vidogo-vidogo mwanzoni, kisha wakaiba mali zenye thamani sana, na hatimaye wakaanza kuwatendea kinyama wanadamu wenzao,” yeye asema. “Wafungwa hao wanaona magereza kuwa kama shule ya kujifunzia mbinu mpya za uhalifu. Wanapotoka gerezani wanakuwa wahalifu hatari zaidi.”
Ingawa magereza hupunguza kwa muda idadi ya wahalifu mitaani, yaonekana kwamba magereza hayakomeshi uhalifu kwa vyovyote. Vijana wanaoishi kwenye mitaa mikubwa majijini huona kufungwa gerezani kuwa dalili ya ukomavu. Mara nyingi wengi wao wanakuwa wahalifu wabaya zaidi mwishowe. “Gereza halimrekebishi mtu hata kidogo,” asema Larry, ambaye amefungwa gerezani mara nyingi sana. “Wahalifu wanapoachiliwa huru wanaendelea kutenda mambo yaleyale.”
Ndiyo sababu uchunguzi mmoja nchini Marekani unaonyesha kwamba asilimia 50 ya visa vyote vibaya vya uhalifu hutendwa na asilimia 5 hivi ya wahalifu. “Mara nyingi wafungwa wanapokosa la kufanya, wanatumia wakati wao kusitawisha chuki, na kujifunza njia nyingine za uhalifu, ambazo . . . watatumia wanapoachiliwa huru,” lasema gazeti Time.
Ndivyo ilivyo katika nchi nyingine mbali na Marekani. John Vatis, daktari katika gereza la kijeshi nchini Ugiriki, asema: “Wafungwa wengi wanapotoka kwenye magereza yetu wanakuwa wakali zaidi, wajeuri, na wakatili zaidi. Wafungwa wengi huazimia kulipiza kisasi wanapoachiliwa huru.”
Matokeo kwa Jamii
Matatizo ya magereza huathiri hali yako ya kifedha. Kwa mfano, inakadiriwa kwamba kila mfungwa nchini Marekani hutunzwa kwa dola 21,000 hivi kila mwaka. Fedha hizo zinatokana na malipo ya kodi. Wafungwa wenye umri unaozidi miaka 60 hutunzwa kwa kiasi kinachozidi hicho kwa mara tatu. Kuna sababu nyingine zinazofanya raia wa nchi nyingi watilie shaka mpango wa magereza. Wengi
wanaogopa wahalifu wanaoachiliwa huru kabla ya kifungo kwisha. Wanaogopa pia wahalifu ambao kesi zao zinatupiliwa mbali kwa sababu ya kasoro fulani ya kisheria inayogunduliwa na wakili mwenye busara. Kwa kawaida, wale waliotendewa uhalifu hawahisi wamelindwa vya kutosha ili wasishambuliwe tena na mhalifu aliyeachiliwa huru. Na huenda wasiweze kujitetea mahakamani.Watu Wazidi Kuogopa
Sababu nyingine inayofanya watu wakose kutumaini mpango wa magereza ni kwa sababu wafungwa huishi chini ya hali mbaya sana. Hali hizo zimeelezwa kwenye sanduku lililoonyeshwa. Yaelekea wafungwa ambao wametendewa kinyama vifungoni hawawezi kurekebishwa. Vikundi kadhaa vinavyotetea haki za binadamu vinashangazwa pia na idadi kubwa ya wafungwa kutoka makabila yasiyopendwa. Vikundi hivyo vinauliza kama hali hiyo imetukia tu au imesababishwa na ubaguzi wa kikabila.
Ripoti moja ya mwaka wa 1998 ya Shirika la Habari la Associated Press ilieleza hali ya wale waliokuwa wafungwa katika Gereza la Holmesburg, huko Pennsylvania, Marekani, ambao waliomba kulipwa fidia kwa sababu ya kutumiwa kwa majaribio ya kemikali walipokuwa gerezani. Vipi kuhusu kuanzishwa tena nchini Marekani kwa mtindo wa kuwafunga wafungwa wengi kwa minyororo? Shirika la Amnesty International laripoti hivi: “Wafungwa hao waliofungwa minyororo hufanya kazi kwa muda wa saa 10 hadi 12 katika jua kali. Wao hupumzika kwa muda mfupi tu ili kunywa maji, na saa moja ili kula chakula cha mchana. . . . Wafungwa hao hujisaidia kwenye ndoo tu iliyozingirwa na kiwambo. Wafungwa hawafunguliwi minyororo wakati wa kujisaidia. Wafungwa wanaposhindwa kufikia ndoo wanajisaidia popote hadharani.” Lakini, magereza yote hayana mazoea hayo. Hata hivyo, kuwatendea wafungwa kinyama huwaletea aibu wafungwa na wale wanaotenda mambo hayo.
Je, Jamii Inafaidika?
Kwa wazi, jamii nyingi huhisi zikiwa salama wakati wahalifu hatari wanapofungwa gerezani. Jamii nyingine hupendelea magereza kwa sababu tofauti. Watu walilalamika sana wakati wenye mamlaka walipotaka kufunga gereza moja katika mji mdogo wa Cooma nchini Australia. Kwa nini? Kwa sababu wakazi wengi wenye shida ya kifedha waliandikwa kazi kwenye gereza hilo.
Hivi karibuni serikali nyingi zimebinafsisha magereza ili kupunguza gharama. Jambo la kusikitisha ni kwamba watu fulani hupata faida kutokana na kuwapo kwa wafungwa wengi waliohukumiwa vifungo virefu. Hivyo, watu wanapata faida kifedha kutokana na magereza.
Kwa ujumla, swali la msingi bado ni: Je, magereza yanawarekebisha wahalifu? Ijapokuwa kwa kawaida jibu ni la, utashangaa kujua kwamba wafungwa kadhaa wamesaidiwa kubadilika. Acheni tuone ilivyotukia.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 6 Baadhi ya majina katika makala hii yamebadilishwa.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 6, 7]
Hali Ilivyo Magerezani
MSONGAMANO: Haishangazi kwamba magereza nchini Uingereza yamesongamana watu sana! Uingereza ndiyo nchi ya pili yenye idadi kubwa zaidi ya wafungwa katika Ulaya Magharibi. Ina uwiano wa wafungwa 125 kwa kila watu 100,000. Huko Brazili, gereza kubwa zaidi jijini São Paulo linaweza kutoshea wafungwa 500. Badala yake lina wafungwa 6,000. Huko Urusi, vyumba vya magereza vinavyopasa kuwa na wafungwa 28 vina wafungwa wapatao 90 hadi 110. Hali ni mbaya sana kiasi cha kwamba wafungwa hulala kwa zamu. Katika nchi moja ya Asia, wafungwa 13 au 14 wamefungiwa kwenye chumba chenye ukubwa wa meta 3 za mraba. Na katika Magharibi mwa Australia, maofisa wa gereza wametatua tatizo la msongamano kwa kununua makontena ya kuwaweka wafungwa.
JEURI: Gazeti Der Spiegel la Ujerumani laripoti kwamba wafungwa wakatili huwaua na kuwatesa wafungwa wengine katika magereza ya Ujerumani. Kunakuwa na “mapambano ya makundi yanayofanya biashara haramu ya pombe na dawa za kulevya, ngono, na ulaji wa riba.” Mara nyingi chuki za kikabila husababisha jeuri gerezani. “Kuna wafungwa kutoka mataifa 72,” lasema gazeti la Der Spiegel. “Uhasama na mapambano yanayosababisha jeuri hayawezi kuepukwa.” Katika gereza moja huko Amerika Kusini, maofisa walisema kwamba kwa wastani wafungwa 12 waliuawa kila mwezi. Wafungwa walisema kwamba idadi ya wale waliouawa ilikuwa maradufu, likaripoti gazeti Financial Times la London.
KUTENDEWA VIBAYA KINGONO: Makala “Tatizo la Ubakaji Gerezani (The Rape Crisis Behind Bars),” katika gazeti la The New York Times yasema kadirio moja laonyesha kwamba huko Marekani, “zaidi ya wanaume 290,000 hutendewa vibaya kingono gerezani kila mwaka.” Ripoti hiyo yaendelea kusema hivi: “Hali ya kutisha ya kutendewa vibaya kingono ni jambo la kawaida tu.” Shirika moja lakadiria kwamba kila siku kuna visa vipatavyo 60,000 vya ngono zisizofaa katika magereza ya Marekani.
AFYA NA USAFI: Imethibitishwa kwamba magonjwa yaambukizwayo kingono yameenea sana magerezani. Watu wengi ulimwenguni wanajua kuwa wafungwa nchini Urusi na katika nchi fulani za Afrika huugua kifua kikuu. Inajulikana kote pia kuwa magereza mengi ulimwenguni hayaandai matibabu, si safi, wala hayaandai chakula kinachofaa.
[Picha]
Gereza lililosongamana watu huko São Pau
[Hisani]
AP Photo/Dario Lopez-Mills
[Picha katika ukurasa wa 4, 5]
Gereza lenye ulinzi mkali la La Santé huko Paris, Ufaransa
[Hisani]
AP Photo/Francois Mori
[Picha katika ukurasa wa 6]
Wanawake wakiwa gerezani huko Managua, Nikaragua
[Hisani]
AP Photo/Javier Galeano