Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Sanaa za Maua Huko Montreal

Sanaa za Maua Huko Montreal

Sanaa za Maua Huko Montreal

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI KANADA

TANGU Juni 19 hadi Oktoba 9, 2000, katika jiji lenye kupendeza la Kanada, Montreal, kulikuwa na onyesho la kwanza la kimataifa la maua ambayo yamepangwa katika mipangilio yenye nyuso tatu. Onyesho hilo linaitwa Onyesho la Kimataifa la Mpangilio wa Maua la Montreal 2000 (MIM 2000). Wasanii wa nchi 14 walialikwa kuunda na kubuni mipangilio 100 kwa kutumia maua. Mipangilio hiyo ya maua ilipatana na kichwa “Dunia Ina Rangi Nyingi.”

Kwa mamia ya miaka mimea imetumiwa kutokeza picha katika bustani za umma. Hata hivyo, kwa miaka 50 iliyopita wakuzaji wa maua katika nchi za Ulaya, China, na penginepo wametengeneza mipangilio ya maua yenye nyuso tatu kwa kupanga maua na mimea iliyochaguliwa kwa uangalifu kwenye viunzi vya metali vyenye miundo mbalimbali. Waliopanga onyesho hilo la MIM 2000 walianza tena kutumia usemi “mpangilio wa maua,” ambao awali ulitumiwa kuhusiana na mipangilio ya maua ya picha kwenye bustani za umma za Ufaransa. Kwa wakati huu, walitumia usemi huo kurejezea mipangilio ya maua ya picha na pia kuhusu mipangilio yenye nyuso tatu. Mimea milioni tatu, iliyochaguliwa kwa uangalifu, ilitumiwa katika onyesho la MIM 2000. Wakuzaji wa maua na mimea na watunzaji 68 wa bustani walifanya kazi ya kumwagilia maji na kutunza mipangilio hiyo.

Mipangilio ya China hasa ilivutia, kwa maana wasanii wake walisokota michanganyiko ya udongo, mbolea ya farasi, na mpunga mkavu kwenye kiunzi cha metali chenye nyuso tatu. Na walitumia mimea midogo sana yenye mizizi midogo ambayo haihitaji udongo mwingi.

Wasanii wote walioshindana katika onyesho la MIM 2000 walitaka kupata tuzo. Lakini watu waliozuru waliridhika kutazama tu ubuni na uzuri wa ajabu wa kila mpangilio. “Hiyo ndiyo sanaa,” akasema Lynn Duranceau, mkurugenzi wa mashindano hayo ya kimataifa. “Ni kama nyumba ndogo ya makumbusho. Tunaonea fahari onyesho hilo.”

[Picha katika ukurasa wa 24, 25]

Juu: Mpangilio wenye umbo la dubu wa Tibeti, China

Katikati: Jumba la kifalme la kale, Thailand, pamoja na kipepeo, China

Chini: Bata-mwitu, Quebec, Kanada

[Picha katika ukurasa wa 25]

Juu: Mpangilio wa maua unaoonyesha mchoro wa Vincent van Gogh, kutoka Kanada; tausi, kutoka Ufaransa