Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mamilioni Waliuawa—Je, Itatokea Tena?

Mamilioni Waliuawa—Je, Itatokea Tena?

Mamilioni Waliuawa—Je, Itatokea Tena?

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI SWEDEN

KATIKA Januari 26-28, 2000, viongozi wa Serikali na wawakilishi wa serikali wa nchi 48 walikusanyika katika mji mkuu wa Sweden ili kuhudhuria Mkutano wa Kimataifa wa Stockholm Kuhusu Mauaji Makubwa (wakati wa Unazi). Baadhi ya maelezo ya viongozi wa ulimwengu yalifichua kwamba wanahofia kwamba Unazi utatokea tena. Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Israel, Ehud Barak, alisema hivi: “Mkutano huu unatangazia watu wote duniani ujumbe huu: Hatupaswi kamwe, mahali popote duniani, kukubali utawala mwovu unaoua na kubagua watu wa dini, kabila, au rangi tofauti.”

Si Wayahudi tu Waliohusika

Watu wengi ulimwenguni hufikiri kwamba “Mauaji Makubwa” yaliathiri Wayahudi pekee. Hata hivyo, wengine waliathiriwa pia. Mkutano huo ulipoendelea Wayahudi walikuwa na ukumbusho wa Mauaji Makubwa kwenye Sinagogi Kuu la Stockholm. Ukumbusho huo ulitangazwa sana na vyombo vya habari. Na Waziri Mkuu wa Sweden alipendekeza kwamba hifadhi zote zenye nyaraka kuhusu Mauaji Makubwa zifunguliwe kwa umma ili kuelimisha watu juu ya tukio hilo. “Acheni watu wajue juu ya mauaji makubwa ya Waromani [Wazungukaji]. Wajue kuhusu mauaji makubwa ya walemavu, mnyanyaso na mauaji ya wanaume na wanawake wanaofanya ngono pamoja na watu wa jinsia yao, ya wapinzani wa serikali, na ya Mashahidi wa Yehova.”

Serikali ya Sweden imechapisha kitabu juu ya Mauaji hayo Makubwa chenye kichwa Tell Ye Your Children, (Waelezeni Watoto Wenu), ambacho kimegawanywa bila malipo kwa jamaa zote zenye watoto kotekote nchini. Kitabu hicho chaeleza kwamba Mashahidi wa Yehova “walikataa kula kiapo cha utii kwa Hitler na Serikali ya Unazi ya Ujerumani. Kukataa huko hakuna kifani kwa kuwa ikiwa wangalitia sahihi hati hiyo, wangaliachiliwa huru—hata hivyo, ni wachache tu waliofanya hivyo.”

Mauaji Makubwa na Mashahidi wa Yehova

Mnamo 1933, kulikuwa na Mashahidi wa Yehova 25,000 hivi nchini Ujerumani. Maelfu miongoni mwao walikuwa watu wa kwanza kufungwa katika kambi na magereza ya Wanazi. Walionyesha peupe kwamba, kama Wakristo hawangeunga mkono utendaji wowote wa kisiasa wala wa kijeshi. Hawakumsalimu Hitler kwa kusema “heil Hitler.” Walikataa kuunga mkono ubaguzi wa rangi wa Wanazi na kuingia katika chama cha kisiasa na kijeshi cha Hitler. Mashahidi 2,000 hivi walikufa, zaidi ya 250 kati yao waliuawa.

Isitoshe, Mashahidi waliofungwa walisaidia wafungwa wenzao kuvumilia, kutia ndani Wayahudi na wengineo. Waliwasaidia kuwa na tumaini la Biblia na kuwapa wagonjwa na wanyonge chakula. Mara nyingi waligawana nao kipande cha mwisho cha mkate walichokuwa nacho. Katika miaka ya mapema ya mnyanyaso wa Wanazi, walijulisha nchi nyingine kisirisiri juu ya kambi za mateso na mambo yaliyoendelea katika kambi hizo. Tangu wakati huo, magazeti yao yanayosambazwa duniani pote, Mnara wa Mlinzi na Amkeni!, yamekuwa na makala nyingi juu ya ujeuri wa Wanazi na vilevile masimulizi ya maisha ya wale waliookoka.

Wajumbe wa Mkutano wa Kimataifa wa Stockholm Kuhusu Mauaji Makubwa wanahofu kwamba Unazi unaweza kutokea tena. Profesa Yehuda Bauer, mkurugenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Uchunguzi wa Mauaji Makubwa kwenye Taasisi ya Wayahudi wa Kisasa, huko Israel, alisema hivi: “Imewahi kutukia, kwa hiyo, inaweza kutukia tena. Huenda isiwe Unazi utakaozuka tena, huenda isiwe watu walewale ndio watakaoathiriwa, huenda isiwe watu walewale watakaofanya tena ukatili huo, lakini mtu yeyote anaweza kumtenda mwingine jambo hilohilo. Haikuwa imetukia mbeleni, lakini sasa tunajua inaweza kutukia.”

[Picha katika ukurasa wa 12]

Kambini Mashahidi wa Yehova walitambuliwa kwa pembetatu ya rangi ya zambarau

[Picha katika ukurasa wa 12, 13]

1. Julius Engelhardt, mmoja wa Mashahidi wa Yehova aliyeuawa na Wanazi huko Brandenburg, Agosti 14, 1944

2. Mashahidi wa Yehova watatu wanarudi nyumbani baada ya kuachiliwa kutoka katika kambi ya Sachsenhausen, mwaka wa 1945

3. Elsa Abt, Shahidi ambaye alitenganishwa na binti yake mdogo na kufungwa kwa muda wa karibu miaka mitatu

[Hisani]

Nordrhein-Westfälisches Hauptstaatsarchiv, Düsseldorf

[Picha katika ukurasa wa 13]

Mashahidi waliookoka wanasimulia mambo yaliyowapata katika vidio hizi