Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Wauguzi kwa Nini Twawahitaji?

Wauguzi kwa Nini Twawahitaji?

Wauguzi kwa Nini Twawahitaji?

“Uuguzi ni mojawapo ya ustadi ulio mgumu sana. Huenda huruma ikawa kichocheo, lakini ujuzi ndio kipawa chetu pekee.” —Mary Adelaide Nutting, profesa wa kwanza wa uuguzi ulimwenguni, mwaka wa 1925.

UUGUZI ulianza zamani za kale—hata nyakati za Biblia. (1 Wafalme 1:2-4) Katika historia, wanawake wengi mashuhuri wameuguza wagonjwa. Kwa mfano, mfikirie Elizabeth wa Hungaria (1207-1231), binti ya Mfalme Andrew wa Pili. Alifanya mpango wa kugawanya chakula wakati wa njaa kali mwaka wa 1226. Baadaye, alipanga hospitali zijengwe, na humo akatunzia wenye ukoma. Elizabeth alikufa akiwa na umri wa miaka 24 tu, akiwa ametumia maisha yake mafupi kutunza wagonjwa.

Haiwezekani kuongea juu ya historia ya uuguzi bila kumtaja Florence Nightingale. Akiwa na kikundi cha wauguzi 38, bibi huyo Mwingereza aliye jasiri alipanga upya hospitali ya kijeshi huko Scutari, kiungani mwa Constantinople, wakati wa Vita ya Krimea ya mwaka wa 1853-1856. Alipofika huko, kiwango cha vifo kilikuwa karibu asilimia 60, alipoondoka mwaka wa 1856, kilikuwa chini ya asilimia 2.—Ona sanduku kwenye ukurasa wa 6.

Kichocheo kingine cha uuguzi kilikuwa chuo cha Institution of Protestant Deaconesses huko Kaiserswerth, Ujerumani, ambacho Nightingale alihudhuria kabla ya kwenda Krimea. Muda si muda, vikundi vingine vyenye kutokeza vya uuguzi vikasitawi. Kwa mfano, mwaka wa 1903, Agnes Karll alianzisha Shirika la Kitaalamu la Wauguzi Wajerumani.

Leo, wauguzi hujumuisha kile kionwacho kuwa kikundi kikubwa mno cha wataalamu katika mfumo wa utunzaji wa afya. Shirika la Afya Ulimwenguni laripoti kwamba sasa kuna wauguzi na wakunga zaidi ya 9,000,000 wanaofanya kazi katika nchi 141. Nao wanafanya kazi muhimu kama nini! Kichapo The Atlantic Monthly chaandika kwamba wauguzi “huchanganya kwa ufundi utunzi, ujuzi, na itibari, sifa ambazo ni muhimu sana ili mgonjwa apone.” Hivyo basi, kwa kufaa twaweza kuuliza hivi kuhusu wauguzi, Tungefanyaje bila wao?

Fungu la Mwuguzi Katika Kupona

Ensaiklopedia moja hufafanua uuguzi kuwa “utaratibu ambao kupitia huo mgonjwa anasaidiwa na mwuguzi apone ugonjwa au jeraha, au apate tena uhuru wake kadiri awezavyo.”

Bila shaka, mengi yahusika katika utaratibu huo. Unatia mengi zaidi ya uchunguzi wa kawaida, kama vile kuangalia mpigo wa moyo na msongo wa damu. Mwuguzi hutimiza fungu muhimu katika kupona kwa mgonjwa. Kulingana na The American Medical Association Encyclopedia of Medicine, “mwuguzi huhangaikia jinsi mgonjwa auonavyo ugonjwa wake kuliko kuhangaikia ugonjwa wenyewe, naye anashughulika na kuzuia maumivu ya kimwili, kupumzisha kuteseka kwa kiakili, na inapowezekana, kuepuka kuleta athari nyingine.” Kwa kuongezea, mwuguzi huandaa “utunzi wenye uelewevu, ambao hutia ndani kusikiliza kwa subira hali ya wasiwasi na hofu, na kuandaa tegemezo la kihisia-moyo na faraja.” Na mgonjwa anapoelekea kufa, kichapo hiki chasema kwamba, daraka la mwuguzi ni “kumsaidia mgonjwa akabili kifo bila mkazo mwingi sana na akiwa na heshima zake kadiri iwezekanavyo.”

Wauguzi wengi hufanya mengi zaidi ya wajibu wao. Kwa mfano, Ellen D. Baer aliandika juu ya kazi yake kwenye Kituo cha Kitiba cha Montefiore huko New York City. Hakutaka kuharakisha ziara zake za kuangalia waliopasuliwa. “Nilitaka kukaa na wagonjwa,” aandika. “Nilitaka kuwasaidia waboreshe hali yao ya kupumua, nilitaka kuwasaidia kutembea hapa na pale, kubadilisha bendeji, kujibu maswali yao, kuwaelezea mambo, na kuwafariji. Nilifurahia kuwa na uhusiano mzuri pamoja na wagonjwa.”

Hapana shaka kwamba yeyote ambaye amekuwa mgonjwa hospitalini anaweza kumkumbuka mwuguzi mwenye huruma aliyekuwa na roho hiyohiyo ya kujitolea. Lakini ni nini kinachohusika ili mtu awe mwuguzi stadi?

[Picha katika ukurasa wa 3]

Florence Nightingale

[Hisani]

Courtesy National Library of Medicine