Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kujitahidi Kunenepa kwa Sababu ya Hofu

Huku wakihofu kwamba watadhaniwa kimakosa kuwa na UKIMWI, “baadhi ya wanawake wanaoishi kaskazini ya Kamerun hutumia sana madawa yanayonenepesha,” yataarifu ripoti moja kwenye gazeti Le Messager la Douala, kama ilivyochapishwa katika gazeti Courrier International. “Habari huenea kasi sana mtu mgonjwa anapokonda, na watu huona kukonda kuwa dalili dhahiri kabisa ya UKIMWI.” Huo huitwa pia ugonjwa wa kukonda barani Afrika. Madawa yanayouzwa kimagendo, yanatumiwa “bila maagizo yoyote ya daktari,” chasema chanzo hicho kutoka Afrika. Hata hivyo, wanawake vijana wembamba wanahofia uvumi na kutengwa na jamii kwa sababu ya kudhaniwa kuwa na virusi vya UKIMWI kuliko wanavyohofia hatari inayoweza kusababishwa na madawa hayo.

Je, Ni Uthibitisho wa Ziara ya Paulo Huko Saiprasi?

“Waakiolojia Waitalia katika Pafosi, pwani ya kusini-magharibi ya Saiprasi yenye mawemawe na jua kali, wanasema kwamba wamegundua vifaa vya kale zaidi vinavyothibitisha kuwapo kwa Paulo katika kisiwa hicho,” chasema kichapo Biblical Archaeology Review. “Kufikia sasa, ni Agano Jipya tu lililoeleza kuhusu ziara ya huyo mtume, nalo lasema kwamba wakati wa safari yake ya kwanza ya umishonari, Paulo ‘alisafiri kwa mashua kwenda Saiprasi,’ ambako alivuka ‘kisiwa chote hadi Pafosi’ (Matendo 13:4-6).” Uthibitisho huo watia ndani kipande cha bamba la marumaru lenye maneno mawili ya Kigiriki. Neno la juu ni “LOY,” na chini yake kuna “OSTO.” Maneno hayo yamerekebishwa na waakiolojia ili yasomeke (PAU)LOY (AP)OSTO(LOY),” au “Paulo mtume,” nao wasema yaliandikwa katika karne ya kwanza au ya pili W.K. “Kipande hicho cha Pafio [Paphos] chatuwezesha kuchora upya ramani ya safari za Paulo,” akasema Filippo Giudice, kiongozi wa kikundi hicho cha waakiolojia.

Kuita Jamii Mpya kwa Jina Lako

“Je, unatafuta zawadi ya pekee sana kwa ajili ya wapendwa wako ambao yamkini wana kila kitu?” lauliza gazeti la Science. “Kuna msaada. Kwa kutoa mchango kwa ajili ya utafiti wa viumbe mbalimbali, jamii zisizojulikana awali za okidi, au mbu, au konokono wa baharini zaweza kuitwa kwa majina ya wapendwa wako na kuandikwa kwenye vichapo vya kisayansi ili yadumu.” Au zaweza kuitwa kwa jina lako. Utafiti wa hivi karibuni wadokeza kwamba ni idadi isiyozidi asilimia moja kwa kumi tu ya jamii zilizopo leo ambazo zimeelezwa kwenye vichapo vya kisayansi. Maelfu ya jamii zilizokusanywa zimehifadhiwa pasipo majina kwenye saraka za majumba ya ukumbusho, zikisubiri kupewa majina na kuelezwa kwenye jarida la kisayansi. Sasa watu wanaweza kufungua kituo fulani katika Internet na kutazama picha za viumbe ambao maelezo yao yako tayari kuchapishwa lakini hawana majina. Kisha, kwa kutoa mchango wa dola za Marekani 2,800 au zaidi, wanaweza kuwapa majina ya Kilatini jamii wanazochagua. Hivyo ndivyo shirika linaloitwa BIOPAT linavyonuia kuchanga fedha za kuainisha na kuhifadhi jamii mpya za viumbe.

Watoto Wahasiriwa

“Kila siku, . . . wavulana na wasichana 30,500 wenye umri usiozidi miaka mitano hufa kutokana na visababishi vinavyoweza kuzuiwa,” lasema shirika la Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa katika ripoti yake ya The State of the World’s Children 2000. Gazeti la Indian Express laripoti kwamba “takriban watoto milioni mbili wameuawa na milioni sita kujeruhiwa au kulemazwa katika mapambano ya silaha katika mwongo uliopita na mamilioni wengine wangali wanatendwa vibaya na watu wanaokiuka haki za binadamu.” Zaidi ya watoto milioni 15 ni wakimbizi, na zaidi ya milioni moja wametengwa na wazazi wao au ni mayatima. Pamoja na hayo, ripoti hiyo yataja uchunguzi uliofanywa na Shirika la Wafanyakazi Ulimwenguni unaoonyesha kwamba angalau watoto milioni 250 wenye umri wa kati ya miaka 5 na 14 wanatumikishwa kazi za sulubu, asilimia 20 kati yao hutumikishwa chini ya hali hatari sana. Takriban watoto milioni moja ulimwenguni pote wanashurutishwa kuwa makahaba, na watoto 250,000 huambukizwa virusi vya UKIMWI kila mwezi. Na watoto milioni 130—thuluthi mbili wakiwa wasichana—hawaendi shuleni.

Biblia ya Kisasa Iliyoandikwa kwa Mkono

Kazi ya kutayarisha Biblia maridadi sana iliyoandikwa kwa mkono imeanza, itahitaji muda wa miaka sita na gharama ya dola milioni tatu hivi za Marekani. Ilianzishwa rasmi na watawa wa kiume wa shirika la St. Benedict katika Chuo Kikuu cha St. John huko Minnesota, Marekani. Mwandishi Mwingereza Donald Jackson anasimamia kikundi kidogo cha waandishi wanaomsaidia kufanya kazi hiyo katika karakana yake huko Wales. Wanaandika kwenye karatasi ya ngozi, kwa kutumia unyoya wa bata-bukini na kijiti cha kale cha Kichina na wino uliotengenezwa kutoka kwa masizi mabichi laini yaliyochanganywa na gundi. Hati ya mkono iliyobuniwa kwa njia ya pekee kwa ajili ya kazi hiyo itachapishwa kutoka kwa kompyuta kisha kunakiliwa kwa mkono, itaongezwa picha na herufi maridadi baadaye. Biblia nzima itakuwa na mabuku saba, na zaidi ya kurasa 1,150, kila ukurasa ukiwa na urefu wa sentimeta 60 na upana wa sentimeta 40. Biblia iliyoteuliwa kwa ajili ya kazi hii ya pekee ambayo haijafanywa tena kwa muda wa miaka 500, ni tafsiri ya Kiingereza ya New Revised Standard Version. Lakini mpangilio wa vitabu vya Biblia umebadilishwa, buku la kwanza litaanza na Gospeli. Baadaye, nakala 100 za tafsiri inayonuiwa watu wanaopenda kukusanya Biblia mbalimbali zitatolewa, seti moja itagharimu kati ya dola za Marekani 60, 000 hadi 80,000.

Uchafuzi Hauepukiki, Haidhuru Uvutaji-Sigareti

Ripoti moja ya taasisi ya Tata Institute of Fundamental Research, katika Mumbai, yasema kwamba watoto wengi wanaovuta sigareti katika India huanza kuvuta wakiwa na umri mchanga sana. Kwa wastani, watoto wa mitaani wasiotunzwa na wazazi huanza wakiwa na umri wa miaka 8, ilhali watoto wanaoenda shuleni wanaotunzwa huanza wakiwa na umri wa miaka 11. Hata hivyo, uchunguzi mwingine huko Mumbai ulionyesha kwamba watoto waliotunzwa ifaavyo na wazazi na ambao hawavuti sigareti walikuwa wakipumua vichafuzi vinavyolingana na kuvuta paketi mbili za sigareti kila siku! Kama ilivyoripotiwa kwenye gazeti la The Asian Age, Mumbai na Delhi ni miongoni mwa majiji matano yenye uchafuzi mkubwa zaidi ulimwenguni. Kukiwa na takriban magari 900,000 yanayozunguka kila siku katika jiji la Mumbai na mengine 300,000 yanayotoka na kuingia jijini kila siku, yaripotiwa kwamba viwango vya uchafuzi wa hewa, ni asilimia 600 hadi 800 zaidi ya viwango vinavyokubaliwa na Shirika la Afya Ulimwenguni.

Wanyama wa Pori Wapikwa Huko China

Wanyama wa pori wa China wako hatarini kwa sababu ya “mabadiliko ya mitindo ya maisha na milo ya kawaida,” lasema gazeti la Down to Earth. Kuenea kwa maoni ya kwamba wanyama fulani wa pori huboresha afya wanapoliwa kuliko vyakula vingine kumetokeza uhitaji mkubwa wa milo isiyo ya kawaida. Nyoka ndio wanaopendwa sana, bei ya nyoka wenye sumu ni maradufu ya bei ya nyoka wasio na sumu. Nguruwe-mwitu, ngawa, chura, ngele, chatu, kakakuona, swala wa Tibet, na ndege adimu wote hao wanapendwa sana na hupikwa kwenye mikahawa kotekote katika China. Wengi wa viumbe hao wako katika hatari ya kutoweka, na hivyo wanastahili kuhifadhiwa na serikali. Na bado, baadhi ya wamiliki wa mikahawa huweka ishara zinazowahakikishia wateja wao kwamba wanyama wanaopikwa humo ni wa porini kikweli wala si wa kufugwa wala kukuzwa kwenye maabara. Serikali ya China imeanzisha kampeni ya kuhifadhi wanyama wa pori kutokana na watu wanaojitwika utaalamu wa mapishi hayo na inatumia wito wa, “Kataa katakata kula wanyama wa pori.”

Ni Hatari kwa Ndege

“Majengo ya ofisi na minara ya mawasiliano ya Amerika Kaskazini inaua pasipo kujulikana,” lataarifu gazeti la The Globe and Mail la Toronto, Kanada. “Yaaminika kwamba ndege milioni 100 hufa kwenye bara hilo kila mwaka kwa sababu ya kujigonga kwenye majengo, na kwenye madirisha ya nyumba.” Taa za ofisi zinazoachwa zikiwaka usiku hutatanisha isivyoelezeka uwezo wa kusafiri wa ndege wanaohama. Wataalamu wanasema kwamba tatizo hilo limeenea sana. “Tatizo hilo limeenea kila mahali nchini, na barani,” asema mtaalamu wa elimu ya ndege David Willard. Vikundi kama vile Fatal Light Awareness Program cha Toronto vinajitahidi kuwaelimisha wafanyakazi wa ofisini wawe wakizima taa za ofisini usiku.

Isitoshe, taa za angani zenye mwanga mkali—zinazomulika huku na huku angani ili kuwavutia watu kwenye madisko au sehemu nyingine za burudani—hukanganya wanyama wanaosafiri usiku, laripoti gazeti la kila siku la Frankfurter Allgemeine Zeitung la Ujerumani. Taa hizo hutatanisha mfumo tata wa usafiri wa ndege na popo. Kwa sababu ya kuvurugika, ndege wameonekana wakiharibu utaratibu wao wa kuhama, wakibadili mwelekeo, wakilia kwa wasiwasi, na hata kukatiza kuhama kwao. Nyakati nyingine ndege waliopotea, hutua kwa uchovu baada ya kuzunguka kwa muda mrefu angani, na hata wale walio dhaifu hufa. Taasisi ya Kuhifadhi Ndege iliyoko Frankfurt imeomba taa za angani zenye mwanga mkali zipigwe marufuku.