Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

“Mkazi wa Msituni Mwenye Kuvutia Kuliko Wote”

“Mkazi wa Msituni Mwenye Kuvutia Kuliko Wote”

“Mkazi wa Msituni Mwenye Kuvutia Kuliko Wote”

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA SWEDEN

MARA ya kwanza nilipomwona yule aitwaye na watu fulani hapa, “mkazi wa msituni mwenye kuvutia kuliko wote,” ilikuwa siku fulani, mwezi wa Juni. Mkazi huyo ni yule bundi mkuu wa kijivu, ambaye nyakati nyingine huitwa bundi wa Lapland.

Bundi huyo mkubwa sana mwenye kustaajabisha hukaa sehemu fulani-fulani za Finland na sehemu ya kaskazini mwa Sweden hali kadhalika sehemu ya mbali zaidi upande wa mashariki huko Siberia, Alaska, na Kanada. Yeye hupenda kujificha naye hapatikani kwa urahisi iwapo hujui kilipo kiota chake. Mara ukionapo kiota hicho, utapata pia kujua kwamba bundi huyo si mwoga hata kidogo.

Kumchunguza Mwindaji Huyo

Niliwahi kumchunguza bundi wa kiume wa Lapland mwenye alama zenye kuvutia, alipokuwa akitafuta chakula. Angeruka ghafula kutoka katika tawi la mti na kujaribu kumkamata panya. Wadhani alifaulu kukamata windo lake? Bila shaka, ndiyo! Ningeweza kumwona waziwazi mnyama mdogo akining’inia kwenye kucha za ndege huyo, alipokuwa akiruka juu polepole, kwa njia yenye kuvutia, kwa mabawa yake yapanukayo kufikia sentimeta 140.

Bundi wa Lapland hawazaani kwa ukawaida kila mwaka kama wafanyavyo bundi wengine wengi. Bundi huyo mkubwa sana hula wanyama wadogo tu, kwa hiyo miaka fulani, wakati hakuna wanyama wa kutosha, bundi hao huacha kuzaana kabisa. Miaka mingine, kunapokuwa na chakula tele, kila kiota chaweza kuwa na makinda wanne au zaidi.

Kumteua Mwenzi

Masika ndio wakati wa bundi kupandana, naye bundi wa kike humteua mwenzi wake kwa uangalifu, ingawa hahangaikii hasa sura yenye kupendeza ya bundi wa kiume—kama wafanyavyo wanawake walio wengi. Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na wachunguzi fulani wa ndege, lazima bundi wa kiume aonyeshe kwamba yeye ni mwindaji stadi. Kabla ya kufanya mipango yoyote ya kuwa na familia, lazima amwandalie bundi wa kike chakula.

Ikiwa kuna panya tele naye bundi wa kiume ni stadi wa “kutafuta riziki,” chakula anachompa bundi wa kike kitamnonesha. Ni kana kwamba unono wake huujulisha mwili wake kiasi cha mayai atakayotaga.

Kisha, bundi wa kiume peke yake ndiye huenda mawindoni, jambo ambalo huhitaji nguvu nyingi. Bundi huyo wa kiume huhimizwa na sauti yenye kusihi ya bundi wa kike, kwa kuwa nguvu zake zote zatumiwa kutaga mayai na kuyakalia.

Kukipata Kiota

Darubini yangu iliniwezesha kumwona bundi wa kiume mwenye kuvutia alipokuwa katika kawaida zake za kuruka akiwa amebeba windo. Hatimaye, nilifaulu kukipata kiota. Bundi wa Lapland hawajengi viota vyao wenyewe lakini mara nyingi hurithi viota vya vijiti vidogo-vidogo, vya ndege wengine wawindaji wanaoishi msituni. Ikiwa hakuna kiota chochote, bundi huyo aweza kutumia kisiki kilichokauka.

Ndani ya kiota hicho, nilipata makinda wawili wadogo wenye manyoya mororo, wakikodoa macho na kushangazwa na kila kitu kinachowazunguka. Wakitoa sauti za kusihi, waligeuka na kumtazama mama yao, aliyekuwa ameketi karibu akiwatazama. Kukaribia makinda hao wakati huo kungeweza kuwa hatari. Bundi wa kike akidhani kwamba makinda wake wanatishwa, ataruka kimyakimya na kumshambulia anayewaingilia kwa kucha zilizo kali kama sindano. Kwa hiyo wapaswa kuwa mwangalifu na kuwachunguza bundi ukiwa mbali.

Kula na Mazoezi

Alipofika kwenye kiota, bundi wa kiume alilihamisha windo toka kuchani hadi mdomoni na kumkabidhi kinda mmoja panya huyo. Kula kwa kinda mmoja huambatana na sauti za ndege atakayekula baada yake.

Baada ya kinda kula mlo wake alioutamani, hubadili tabia kwa njia yenye kuchekesha. Kufikia wakati huo, alikuwa mchangamfu na chonjo, lakini abadilika ghafula, na kuanza kutenda kana kwamba amelewa! Nguvu zake zote zatumiwa kusaga chakula, na punde si punde azimia na kujikunyata hivi kwamba aonekana kama fungu la manyoya mororo tu. Kinda mwingine, aliye karibu zaidi naye aanza kuchangamka polepole naye aelekea kulevuka kutokana na ulevi uliosababishwa na chakula alichokula mara ya mwisho.

Hiyo ndiyo kawaida ya mambo hadi katikati ya mwezi wa Juni. Kufikia wakati huo makinda hao watakuwa wamefikia umri wa majuma manne nao waweza kupapatika na kutoka kwenye kiota chao, wakihimizwa na sauti ya mama yao. Mwanzoni, wao hupanda miti, kwa ustadi mkubwa. Juu mtini, wanyama wawindaji si wengi kama walivyo ardhini.

Hatimaye, makinda hao hujizoeza kwa kuruka toka tawi moja hadi jingine wakitumia mabawa yao. Muda si muda, wanasitawisha uwezo wao wenyewe wa kuruka na kuwinda. Sura yao pia hubadilika, hivi kwamba hata wao wapata kuonwa kuwa ‘wakazi wa msituni wenye kuvutia.’

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 18]

© Joe McDonald

© Michael S. Quinton

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 19]

© Michael S. Quinton

© Michael S. Quinton