Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Miaka Hamsini Nikichora Picha Kwenye Kauri

Miaka Hamsini Nikichora Picha Kwenye Kauri

Miaka Hamsini Nikichora Picha Kwenye Kauri

KAMA ILIVYOSIMULIWA NA ALFRED LIPPERT

MAMA alitaka niwe seremala. Lakini mwalimu wangu wa shule alimsihi anitafutie kazi katika kiwanda cha kutengeneza kauri, karibu na nyumbani kwetu Meissen, Ujerumani. Kwa nini alisisitiza sana jambo hilo? Alinichunguza akatambua kwamba nina kipawa cha kuchora. Nampenda mama yangu, lakini nafurahi kwamba mwalimu wangu alifaulu kumshawishi mama akubali. Hivyo, nikiwa na umri wa miaka 14, nilianza kujifunza kuwa mchoraji wa mojawapo ya kauri zilizotengenezwa kwa mkono zilizo nzuri zaidi ulimwenguni.

Kauri imekuwa ikitengenezwa Meissen, kwa miaka ipatayo 300. Kiwanda cha kwanza huko Ulaya cha kutengenezea kauri halisi kilianzishwa mwaka wa 1710. Miaka 30 hivi baadaye, kiwanda hicho kilianzisha shule ambayo vijana wangeweza kujifunza sanaa ya kuchora kauri. Shule hiyo, ambayo hadi sasa ingalipo na inasimamiwa na Kiwanda cha Kauri cha Meissen, ndipo nilipochora kwa wasiwasi mwingi picha yangu ya kwanza nikiwa mchoraji wa kauri.

Kwenye shule hiyo pia nilijifunza stadi bora kabisa za kuchora picha za maua, miti, wanyama na ndege. Mtalaa huo ulikuwa msingi kwa kazi yangu ya baadaye.

Iliyong’arishwa au Isiyong’arishwa?

Kauri ni udongo mwepesi unaong’aa unaoweza kuchorwa katika njia mbili kuu. Mchoro waweza kuchorwa kabla udongo huo haujang’arishwa. Lakini kauri ambayo haijanga’rishwa hunyonya na kufyonza rangi, kwa hiyo mchoro huo hutaka mtu amakinike vilivyo, kwani makosa mengi hayawezi kurekebishwa. Kwa upande mwingine, kauri yaweza kupakwa rangi baada ya kung’arishwa. Kazi yangu ikawa kuchora mapambo ya maua kwa njia hiyo. Kazi hiyo ilihusisha si kupaka rangi tu bali pia kubuni shada tofauti kwa kila chombo cha kauri. Kwa hiyo mpakaji-rangi, baada ya kujifunza kukaza akili yake na kuepuka vikengeusha-fikira, hujifunza kutumia akili yake ili kubuni kitu maridadi.

Baada ya kuchora picha za maua kwa miaka kadhaa, hatimaye nilifanya maendeleo hadi kufikia sehemu iliyo ngumu zaidi kuliko zote—kuchora picha za viumbe. Hapa ndipo niliponufaika na masomo yangu ya kwanza ya kuchora wanyama na ndege.

Jambo Gumu Linalosisimua Zaidi

Kuchora wanyama, samaki, na ndege ni jambo gumu linalosisimua kwa sababu kila kiumbe anapaswa kuonekana kana kwamba yuko hai, si tuli kama ua au mti. Msanii apaswa kujua habari fulani kuhusu mwili na mazoea fulani ya wanyama na ndege anaochora. Mathalani, mandhari nyingi ninazochora huonyesha wanyama wa porini, kutia ndani paa dume wenye pembe kubwa sana.

Njia bora zaidi ya kujifunza juu ya wanyama, ni kuwachunguza binafsi. Miaka kadhaa iliyopita nilipanga kuchora mfululizo wa picha za samaki, kwa hiyo nilinunua tangi la samaki la nyumbani na kuweka kila aina ya samaki. Mimi na mke wangu tuliketi karibu na tangi hilo la samaki kwa saa nyingi, tukichunguza nyendo na mazoea ya kila aina ya samaki. Nilianza kuwachora tu baada ya kuwafahamu.

Ni Nini Humfanya Mtu Awe Mchoraji Hodari?

Nyakati nyingine marafiki huniuliza ni nini humfanya mtu awe mchoraji hodari wa kauri. Ni wazi kwamba mchoraji anahitaji kuwa na kipawa cha usanii, jicho makini sana, na mkono thabiti. Lakini anahitaji mengi zaidi. Ili msanii afaulu, anahitaji kuwa na mtazamo unaofaa kujielekea yeye mwenyewe, kazi yake, na watu wengine. Mchoraji hodari ni msanii anayejizoeza kufanya kazi kwa bidii ili kuboresha stadi zake. Anajua kwamba asipotumia stadi zake atazipoteza. Hakomi kujifunza kamwe, kwa kuwa yeye husikiliza yale ambayo wengine husema na kukubali shauri lao.

Jambo moja la mwisho. Msanii mwenye uzoefu huzingatia mapendezi ya mteja. Watu wanaonunua kauri iliyotengenezwa kwa mkono hawataki tu kitu cha kawaida kitakachohifadhiwa kwa muda mfupi kisha kutupwa na mahali pake pachukuliwe na kitu kingine. Mteja hutaka kitu fulani cha sanaa, kitu chenye thamani katika utamaduni—kitu kinachovutia, kinachoufurahisha moyo, na kuboresha maisha ya mwenye kukimiliki. Mchoraji hufurahi kushiriki kutosheleza tamaa hizo.

Uchoraji Waongoza Kwenye Imani Katika Mungu

Kazi yangu ya uchoraji ilinichochea niichunguze Biblia zaidi na kusitawisha imani thabiti katika Mungu. Jinsi gani? Naam, nyakati nyingine nimefanya kazi na wataalamu wa ndege, nikichora picha kwa ajili ya vitabu walivyokuwa wakiandika. Nilipoanza kuchora picha hizo, niliamini mageuzi. Lakini kushirikiana kwa ukaribu na waandishi kadhaa kulitokeza mazungumzo kuhusu asili ya uhai. Mazungumzo hayo yalibadili mtazamo wangu.

Jambo lililonisumbua sana ni wazo la kwamba ijapokuwa wataalamu wote waliamini mageuzi, kila mmoja wao alikuwa na nadharia yake mwenyewe, ambayo mara nyingi ilipingana na ya wataalamu wale wengine. Kwa kadiri nionavyo, hakuna nadharia ya mageuzi yenye upatano. Hivyo, nilifikia mkataa kwamba ikiwa wataalamu hawawezi kukubaliana juu ya ufafanuzi mmoja wa mageuzi, vipi juu ya watu wengine? Kama tokeo, nikaacha kuamini mageuzi. Jambo pekee lililo badala ya mageuzi ni kwamba uhai ulioko duniani uliumbwa. Hapo ndipo imani yangu katika Muumba wetu ilipoanzia.

Sasa ninafurahi sana kwa sababu watu wanapendezwa na kazi yangu, na jambo hilo huniridhisha. Upendo nilio nao kwa kazi ya uchoraji au kwa kauri hautakoma kamwe.

[Picha katika ukurasa wa 17]

Picha kwenye ukurasa wa 16 na 17: Mit freundlicher Genehmigung der Staatlichen Porzellan-Manufaktur Meissen GmbH