Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuzuru “Jiji la Kale Zaidi la Urusi”

Kuzuru “Jiji la Kale Zaidi la Urusi”

Kuzuru “Jiji la Kale Zaidi la Urusi”

MIMI na mke wangu Linda, tuliwasili Moscow Julai 1998 tukiwa kwenye mgawo wa kazi. Hatukuwa tumewahi kufika Urusi hapo awali, hivyo tulikuwa na hamu ya kujifunza mambo fulani kuhusu nchi hiyo, lugha yake, na watu wake.

Punde tu baada ya kuwasili, niliona picha yenye kupendeza upande wa nyuma wa noti ya kijani-kibichi ya rubo tano. Ilikuwa na kitu kilichoonekana kama ngome ya matofali ya karne ya 14 au ya 15 iliyoelekeana na mto, kukiwa na kisiwa na ziwa nyuma yake. Kwenye kona paliandikwa jina la mahali hapo: Novgorod.

Niliuliza wakazi wa Moscow kuhusu jina hilo. Wote walifahamu Novgorod, lakini ni mmoja tu kati ya wale niliouliza ambaye alipata kufika huko. Niliambiwa kwamba ni mwendo wa kilometa zisizozidi 550 kutoka Moscow, safari ya usiku mmoja kwa garimoshi kuelekea St. Petersburg. Mimi na mke wangu tukaamua kwenda.

Twasafiri Hadi Novgorod

Kwa kuwa niliwahi kununua tiketi za St. Petersburg hapo awali, nilijua mahali pa kuzinunua. Namba ya behewa na chumba chetu zilichapwa kwenye tiketi. Tuliwasili kwenye stesheni ya garimoshi muda mfupi tu baada ya saa tatu jioni moja mnamo Septemba iliyopita na kukaa kwenye chumba chetu cha faragha katika behewa namba 5.

Baada ya mngurumo na mshtuko, gari hilo lilianza kusonga mbele. Garimoshi la umma tulilopanda lilitenda vivyo hivyo usiku kucha, lilipokuwa likisimama kwenye vituo. Tulisimama, kisha baada ya dakika chache, garimoshi jingine likapita. Dakika chache zilipita garimoshi likingoja kwenye reli iliyo kando katika usiku mtulivu. Kisha breki ziliachiliwa, na behewa letu likatoa kelele za kila namna na kufuatana na mabehewa mengine. Kisha nikalala tena.

Mhudumu wa kike kwenye behewa alibisha mlango wetu kabla tu hatujafika Novgorod. Kulikuwa na shamrashamra nyingi kwenye stesheni ya garimoshi, hata saa moja asubuhi. Kwenye kibanda cha kuuzia magazeti, tulipata ramani ya jiji hilo na pia tukamwuliza karani wa mauzo teksi ingegharimu pesa ngapi hadi kwenye hoteli tulimoishi. Tulimlipa dereva wa teksi hiyo rubo 20 na akatubeba katika gari lake lililotengenezewa Urusi aina ya Lada hadi kwenye hoteli yetu ng’ambo ya Mto Volkhov—mto uliokuwa kwenye picha.

Dereva huyo alituambia kwamba yeye hakuwa Mrusi ila mkewe. Ndiyo sababu anaishi Urusi. Tulikaribishwa na mpokea-wageni kwenye hoteli hiyo na hata akaturuhusu kusajili majina yetu ingawa ilikuwa ni saa 1:30 asubuhi. Alitupa madokezo ya mahali tunapoweza kwenda. Tulitembea kandokando ya mto kisha tukapata kifungua-kinywa.

Tuliona bustani yenye nyasi zilizokatwa vizuri na miti iliyopunwa. Mahali pa matembezi kandokando ya mto paling’aa kwa matuta mazuri ya maua. Ijapokuwa kulikuwa na watalii—basi lililotengenezewa Korea lililokuwa likija pindi kwa pindi, liliwasili na kikundi cha watalii—Novgorod si mji wa watalii. Wengi wa watu tuliowaona walikuwa Warusi.

Tuliambiwa na wakazi wengi wa hapo kwamba Novgorod ndilo jiji la kale zaidi la Urusi. Inasemekana kuwa limedumu kwa miaka zaidi ya 1,100. Urithi wake wa kidini waonyeshwa na makumi ya makanisa ya zamani yaliyo katika jiji lote. Kwenye ramani moja, Linda aliona makanisa 25 katika eneo linalozunguka hoteli hiyo tu.

Tuliona mnara ndani ya kremlin—si Kremlin iliyo Moscow; “kremlin” ni neno la Kirusi linalomaanisha “ngome ya jiji.” Kulikuwa na njia ya kufika kwenye kilele cha mnara huo. Kwa kulipa rubo 5, (zisizozidi senti 20 za Marekani) tuliruhusiwa kupanda ngazi zinazozunguka hadi kileleni. Nililinganisha mandhari hiyo na picha iliyo kwenye noti ya rubo tano. Miti ilikuwa imekua, na njia ya kutembelea ya ukuta wa kremlin ilikuwa imefunikwa. Lakini, kulikuwa na Mto Volkhov—mto uleule na kisiwa kilekile na ziwa lililokuwa upande wa nyuma. Ni kreni pekee iliyokuwa ikichimba mto huo ndiyo iliyokosekana kwenye picha hiyo.

Tuliona kitu cha kutazamisha siku ya pili tukiwa Novgorod. Ingawa Warusi huona jiji hilo kuwa dogo—licha ya idadi ya watu 250,000—watu wake walitukumbuka na kukumbuka mapendezi yetu! Mhudumu wa kike kwenye hoteli alitukumbuka kutoka siku iliyotangulia. Alikumbuka kwamba tunapenda kahawa, na alizidi kutuletea. Pia alikumbuka kwamba hatukutaka maji ya matunda kwa hiyo siku ya pili hakutuuliza ikiwa tuliyataka. Nilipoomba cheki, Olga—nakumbuka jina lake—alitabasamu na kusema, huku akinitazama uso, “Ni chumba namba 356, sivyo?”

Jumapili watu walifurika huko kremlin, daraja la kuvukia kwa miguu ng’ambo ya Mto Volkhov, barabarani, na mahali pa matembezi. Linda alienda kununua bisi kutoka kwa mchuuzi wa barabarani karibu na daraja hilo la kuvukia kwa miguu, ambaye—kama unavyoweza kukisia!—alimkumbuka tangu siku iliyotangulia.

Tuliporudi tena kupanda mnara ili kuona mandhari, msichana aliyekuwa akikusanya pesa za kiingilio alituonyesha tabasamu na kusema: “Mlikuwa hapa jana, ama sivyo? Kwa kuwa tayari mlilipa jana, hamhitaji kulipa tena.”

Tulikutana na David, rafiki tuliyemjua miaka kadhaa huko New York. Alikuwa ameoa msichana Mrusi, Alyona, na sasa walikuwa wakiishi Novgorod, wakitumikia wakiwa wahudumu katika kutaniko moja la Mashahidi wa Yehova. Tulikutana mbele ya Mkahawa wa Detinets, ambao umejengwa ukutani kwenye kilele cha kremlin. Tulipewa chakula bora zaidi cha Urusi tulichopata kula. Mbali na hilo kilikuwa cha bei nafuu. Milo yenye sehemu tatu (kachumbari, mchuzi, mlo mkuu, kahawa, na kitindamlo) iligharimu takriban dola 6 za Marekani.

Novgorod ni jiji lililo na watu wenye urafiki waliotukumbuka, lenye chakula bora kabisa, na historia na vitu vya namna mbalimbali vyenye kupendeza. Tutarudi tena.—Imechangwa.

[Picha katika ukurasa wa 23]

Noti ya Urusi ya rubo tano, na picha ya mandhari hiyohiyo ya Novgorod

[Picha katika ukurasa wa 23]

Kremlin, kutoka kwenye Mto Volkhov

[Picha katika ukurasa wa 24]

Kuvuka daraja la miguu kwenye Mto Volkhov

[Picha katika ukurasa wa 24]

Dini ilikuwa mashuhuri kwa karne nyingi huko Novgorod