Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Matatizo Yangu ya Endometriosis

Matatizo Yangu ya Endometriosis

Matatizo Yangu ya Endometriosis

KAMA ILIVYOSIMULIWA NA DEBORAH ANDREOPOULOS

KWANZA ninataka kusema kwamba mimi sihangaikii daima afya yangu. Sihangaishwi na maumivu madogo-madogo ya mara kwa mara. Ninajaribu kukubali maisha vile yalivyo. Siku fulani ni nzuri; siku nyingine ni mbaya.

Hata hivyo, nilipokuwa kijana, nilianza kuhisi maumivu makali. Mara nyingi katika zile siku mbaya za hedhi nilihisi maumivu makali katika vifuko vya mayai, na pia nilihisi maumivu ya kichwa, mgongo, niliendesha, nilikuwa na kizunguzungu, na kichefuchefu. Mara kwa mara nilihisi maumivu kadhaa kwa wakati mmoja. Ndipo niligundua kwamba mazoezi ya mwili na kupumzika kulisaidia, lakini haikuwa rahisi kupata nafasi.

Maumivu ni jambo la kibinafsi. Hayapimiki, na ni vigumu kuwaelezea wengine waelewe kabisa. Wakati mwingine nililala kitandani kwa siku kadhaa, nikiwa nimedhoofika sana kutokana na matatizo ambayo nimetaja hapo juu, au nilijilazimisha kuamka na kufanya mambo mbalimbali, nikiwa nimekunywa dawa ya kutuliza maumivu hadi niduwazwe. Sikuweza kufanya kazi wala kuwa na maisha ya kawaida. Nilikuwa nimekatishwa tamaa kabisa. Nilisikia kana kwamba nilikuwa mgonjwa. Lakini nilipochunguzwa kwa ukawaida na madaktari, maneno yenye kutia moyo ya madaktari yaliondoa wazo hilo.

Maumivu yakawa makali zaidi nilipopita umri wa miaka 30. Nilihisi maumivu makali yaliyoanza na kuacha bila sababu yoyote iliyojulikana. Niliamka usiku wa manane nikihisi maumivu makali. Pindi moja, nililala usingizi kwa muda wa saa chache tu kwa juma nzima. Isitoshe, mara kwa mara nilikuwa na joto mwilini kwa siku kadhaa. Nilikunywa dawa za kutuliza maumivu mbalimbali na za kutuliza matumbo yangu, nilimeza vidonge kwa ajili ya tumbo langu na mgongo wangu, nami nilitumia mafuta ya kupaka mgongo wangu.

Mstadi wa Uigaji

Dalili nilizokuwa nazo zingaliweza kusababishwa na magonjwa kadhaa yanayoeleweka vizuri. Ugonjwa wangu ulifanana na kipandauso, ugonjwa wa kuungana kwa tishu katika fupanyonga, maumivu ya hedhi, ugonjwa wa kuhara, mchochota wa sehemu ya chini ya utumbo mpana, na kidonda cha tumbo. Kwa muda mrefu nilifikiri kwamba maumivu yangu yalisababishwa na hedhi, hata hivyo wakati huo sikujua kwamba maumivu ya hedhi si makali kiasi cha maumivu niliyokuwa nayo.

Niliambiwa kwamba kuwa na siku ngumu za hedhi na kuhisi maumivu wakati wa hedhi ni mambo ya kawaida na kwamba magumu haya yanatokana na urithi, kutofanya mazoezi ya mwili kwa ukawaida, kazi nyingi ya kukaakaa, hitilafu ya homoni, uchovu, na mikazo ya akilini na pia kutozaa mtoto hali nilikuwa na zaidi ya miaka 30. Daktari mmoja hata aliniambia kwamba dalili zangu zilikuwa dalili za afya njema!

Namna gani yale matatizo mengine yenye kusumbua? Ilisemekana kwamba, uchovu wangu ulisababishwa na kazi nyingi na mikazo ya akilini. Joto mwilini lilisababishwa na uchovu. Maumivu katika matumbo na matatizo ya tumbo yalisababishwa na mikazo ya akilini na kutokula chakula chenye afya. Nayo maumivu ya mgongo yalisababishwa na tatizo la uti wa mgongo na kwa kuwa sikusimama na kuketi ifaavyo. Ilionekana kwamba kila dalili ilikuwa na sababu yake. Hata hivyo, bado nilisikia vibaya sana.

Mwishowe, Uchunguzi Unaofaa

Nilichunguzwa kwa chombo cha ultrasound, mwezi wa Aprili 1998, lakini uchunguzi huo ulionyesha kwamba vifuko vya mayai havikuwa na tatizo. Kwa miezi minne iliyofuata niliendelea kudhoofika. Niliamua kumwona daktari. Aliamua kufanya uchunguzi kwa chombo cha ultrasound tena, akapata kitu kikubwa sana nje ya tumbo langu la uzazi. Alinituma nimwone daktari wa wanawake. Yule daktari wa wanawake alithibitisha kwamba nilikuwa na ama uvimbe mmoja mkubwa wenye sentimeta 10 kwa 12 ama uvimbe kadhaa, karibu na tumbo la uzazi—ni kana kwamba nilikuwa na mimba ya miezi minne! Kisha akadhani kwamba sababu ya matatizo yangu ilikuwa ugonjwa wa endometriosis.

Kwanza nilifadhaishwa. Sikujua mengi kuhusu ugonjwa wa endometriosis. Nilikuwa na maswali mengi sana. Unasababishwa na nini? Ugonjwa huo ungeathirije maisha yangu? Kisha nikatulia. Kwa miaka mingi nilikuwa nikiteseka kwa maumivu yenye kuendelea. Miaka iliyopita nilipochunguzwa tena na tena na madaktari na hakuna matibabu yenye kutuliza wala maelezo ya kuridhisha yaliyopatikana, nilishuka moyo na kujisikia bila msaada, nikijilaumu kwamba ninajihurumia mno kwa sababu ya maumivu ambayo kila mtu anavumilia. Nilijiambia kwamba maumivu yangu hayakuwa makali kama nilivyokuwa nikiwazia. Sasa nilipata kuelewa dalili hizi zote zilizokuwa zimenivuruga.

Visababishi vya Ugonjwa Huo na Matibabu Mbalimbali

Daktari alitaka nipasuliwe kabla hazijapita siku nyingi—uvimbe au fungu la uvimbe lingeweza kupasuka wakati wowote. Hata hivyo, kabla ya kuamua la kufanya, mume wangu nami tulichunguza matokeo ya uchunguzi huo, nasi tulitaka kujua mengi iwezekanavyo juu ya ugonjwa huo uitwao endometriosis.

Tulipata kujua kwamba kulingana na baadhi ya makadirio, asilimia 30 ya wanawake wenye umri wa kuzaa huenda wakawa na ugonjwa wa endometriosis! Kinachosababisha endometriosis hakijulikani. Nadharia moja ni kwamba wakati wa hedhi, baadhi ya damu ya hedhi, badala ya kutoka mwilini, hurudi nyuma kupitia mirija ya mayai. Damu hiyo huingia tumboni na kukua humo. Nadharia nyingine ni kwamba damu ya hedhi inasafirishwa kutoka tumbo la uzazi hadi sehemu nyingine ya mwili kupitia mfumo wa limfu ama kupitia mishipa ya damu. Nadharia ya jeni inasema kwamba endometriosis yaweza kurithiwa, au kwamba wanawake fulani wana udhaifu mbalimbali ambao unawaweka hatarini mwa kushikwa na ugonjwa huo. Wengine wanadhani kwamba sumu mbalimbali katika mazingira yetu yenye uchafuzi mwingi, ndizo zinazosababisha ugonjwa huo.

Tuliambiwa kwamba visa vya endometriosis hutofautiana. Mahali uvimbe unapopatikana, kadiri unavyoingia katika tishu, na ukubwa wake hufanya ugonjwa huo kuwa tofauti na magonjwa mengine. Tulipata kujua kwamba hata uvimbe mdogo sana unaweza kusababisha maumivu yenye kumaliza nguvu kabisa ukiathiri neva iliyopo karibu.

Baadhi ya madaktari wanaamini kwamba kuondoa kabisa tumbo la uzazi na vifuko vya mayai ndiyo matibabu pekee. Hata hivyo, kabla ya kufanya upasuaji huo, homoni zaweza kutumiwa ili kusimamisha kufanyizwa kwa mayai kwa muda mrefu iwezekanavyo. Matibabu hayo yaweza kupunguza ukuzi wa uvimbe wa endometriosis wakati wa matibabu na hata kwa miezi au miaka kadhaa baadaye. Matibabu yasiyoondoa tishu nyingi, ama ya upasuaji, au kwa kutumia laparoscope, ili kuondoa uvimbe au kuuharibu kwa miali ya leza; wapendekezwa kwa visa kadhaa, nao waweza kuleta kitulizo.

Upasuaji na Uwezekano wa Ugonjwa Kutokea Tena

Upasuaji wa laparoscope, ulionekana kunifaa zaidi. Baada ya kuondolewa kwa uvimbe, nilishangaa nilipojulishwa na dakatari wangu kwamba upasuaji huo haungeondoa matatizo yangu yote ya afya. Aliniambia kwamba lazima nikubali hali yangu na niwe na tumaini ili niweze kuendelea kuishi maisha ya kawaida ijapokuwa kulikuwa na uwezekano wa ugonjwa huo kutokea tena. Alinihakikishia kwamba alikuwa tayari kunisaidia wakati wowote.

Daktari huyo aliniambia kwamba ninapaswa kufanya uchunguzi wa vifuko vyangu vya mayai kwa chombo cha ultrasound kila baada ya miezi mitatu, na kwamba ninapaswa kuwa tayari kutumia dawa kwa vipindi fulani, kulingana na hali yangu. Alipendekeza kwamba nianze mara moja matibabu ya dawa iitwayo gonadotropin-releasing hormone. Dawa hiyo ilisimamisha homoni zinazofanya vifuko vya mayai vifanyize mayai, nami nikaingia katika hali kama ya koma-hedhi. Dawa hiyo inatumiwa tu kwa miezi sita kwa kuwa inaweza kudhoofisha mifupa ama kutokeza mabadiliko mengine yanayotokea wakati wa kipindi cha koma-hedhi.

Mwezi mmoja na nusu baada ya kutibiwa kwa dawa hizo, nilianza kuhisi maumivu tena. Nilikuwa nimesoma kuhusu kadiri ambavyo ugonjwa huo unatokea tena, nami nilikuwa nimejaribu kujitayarishia kurudi tena kwa ugonjwa wa endometriosis. Lakini sikutarajia urudi tena mapema hivyo. Uchunguzi wa chombo cha ultrasound ulionyesha kwamba sasa nilikuwa na uvimbe mkubwa katika kifuko changu cha mayai cha upande wa kushoto. Mara moja nilikunywa dawa iliyopendekezwa kwa juma moja, nayo maumivu yakapungua. Baada ya miezi michache uvimbe huo ulitoweka. Hata hivyo, mwaka mmoja baadaye uvimbe mwingine ulitokea. Kwa vyovyote, lazima niwe chonjo na niendelee kutibiwa maishani mwangu mwote.

Kwa kuwa endometriosis ni ugonjwa wa homoni na wa mfumo wa kinga wa mwili, mbali na dawa kuna mambo mengine yawezayo kusaidia mwili wangu kupona. Nimeanza kutumia mboga na matunda mengi pamoja na vitamini, nami nimepunguza utumizi wa vinywaji vyenye kafeini. Ninafanya mazoezi ya mwili zaidi na kupumzika zaidi. Hayo yote yamenisaidia kupunguza athari za dawa na kujenga mwili wangu.

Katika majaribu haya nimethamini sana tegemezo lenye huruma na uelewevu wenye upendo wa mume wangu. Pia, wafanyakazi wenzangu—ambao wote ni wajitoleaji katika ofisi ya tawi ya Watch Tower Society nchini Ugiriki—wamenisaidia, na hilo limenichangamsha. Zaidi ya yote, nimeimarishwa na uhusiano wangu wa binafsi na Yehova, ambaye ‘amenitegemeza nilipokuwa mgonjwa kitandani.’—Zaburi 41:3.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 10]

Wasilianeni!

Ugonjwa na maumivu yaweza kusababisha mikazo katika uhusiano wowote baina ya watu. Hata hivyo, yatupatia pia fursa ya kuongeza ufahamu wetu juu ya hali ya wengine. Ugonjwa udumupo kwa muda mrefu, huenda tabia za mgonjwa zikabadilika kabisa. Jambo hilo laweza kutatiza jamaa nzima, hasa wenzi wa ndoa. Badala ya kusalimu amri, wenzi wa ndoa wapaswa kusitawisha na kutumia ustadi wao wa kuwasiliana—wakiwa tayari kusamehe na kutolaumu.

Mwanamke mwenye ugonjwa wa endometriosis apaswa kukumbuka kwamba mambo yote yanayohusu hedhi ni mageni sana kwa mwanamume, naye labda haelewi hali yake hata kidogo. Hata hivyo, ikiwa mume anashiriki katika uchunguzi wa kukadiria uzito wa tatizo, atapata kuelewa vizuri zaidi. Hapa pana madokezo machache kwa mgonjwa.

Mume wako hawezi kujua mawazo yako bila kuelezwa; mwambie jinsi unavyoumwa na mahali maumivu yalipo

Chagua daktari atakayekuelimisha wewe na mume wako kuhusu endometriosis, atakayetumia wakati wa ziada ikihitajika

Mweleze mume wako kuhusu mabadiliko yoyote ya afya yako—kutia ndani unaposikia vizuri!

Mwombe asome kuhusu ugonjwa huo

[Sanduku/Michoro katika ukurasa wa 11]

Endometriosis Ni Nini?

Jina endometriosis linatokana na endometrium—ambayo ni ngozi ya ndani ya tumbo la uzazi. Ugonjwa wa endometriosis unatokea wakati tishu zinazofanana na chembe za endometrium zinapopatikana nje ya tumbo la uzazi. Ugonjwa huo unaweza kupatikana katika viungo kama vifuko vya mayai, kibofu cha mkojo, na matumbo, na katika baadhi ya wagonjwa unapatikana katika sehemu zote za fupanyonga.

Ijapokuwa endometriosis hufanya tishu ya mwili ikue kwa njia isiyo ya kawaida, ugonjwa huo si kansa. Kinachofanya uvimbe wa endometriosis kuwa ugonjwa si tishu ya uvimbe yenyewe bali ni kwa sababu tishu hiyo inaanza kukua, nje ya tumbo la uzazi. Tishu hii ikiwa ndani ya tumbo la uzazi, inasaidia kulisha kijusi wakati wa mimba. Katika wanawake wasio na mimba tishu hiyo inatoka mwilini siku za hedhi.

Hata hivyo, tishu ya endometrium iliyoko nje ya tumbo la uzazi, haina njia ya kutoka mwilini. Matokeo ni kutokwa na damu ndani ya mwili, kuharibika kwa damu na tishu ya uvimbe, mchochota wa sehemu za karibu na uvimbe, na kovu linalotokana na uvimbe huo. Ikitegemea mahali uvimbe upo matatizo mengine yaweza kutokea kama vile, kuunganishwa kwa tishu kwa sababu ya mwako, kutokwa na damu katika matumbo au matumbo kuziba, matatizo ya kibofu cha mkojo, na kupasuka kwa uvimbe ambako kwaweza kueneza ugonjwa. Dalili zaweza kuzidi, ilhali baadhi ya wagonjwa wanapona na kurudi kuwa wagonjwa mara kwa mara.

[Michoro]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Mirija ya mayai (fallopian tubes)

Tumbo la uzazi

Vifuko vya mayai

Endometrium (ngozi ya ndani ya tumbo la uzazi)

Kila mwezi uvimbe wa “endometrium” unaharibika na kutokwa damu lakini hauna njia ya kutoka mwilini

Uvimbe wa “endometrium”

Tishu ya “endometrium” iliyojinata kwenye vifuko vya mayai

Uvimbe wa “endometrium”

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 12, 13]

“JE, NI UGONJWA WA WANAWAKE USIOELEWEKA”?

Ili kupata habari zaidi kuhusu athari za kiakili na kihisia za ugonjwa wa endometriosis, mwandishi wa gazeti la Amkeni! alimhoji Mary Lou Ballweg aliye msimamizi wa shirika la Endometriosis Association, katika Milwaukee, Wisconsin. Hapa pana hoja muhimu za mahojiano hayo.

S: “Endometriosis” huwaathirije wanawake kihisia?

J: Hilo linategemea jinsi ugonjwa huo unavyoendelea kwa wakati fulani. Wanawake vijana wanaweza kuathiriwa vibaya sana kihisia. Wasichana hawawezi kuelewa hali yao vizuri, hasa kwa kuwa mara nyingi uchunguzi hauonyeshi kwamba wanao ugonjwa huo. Pia, hawataki kuongea kuhusu mambo kama hayo. Hawataki kuzungumza na wazazi wao wala wengine wowote kuhusu hali yao. Kwa hiyo, wasichana hao huenda wakaamini kwamba wao si wenye nguvu kama wengine. Mara nyingi wasichana hao wanapata ugumu shuleni, nao hawawezi kudumisha ushirikiano wa kawaida na wengine nje ya shule. Tumepata habari za wasichana wengi ambao wameacha shule. Kila juma tunapata habari juu ya angalau msichana mmoja ambaye ameshindwa shuleni kwa sababu ya matatizo magumu ya afya yatokanayo na endometriosis.

S: Namna gani wanawake wazee na walioolewa?

J: Maumivu yaweza kuvuruga kabisa maisha ya ndoa, hasa ikiwa ugonjwa maalumu haujulikani. Mara ugonjwa ujulikanapo, mume na mke waweza kusaidiana kwa kuwa wanaelewa hali. Ndipo pamoja waweza, twatumaini, kupata njia za kushinda athari za ugonjwa huo. Lakini, uchunguzi usipothibitisha kwamba mwanamke ni mgonjwa, matokeo ni mabaya sana. Mfanyakazi mwenzetu alielezwa na daktari wake—mbele ya mume wake—kwamba aliwazia tu maumivu na dalili zote za ugonjwa huo, yaani hazikuwa halisi. Mume alimwamini daktari, nao sasa wametalikiana. Kutoelewana kwa aina hiyo ni tatizo kubwa. Ukienda nyumbani na kueleza familia yako kwamba una ugonjwa wa kudumu wa multiple sclerosis, yaelekea ungehurumiwa na kupata utegemezo wa kadiri fulani. Lakini ukienda nyumbani na kuwaeleza kwamba una ugonjwa wa endometriosis, watajiuliza, ‘Huo ni ugonjwa wa aina gani?’ Kwao huo ni ugonjwa wa wanawake usioeleweka ambao watu wanakataa hata kuzungumza juu yake. Huenda wasikujali hata kidogo.

S: Mume, watoto, na wazazi waweza kumsaidiaje mwanamke aliye na ugonjwa wa “endometriosis”?

J: Kwanza, nadhani ni lazima wamwamini mwanamke huyo kwamba yeye ni mgonjwa. Wapaswa kumpatia utegemezo uleule ambao wangempatia iwapo angeshikwa na ugonjwa mwingine wowote. Jambo kuu ni kujifunza mengi wawezavyo kuhusu ugonjwa huo. Mtu akielewa ugonjwa huo, aweza kuelewa pia athari zake, naye aweza kuelewa athari za baadhi ya dawa za ugonjwa huo. Isitoshe, nimeona kwamba katika jamii nyingi ulimwenguni ni mwiko kuongea kuhusu umbo la mwanamke—watu wanaona haya kuongea juu ya habari hiyo. Hilo lasikitisha sana. Kwa hiyo, nadhani kwamba kazi kubwa zaidi tuliyo nayo ulimwenguni pote ni ya kubadili mitazamo ya watu juu ya wanawake na umbo lao.

[Picha]

Mary Lou Ballweg