Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Antaktika Bara Lililo Hatarini

Antaktika Bara Lililo Hatarini

Antaktika Bara Lililo Hatarini

WANAANGA wanapotazama dunia kutoka angani, chasema kitabu Antarctica: The Last Continent, sehemu yenye kutokeza zaidi ya sayari yetu ni bamba la barafu la Antaktika. “Hung’aa kama taa kubwa nyeupe iliyo sehemu ya chini ya ulimwengu,” wakaripoti wanaanga hao.

Antaktika iliyo na ukubwa wa kilometa za kyubiki 30,000,000 ni kama mashine ya kutengenezea barafu inayotoshana na bara nzima. Theluji huanguka ardhini na kurundamana ili kufanyiza barafu. Nguvu za uvutano hufanya barafu itiririke polepole kuelekea pwani, na huko huingia baharini na kufanyiza miamba mikubwa sana ya barafu.—Ona sanduku kwenye ukurasa wa 18.

Miamba ya Barafu Inayopungua

Hata hivyo, katika miaka ya majuzi, kuyeyuka kunakoongezeka kumepunguza ukubwa wa miamba kadhaa ya barafu, na mingine imetoweka kabisa. Mwaka 1995 sehemu yenye ukubwa wa kilometa za mraba 1,000 kati ya Mwamba wa Barafu wa Larsen wenye ukubwa wa kilometa 1,000 iliporomoka na kuvunjika na kuwa maelfu ya vilima barafu, kulingana na ripoti moja.

Eneo ambalo limeathiriwa kufikia sasa na kupungua kwa barafu ni Peninsula ya Antaktiki. Katika miaka 50 iliyopita, mwendelezo wa safu ya milima ya Andes ya Amerika Kusini, ambayo ni peninsula yenye umbo la S imepata ongezeko la joto la nyuzi Selsiasi 2.5. Tokeo ni kwamba Kisiwa cha James Ross, ambacho wakati mmoja kilizingirwa na barafu, sasa chaweza kuzungukwa. Kupungua kwa barafu kumetokeza pia ongezeko kubwa la mimea.

Kwa kuwa mahali ambapo pameyeyuka sana ni kwenye eneo la Peninsula ya Antaktiki pekee, wanasayansi fulani hawasadiki kwamba jambo hilo ladhihirisha kuongezeka kwa joto ulimwenguni pote. Hata hivyo, kulingana na uchunguzi mmoja wa Norway, barafu ya Aktiki inapungua pia. (Kwa sababu Ncha ya Kaskazini haipo penye ardhi, barafu nyingi ya Aktiki ni ya baharini.) Kulingana na uchunguzi huo, mabadiliko hayo yote yanalingana kabisa na utabiri kuhusu kuongezeka kwa joto ulimwenguni pote.

Lakini Antaktika hutimiza mengi zaidi kuliko kupatwa tu na mabadiliko ya halijoto. Bara hilo limeelezwa kuwa “eneo muhimu ambalo huelekeza sana tabia ya nchi ulimwenguni.” Ikiwa ndivyo, basi huenda halihewa ya wakati ujao ikaathiriwa iwapo bara hilo litaendelea kubadilika.

Kwa sasa, juu ya Antaktika kuna shimo lenye ukubwa maradufu ya Ulaya kwenye tabaka la ozoni la angahewa. Ozoni ambayo ni aina fulani ya oksijeni, hukinga dunia dhidi ya mnururisho hatari wa urujuanimno ambao huharibu macho na kusababisha kansa ya ngozi. Kwa sababu ya kuongezeka kwa mnururisho, watafiti katika Antaktika lazima walinde ngozi yao kutokana na jua na kuvaa miwani ya jua yenye rangi ya pekee inayoakisi nuru ili kulinda macho yao. Wakati ujao itajulikana wanyama wa mwituni wa Antaktika watakuwa wameathiriwa kwa kadiri gani.

Bara Linaloathiriwa kwa Urahisi —Tembea kwa Uangalifu

Huenda kichwa kilicho juu kikawakaribisha ifaavyo wageni Antaktika. Kwa nini? Kuna sababu kadhaa, kulingana na Tarafa ya Australia ya Antaktiki. Kwanza, kwa sababu ya uhusiano sahili wa ikolojia ya Antaktika, mazingira yake yaweza kuathiriwa kwa urahisi sana. Pili, mimea hukua polepole sana hivi kwamba alama ya wayo kwenye tuta la kuvumwani yaweza kuonekana miaka kumi baadaye. Mimea iliyoharibika au kudhoofika haiwezi kustahimili pepo kali za Antaktika, zinazoweza kuharibu mimea mingi sana. Tatu, baridi kali mno hufanya vitu vichukue miongo mingi kuoza. Nne, bila kujua watu wanaweza kuleta viumbe wadogo mno kwenye bara hili lililojitenga na linaloweza kuathiriwa kwa urahisi. Hatimaye, mahali ambapo watalii na wanasayansi huzuru mara nyingi ni kingo za pwani—maeneo yanayowafaa sana wanyama na mimea. Kwa kuwa maeneo hayo ni asilimia 2 hivi ya ardhi, ni rahisi kuelewa kwa nini hivi karibuni Antaktika itakuwa na msongamano wa watu. Hilo lazusha swali, ni nani anayesimamia bara hili kubwa?

Ni Nani Anayetawala Antaktika?

Ijapokuwa nchi saba zinadai kumiliki visehemu katika Antaktika, bara zima kwa ujumla ni la pekee kwa sababu halina mtawala aliyeteuliwa wala raia. “Antaktika ndilo bara pekee duniani kutawaliwa na mikataba ya kimataifa tu,” yaripoti Tarafa ya Australia ya Antaktiki.

Mkataba wa Antaktika ulitiwa sahihi na serikali 12 na ukaanza kutumika Juni 23, 1961. Tangu wakati huo, idadi ya mataifa wanachama imekua na kuzidi 40. Lengo la mkataba huo ni “kuhakikisha kwamba kwa masilahi ya wanadamu wote, Antaktika itaendelea kutumiwa milele kwa makusudi ya amani pekee na haitakuwa mahali pa mizozo ya kimataifa.”

Katika Januari 1998 Kumbukumbu la Kulinda Mazingira lililotangulia Mkataba wa Antaktika likawa sheria ya kimataifa. Kumbukumbu hilo limepiga marufuku uchimbaji wote wa madini katika Antaktika kwa angalau miaka 50. Pia limeteua bara hilo na mifumikolojia ya viumbe wa majini kuwa “hifadhi ya asili iliyotolewa kwa ajili ya amani na sayansi.” Shughuli za kijeshi, majaribio ya silaha, na kutupwa kwa mabaki ya nyuklia yamepigwa marufuku. Hata vigari vya kutelezea juu ya theluji vinavyokokotwa na mbwa vimepigwa marufuku pia.

Mkataba wa Antaktiki umesifiwa kuwa “mfano wa ushirikiano wa kimataifa usio na kifani.” Hata hivyo, bado kuna matatizo mengi yanayohitaji kutatuliwa, kutia ndani utawala. Mathalani, ni nani atakayehakikisha kwamba mkataba huo unafuatwa, na jinsi gani? Na mataifa wanachama yatakabilianaje na ongezeko la haraka la watalii—ambao ni tisho kwa ikolojia ya Antaktika inayoweza kuathiriwa kwa urahisi? Katika miaka ya majuzi zaidi ya watalii 7,000 wanaosafiri kwa meli wamezuru Antaktika kila mwaka, na idadi hiyo yatarajiwa kurudufika baada ya muda mfupi.

Huenda kukatokea magumu mengine wakati ujao. Mathalani, itakuwaje wanasayansi watakapopata madini yenye thamani au mafuta? Je, mkataba huo utazuia shughuli za kibiashara na uchafuzi ambao mara nyingi husababishwa na shughuli hizo? Mikataba yaweza kubadilishwa, kutia ndani Mkataba wa Antaktika. Kwa hakika, Kifungu cha 12 kinaruhusu mkataba huo “kurekebishwa wakati wowote chini ya makubaliano ya wote Waliohusika Kuanzisha Mkataba huo.”

Bila shaka, hakuna mkataba unaoweza kulinda Antaktika dhidi ya uchafuzi kutoka kwa nchi za kisasa zilizositawi kiviwanda. Itasikitisha kama nini iwapo “taa nyeupe” maridadi iliyo sehemu ya chini ya ulimwengu itachafuliwa kwa sababu ya pupa na kukosa ujuzi kwa wanadamu! Kudhuru Antaktika ni kuwadhuru wanadamu. Somo tunalopata kutokana na Antaktika ni kwamba dunia nzima—sawa na mwili wa binadamu—ni mfumo unaotegemeana, ulioratibiwa kikamilifu na Muumba ili kuendeleza uhai na kutufurahisha.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 18]

MWAMBA WA BARAFU NI NINI?

Juu kabisa kwenye sehemu za ndani za Antaktika, vijito vya barafu vinavyofanyizwa na theluji inayoanguka, hutiririka kuelekea pwani—vingine hutiririka kwa umbali wa kilometa moja hivi kwa mwaka, kulingana na picha za karibuni kutoka kwa rada za setilaiti. Vijito vingi vya barafu huungana kama mito na kufanyiza mito mikubwa sana ya barafu. Inapofika baharini, mito hiyo iliyoganda huelea juu ya maji na kufanyiza miamba ya barafu, mwamba ulio mkubwa zaidi ni Mwamba wa Barafu wa Ross (ulioonyeshwa). Una vijito vya barafu au barafuto zisizopungua saba, na unatoshana na Ufaransa na sehemu nyingine zina unene wa kilometa moja hivi. *

Chini ya hali za kawaida, miamba ya barafu haipungui. Barafuto zinapoongeza barafu zaidi kwenye mwamba, tabaka la nje la mwamba husukumwa mbali zaidi na bahari, kama vile dawa ya meno hufinywa kutoka kwenye tyubu. Kufikia hapo hatimaye vipande vikubwa huvunjika (hatua inayoitwa calving), na vipande hivyo huwa vilima vya barafu. Vilima fulani vya barafu vina “ukubwa upatao kilometa za mraba 13,000,” chasema kichapo The World Book Encyclopedia. Hata hivyo, katika miaka ya karibuni calving imeongezeka na miamba ya barafu imepungua, mingine imetoweka kabisa. Ijapokuwa hivyo, viwango vya bahari haviongezeki. Kwa nini? Kwa sababu miamba ya barafu tayari inaelea, na kutwaa nafasi ya maji kwa uzito wao. Lakini iwapo barafu kwenye ardhi ya Antaktika ingeyeyuka, ingekuwa sawa na kumwaga maji kutoka kwa tangi lenye ukubwa wa kilometa kyubiki 30,000,000 baharini! Viwango vya bahari vingeongezeka kwa meta 65 hivi!

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 21 Miamba ya barafu ni tofauti na barafu ya baharini. Barafu ya baharini huanza kama vipande vya barafu vinavyoelea na kujitokeza baharini wakati wa baridi kali maji yanapoganda. Kisha vipande hivyo huungana na kufanyiza barafu ya baharini. Mambo huwa kinyume wakati wa kiangazi. Vilima vya barafu havitokani na barafu ya baharini, lakini, hutokana na miamba ya barafu.

[Picha]

Miamba mikubwa ya barafu yavunjika karibu na Mwamba wa Barafu wa Ross. Hapa mwamba wa barafu una urefu wa takriban meta 65 juu ya usawa wa bahari

[Hisani]

Tui De Roy

[Picha katika ukurasa wa 20]

Kitoto cha sili aina ya “weddell”

[Hisani]

Picha: Commander John Bortniak, NOAA Corps