Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Wahitaji Kitanda Kipya?

Je, Wahitaji Kitanda Kipya?

Je, Wahitaji Kitanda Kipya?

Na mleta-habari wa Amkeni! katika Uingereza

Je, mara nyingi wewe hukosa usingizi, ukijipindua-pindua na kugaagaa angalau ulale starehe, kisha unaamka asubuhi ukiwa mchovu na mwenye maumivu? Ikiwa ndivyo, huenda tatizo likawa ni kitanda chako.

FANICHA hii yaweza kukufaidi au kukudhuru. Iwapo unaishi katika nchi ambamo vitanda hutumiwa, yaelekea kwamba utapumzika kitandani thuluthi ya maisha yako, lakini kitanda chako hakitadumu milele. Je, wafurahia kitanda chako cha sasa?

Je, Wahitaji Kitanda Kipya?

Kwa kawaida kitanda hukuhudumia vyema kwa miaka kumi hivi. Mtu mzito aweza kuchakaza kitanda upesi. Kumbuka kwamba mahitaji yako na mapendezi yako hubadilika kadiri unavyozeeka. Ili kuamua endapo unahitaji kitanda kipya, jiulize maswali haya. ‘Je, mimi huamka nikiwa na shingo iliyokakamaa au maumivu ya mgongo? Je, kitanda changu ni kidogo mno? Je, nafinywa na springi au viunzi? Je, mimi husikia sauti za mkwaruzo au msuguano ninaposogea? Je, mimi na mwenzangu hubingirika kuelekea katikati mwa kitanda bila kupenda? Je, kikalio cha godoro kimekunjamana au kubonyea? Je, miguu yake imechakaa?’ Waweza kuamua iwapo unahitaji kununua kitanda kipya kwa kujibu maswali hayo.

Kitanda Kizuri Kikoje?

Kitanda kizuri hukustarehesha na kukutegemeza, hukidhi mahitaji na mapendezi yako. Vitanda vingi huwa na godoro na viunzi, lakini godoro ni muhimu kwa starehe. Lina sehemu kadhaa. Kwanza, huwa na kifuniko, au mfuko wa godoro, unaobeba kila kitu. Kisha huwa na matabaka ya pedi laini ili kukulinda na kuondoa unyevu wa mwili. Sehemu ya tatu, ambayo inalitegemeza na kuliimarisha, kwa kawaida huwa na koili au springi ngumu za feleji. Kuna namna mbalimbali za viunzi vya godoro, lakini kwa kawaida, utegemezo mzuri zaidi hutegemea springi zaidi zenye nyaya nene zaidi. Siku hizi wengi hutengeneza magodoro kwa sponji; ni nyepesi kuliko springi.

Hata hivyo, godoro zuri hufaa tu liwekwapo kwenye kikalio kifaacho, hususan kwenye kikalio chake. Mara nyingi kochi-kitanda huuzwa pamoja na godoro na kikalio. Umbo lake mfano wa boksi hutenda kama shokomzoba kubwa, huruhusu godoro lifyonze hewa na hivyo kudumu kwa muda mrefu. Au waweza kutumia fremu ya kitanda. Kwa kawaida huwa na vibao na huwa wazi sehemu ya chini, huwezesha godoro lipate hewa. Fremu ya chini isiyogawanywa huandaa kikalio imara cha godoro, ilhali sleti zenye springi hunyumbulika zaidi.

Kuchagua Kitanda Kifaacho

Wapaswa kukumbuka nini unaponunua kitanda? Kitanda kilichotumiwa huwa kimefyonza jasho la watu wengine na huwa na magamba ya ngozi na huenda kikawa na nyenyere wengi ambao waweza kukuletea mizio, ugonjwa wa pumu, au ukurutu. Na huenda kikakosa kutimiza matakwa ya afya au usalama.

Kabla ya kununua kitanda kipya, inapendekezwa kwamba uzingatie mambo muhimu kwanza, kama vile bei, mambo ya kiafya, au ukubwa wake. Jaribu kupangia muda wa kutosha wa kuzuru maduka yanayopendwa, na uulizie habari za kutosha kuhusu kila kitanda au godoro. Kwa kuwa mara nyingi vitanda huwa ghali, usikubali kufanya uamuzi harakaharaka.

Huenda ikawa vigumu kuchagua kitanda kifaacho uwapo mchovu. Vaa mavazi yanayostarehesha. Usihofu kujaribu kitanda chochote. Vua koti lako na viatu kisha ulalie kila kitanda kwa dakika chache. Lala kwa njia mbalimbali, ukizingatia sana namna ambavyo kinategemeza mabega, nyonga, na sehemu ya chini ya mgongo wako.—Ona sanduku lililo chini.

Kutunza Kitanda Chako

Kitanda chako kitadumu kwa muda mrefu sana ukikitunza vyema. Waombe mashauri wauzaji, soma kwa uangalifu maagizo ya utunzaji kutoka kwa watengenezaji. Mara ufikishapo kitanda chako kipya nyumbani, ondoa makaratasi yanayokifunika haraka iwezekanavyo. Kufanya hivyo kutazuia mtonesho, unaoweza kusababisha unyevunyevu, kuvu, na kuoza. Yafuatayo ni madokezo machache ya ziada.

● Pindua godoro jipya la springi toka upande mmoja hadi mwingine kila baada ya juma moja au majuma mawili kwa miezi michache ya kwanza na kila baada ya miezi mitatu tokea hapo. Hilo litasaidia vijazo vyake vitulie na litahakikisha kwamba godoro linachakaa sawia. Ikiwa una maumivu ya mgongo, yafaa ufikirie kununua godoro la sponji, kwa kuwa huenda lisihitaji kupinduliwa kwa kawaida.

● Usikunje, au kubana kamwe godoro. Ili kuepuka kuharibu kitambaa chake, tumia vishikio vyake unapolinyoosha kitandani wala si kulibeba.

● Kila asubuhi ondoa shuka za kitanda kwa angalau dakika 20 ili kitanda chako kipate hewa na kuondoa mvuke wa mwili.

● Dumisha usafi wa godoro lako kwa kulifunika kwa kifuniko kinachoweza kufuliwa. Vuta vumbi na manyoya kwa ukawaida kutoka kwenye godoro na kikalio chake, ondoa haraka madoa yoyote kwa maji baridi yenye sabuni kiasi.

● Jitahidi kutoketi mahali palepale pembeni mwa godoro kila mara. Usiwaruhusu watoto au mtu mwingine yeyote arukeruke kitandani.

Kitanda chako ni muhimu si tu kwa ajili ya gharama yake. Ni muhimu katika thuluthi ya maisha yako—ambayo inaweza kuathiri sana sehemu mbili kwa tatu inayosalia. Ukichagua kwa hekima na kutunza kitanda chako muhimu, kitakutunza.

[Sanduku katika ukurasa wa 22]

Ni Kitanda Gani Kinachokufaa?

Starehe na utegemezo. Godoro linalokufaa halihitaji kuwa gumu kama ubao. Kwa kweli, yaaminika kwamba godoro gumu sana laweza kuzidisha matatizo ya mgongo. Mwili wako wapasa kukusaidia uchague kitanda kinachostarehesha. Lala chali. Endapo unaweza kupenyeza mkono wako kwenye upinde wa mgongo kwa urahisi na ikiwa waweza kugeuka kwa urahisi, yaelekea godoro hilo ni gumu ifaavyo. Godoro lenye kutegemeza lapasa kuruhusu uti wako unyooke barabara unapolala kwa upande. Mtu mzito atahitaji kitanda imara zaidi.

Ukubwa. Chagua kitanda kinachokuwezesha ujisogeze kwa wepesi. Watu wawili wakilala kwenye kitanda kimoja, kumbuka kwamba kila mmoja wa watu wazima wawili wanaolalia kitanda cha wastani cha watu wawili atatumia nafasi sawa na mtoto aliye katika kitanda cha watoto.

Vifaa vinavyofaana. Iwezekanapo, nunua godoro na kikalio vinavyofaana na ambavyo vimekusudiwa kutumiwa pamoja ili kukustarehesha na kukutegemeza. Kikalio kikuukuu chaweza kuharibu godoro jipya na kuathiri pia dhamana yake.

Ubora. Kwa kawaida ubora wa kitu ununuacho hutegemea gharama, kwa hiyo nunua kitanda bora chenye bei uwezayo kumudu.

Nafasi. Ikiwa nafasi ni haba, kitanda kiwezacho kukunjwa au kutiwa ukutani huenda kikafaa. Au huenda ukatumia godoro lenye matabaka ya pamba linalotandazwa upesi sakafuni usiku. Huenda magodoro hayo ya pamba yakauzwa yakiwa vitanda vya kukalia vyenye vipande vya fremu viwezavyo kugeuzwa umbo.

Matatizo ya kiafya. Ikiwa hupati starehe ulaliapo kitanda cha kawaida, unaweza kulala kwa njia mbalimbali katika kitanda kinachorekebishika. Godoro la mpira lililojazwa maji hutegemeza na kusambaza sawia uzito wa mwili, laweza likawastarehesha wale walio na maumivu ya mgongo yanayosababishwa na sehemu zinazouma.

Watu wenye mizio. Ikiwa una mzio wa vumbi au vijazo vya kiasili, waweza kutumia godoro la nyuzi za sanisia au sponji. Pia yafaa kukumbuka kwamba vizio havirundikani kwa urahisi kwenye fremu ya kitanda yenye kikalio kilichogawanywa au kwenye godoro la maji.

Wazee. Hakikisha kwamba nyayo za miguu zakanyaga sakafuni unapoketi pembeni mwa kitanda chako. Kikalio chenye pembe thabiti kitafanya iwe rahisi kwako kushuka na kupanda kitandani unapoketi.

[Sanduku katika ukurasa wa 23]

Madokezo ya Usalama

▪ Valia mavazi ya kulala yasiyoshika moto.

▪ Hakikisha kwamba matandiko yako mbali na moto na vipasha-joto.

▪ Chunguza blanketi ya umeme mara kwa mara uone kama ina nyuzi zinazoning’inia, mikunjo mikubwa, alama za kuchomeka, na waya wa umeme uliochanika. Usitumie kamwe blanketi hiyo ikiwa imelowa, iache ikauke yenyewe. Usiwekelee vitu vizito kitandani blanketi hiyo inapowashwa.

▪ Usitie maji yanayochemka kwenye chupa ya maji moto, wala usiitumie pamoja na blanketi ya umeme. Iondoe kabla ya mtoto kupanda kitandani.

[Mchoro katika ukurasa wa 23]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Mfuko wa godoro

Tandiko la kitanda lenye mshono tata wa almasi

Tandiko lenye mshono mdogo

Ushonaji wa vishungi

Matabaka ya pedi laini

Fremu ya ndani

Sponji

Springi mfululizo

Springi wazi

Springi zilizositiriwa

[Hisani]

Reproduced by courtesy of the Sleep Council

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 21]

Reproduced by courtesy of the Sleep Council