Hamia kwenye habari

Chanzo cha Halloween Ni Nini?

Chanzo cha Halloween Ni Nini?

Jibu la Biblia

 Biblia haitaji lolote kuhusu Halloween, sherehe inayoadhimishwa na wengi Oktoba 31 kila mwaka. Hata hivyo, tangu zamani chanzo na desturi za Halloween zinapingana na mafundisho ya Biblia.

Katika makala hii

 Historia na desturi za Halloween

 •   Samhain: Kitabu The World Book Encyclopedia kinasema Halloween ilitokana na “sherehe ya kale ya wapagani iliyosherehekewa na Waselti zaidi ya miaka 2,000 iliyopita. Waselti waliamini kwamba wafu wanaweza kutembea katikati ya watu walio hai. Wakati wa sherehe ya Samhain, walio hai wangeweza kuwatembelea wafu.”​—Ona kichwa “ Jina Halloween lilitoka wapi?

 •   Nguo zinazovaliwa wakati wa Halloween, kuwaomba watu peremende na kuwatisha wasipowapatia (trick or treat): Kulingana na kitabu kimoja, baadhi ya Waselti walivalia mavazi yenye kutisha ili roho waovu wanaozunguka-zunguka “wadhani wao ni wenzao” na hivyo wasiwadhuru. Wengine waliwatuliza roho waovu kwa kuwapa peremende. a

   Katika enzi za kati barani Ulaya, makasisi Wakatoliki walikubali desturi za wapagani na kuwahimiza wafuasi wao waende nyumba kwa nyumba wakiwa wamevalia mavazi maalum na kuomba zawadi ndogo ndogo.

 •   Mizuka, wanyonya damu, watu-mbweha, wachawi, na maiti zinazotembea: Tangu zamani hawa wamehusianishwa na roho waovu. Kitabu Halloween Trivia kinawaita “viumbe wenye kutisha walio na nguvu zisizo za kawaida.” Kitabu hicho kinasema pia kwamba viumbe hao “wanahusianishwa na kifo, wafu, au hofu ya kifo.”

 •   Maboga ya Halloween na taa zenye sura ya binadamu zilizotengenezwa kwa maboga: Katika enzi za kati nchini Uingereza, watu “walienda nyumba kwa nyumba kuomba chakula kama malipo ya kusali kwa ajili ya wafu,” na walibeba “mishumaa iliyotiwa ndani ya tanipu, na mishumaa hiyo iliwakilisha nafsi iliyokwama toharani.” (Halloween​—From Pagan Ritual to Party Night) Wengine wanasema kwamba taa hizo za tanipu zilitumiwa kufukuza roho waovu. Katika miaka ya 1800, kule Amerika Kaskazini, maboga yalianza kutumiwa badala ya tanipu kwa kuwa yalipatikana kwa wingi na ilikuwa rahisi kuondoa sehemu ya ndani.

 Je, ni muhimu kuzingatia chanzo cha kipagani cha Halloween?

 Ndiyo. Baadhi ya watu wanahisi kwamba kusherehekea Halloween hakuna madhara lakini mambo yanayofanywa katika sherehe hiyo yanapingana na mafundisho ya Biblia. Halloween imetokana na imani za uwongo kuhusu wafu na roho waovu.

 Soma mistari ifuatayo inayoonyesha maoni ya Mungu kuelekea imani zinazohusianishwa na Halloween:

 •   “Pasiwe mtu yeyote miongoni mwenu . . . mwenye kutaka kauli kwa mizimu na pepo au kutoka kwa wafu.”​—Kumbukumbu la Sheria 18:10-12, Biblia Habari Njema.

   Maana: Mungu anachukizwa na jitihada zozote za kuwasiliana na wafu au hata kuigiza au kujifanya kwamba tunawasiliana na wale waliokufa.

 •   “Waliokufa hawajui jambo lolote kamwe.”​—Mhubiri 9:5.

   Maana: Kwa kuwa wafu hawajui lolote hawawezi kuwasiliana na walio hai.

 •   “[Msiwe] washiriki pamoja na roho waovu. Hamwezi kuwa mkinywa kikombe cha Yehova na kikombe cha roho waovu.”​—1 Wakorintho 10:20, 21.

   Maana: Wale wanaotaka kupata kibali cha Mungu ni lazima waepuke kabisa uhusiano wowote na roho waovu.

 •   “[Simama] imara dhidi ya matendo yenye hila ya Ibilisi; kwa sababu tunapambana . . . dhidi ya majeshi ya roho waovu.”​—Waefeso 6:11, 12.

   Maana: Wakristo wanapaswa kuyapinga majeshi ya roho waovu na si kuigiza kana kwamba wanasherehekea pamoja nao.

a Ona kitabu Halloween: An American Holiday, an American History, ukurasa wa 4.