Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

 TUNAYOJIFUNZA KUTOKANA NA HISTORIA

Wamorisko Wafukuzwa Hispania

Wamorisko Wafukuzwa Hispania

Inasemekana kwamba, karibu kila jambo lililofanywa na Wahispania katika tukio hili lenye kuhuzunisha, lilichochewa na kanisa. Unapaswa kusoma kuhusu tukio hili.

WATAWALA Wahispania walitaka Nchi yao iwe ya Kikristo na iwe na mfumo mmoja wa kisheria. Wamorisko walionwa kuwa watu wasiomjua Mungu na chukizo machoni pa Mungu. Miaka mingi baadaye uamuzi ulifanywa. Suluhisho lilikuwa nini? Kuwafukuza Wamorisko! *

WABADILI DINI KWA NGUVU

Kwa miaka mingi, kikundi kidogo cha Waarabu nchini Hispania kilichoitwa Mudéjar kiliishi kwa amani katika maeneo yaliyotawaliwa na Wakatoliki. Kwa muda fulani, walitambuliwa kisheria na kuruhusiwa kufuata sheria, desturi, na dini yao katika maeneo mbalimbali.

Hata hivyo, mwaka wa 1492 watawala Wakatoliki Ferdinand wa Pili na Isabella walishinda eneo la Granada, ambalo lilikuwa eneo la mwisho la Iberia lililomilikiwa na Waislamu. Baada ya ushindi huo, Waarabu walipewa uhuru kama wa kikundi cha Mudéjar. Hata hivyo, viongozi Wakatoliki walizidi kuwatesa na kuwashinikiza Waislamu waliokuwa chini ya utawala wao wabadili dini. Waarabu walilalamika kwa sababu viongozi hao walikiuka makubaliano, na wakaasi mwaka wa 1499.  Majeshi ya serikali yalikomesha uasi huo, na Waislamu katika maeneo mengi wakalazimishwa kubadili dini au kuhama. Wahispania waliwaita wale waliobadili dini na kubaki Hispania Wamorisko.

“HAWAKUWA WAKRISTO WAZURI WALA RAIA WAAMINIFU”

Kufikia 1526, Uislamu ulikuwa umepigwa marufuku nchini Hispania, lakini Wamorisko wengi waliendeleza dini yao kisiri. Kwa ujumla walidumisha utamaduni wao.

Mwanzoni, Wamorisko walivumiliwa ingawa walifanya mambo machache tu katika dini ya Katoliki. Hata hivyo, walitimiza majukumu muhimu kama vile kuwa wasanii, mafundi, wafanyakazi, na walipa ushuru. Hata hivyo, Wamorisko walichukiwa kwa kukataa kubadilika kabisa, na walibaguliwa na serikali na pia watu wa kawaida. Ubaguzi huo ulitokea kwa kuwa kanisa lilitilia shaka unyoofu wao katika kubadili dini.

Muda si muda, walianza kulazimishwa. Mwaka wa 1567, Mfalme Philip wa Pili alichapisha uamuzi uliopiga marufuku lugha ya Wamorisko, mavazi, desturi, na tamaduni zao. Hilo lilitokeza uasi mpya na mauaji.

Inakadiriwa kwamba Wamorisko 300,000 waliteseka sana na kulazimika kukimbia Hispania

Kulingana na wanahistoria, watawala Wahispania waliamini kwamba “Wamorisko hawakuwa Wakristo wazuri wala raia waaminifu.” Hivyo, walituhumiwa kushirikiana na maadui wa Hispania yaani maharamia wa Barbari, Waprotestanti Wafaransa, na Waturuki ili wavamie nchi hiyo. Ubaguzi na pia hofu ya kusalitiwa na Wamorisko ilimfanya Philip wa Tatu awafukuze mwaka wa 1609. * Katika miaka iliyofuata, watu waliodhaniwa kuwa Wamorisko waliteswa. Kupitia njia hiyo, Hispania ikawa nchi ya Kikatoliki.

^ fu. 4 Jina Wamorisko linamaanisha “Waarabu” katika Kihispania. Wanahistoria wanatumia jina hilo kuwarejezea Waislamu ambao walibadili dini na kuwa Wakatoliki na kuendelea kuishi kwenye Rasi ya Iberia baada ya kushindwa kwa ufalme wa mwisho wa Kiislamu mwaka wa 1492.

^ fu. 12 Wanahistoria wanasema kwamba huenda mmoja wa watawala wa Hispania alifaidika sana na mali ambazo Wamorisko walinyang’anywa.