Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Ulimwenguni

Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni, ukatili dhidi ya wanawake umekuwa “janga la kiafya lililoenea ulimwenguni pote.” Shirika hilo linasema, “asilimia 35 hivi ya wanawake watakabili ukatili kutoka kwa wapenzi wao au watu wengine. Ukatili kutoka kwa wapenzi ndio ulioenea zaidi . . . , ukiathiri asilimia 30 ya wanawake ulimwenguni.”

Uingereza

Utafiti uliohusisha watu 64,303 ulionyesha kwamba asilimia 79 kati yao wanaamini “dini ni chanzo cha matatizo na migogoro mingi duniani leo.” Isitoshe, kulingana na sensa ya mwaka 2011 huko Uingereza na Wales, ni asilimia 59 tu ya watu waliosema kwamba ni Wakristo, tofauti na mwaka 2001 ambapo idadi yao ilikuwa asilimia 72. Wakati huohuo, idadi ya watu waliodai kutojihusisha na dini yoyote iliongezeka kutoka asilimia 15 hadi 25.

China

Kulingana na ripoti za vyombo vya habari, sheria iliyorekebishwa hivi karibuni inawataka watoto wenye umri mkubwa “wawatunze kihisia” wazazi waliozeeka zaidi ya kuwatembelea mara kwa mara. Hata hivyo, sheria hiyo “haitaji waziwazi adhabu yoyote” kwa wale watakaokosa kufanya hivyo.

Ulaya

Makundi ya wahalifu yanaghushi bidhaa kama vile vipodozi, sabuni, na hata vyakula. “Karibu kila kitu ambacho kina thamani kinaweza kuigwa,” anasema msimamizi wa kampuni inayoshughulika na usalama wa vyakula. Mtaalamu mmoja anakadiria kwamba asilimia 10 ya vyakula vinavyonunuliwa katika nchi zilizoendelea ni bandia.