Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

 JE, NI KAZI YA UBUNI?

Chembe za Neva za Nzige Zinazotambua Mwelekeo

Chembe za Neva za Nzige Zinazotambua Mwelekeo

NZIGE husafiri katika vikundi vikubwa kufikia hata “nzige milioni 80 kwa kila kilometa moja ya mraba.” Hata hivyo, hawagongani. Siri yao ni nini?

Fikiria hili: Nyuma ya macho mawili yenye lenzi nyingi ya nzige, kuna chembe kubwa ya neva inayotambua mwelekeo iitwayo lobula (LGMD). Nzige wanapokaribia kugongana, chembe hizo hutuma ujumbe kwenye mabawa na miguu, na kumfanya nzige abadili mwelekeo. Jambo hilo hutokea kwa kasi inayozidi mara tano kasi ya kupepesa jicho.

Kwa kuiga macho na chembe za neva za nzige, wanasayansi wametengeneza mfumo wa kompyuta unaowezesha roboti kutambua na kuepuka vitu vilivyo njiani bila kutumia mifumo tata ya rada na mnururisho. Watafiti wanatumia teknolojia hiyo mpya katika magari kwa kutengeneza mfumo unaotoa onyo kwa kasi na kwa usahihi ili kupunguza aksidenti. “Tunaweza kujifunza mengi sana kutokana na mdudu wa kawaida kama vile nzige,” anasema Profesa Shigang Yue wa Chuo Kikuu cha Lincoln, Uingereza.

Una maoni gani? Je, chembe za neva za nzige zinazotambua mwelekeo zilijitokeza zenyewe? Au zilibuniwa?