Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Jiji la New York limetunga sheria zinazokataza kuvuta sigara kwenye fuo, bustani, na vijia vya umma. Wanaokaidi sheria hizo watatozwa faini ya dola 50 kwa kila kosa. Maofisa wanatumaini kwamba watu “wataitii bila kulazimishwa.”—THE WALL STREET JOURNAL, MAREKANI.

“Kuavya mimba kimakusudi kwa vijusi vya watoto wa kike, hasa kwa watu ambao kifungua mimba alikuwa wa kike, kumeongezeka sana nchini India.” Katika familia ambazo tayari zilikuwa na mtoto wa kwanza wa kike, idadi ya watoto wa kike wanaozaliwa kwa kila watoto wa kiume 1,000 ilishuka kutoka 906 mwaka wa 1990 hadi 836 mwaka wa 2005.—THE LANCET, UINGEREZA.

Shirika la Afya Ulimwenguni limeorodhesha nguvu za sumaku-umeme za mawimbi ya redio, “kama zile zinazotokezwa na vifaa vya mawasiliano visivyounganishwa kwa nyaya,” kuwa miongoni mwa vitu ambavyo “huenda vinasababisha kansa kwa wanadamu.”—SHIRIKA LA KIMATAIFA LA UCHUNGUZI WA KANSA, UFARANSA.

Umoja wa Mataifa umesherehekea ushindi dhidi ya maradhi ya sotoka. Huo ndio “ugonjwa wa kwanza wa wanyama ambao umekomeshwa katika mazingira ya asili kutokana na jitihada za wanadamu . . . na ndio ugonjwa wa pili kukomeshwa kabisa, baada ya ugonjwa wa ndui unaowapata wanadamu.”—SHIRIKA LA CHAKULA NA KILIMO LA UMOJA WA MATAIFA, ITALIA.

Je, Wako Tayari kwa Ajili ya Msiba wa Ghafula?

“Mwongozo wa Kisheria kwa Ajili ya Msiba wa Ghafula Jijini New York” ndicho kichwa cha makala moja kwenye gazeti la New York Times. Gazeti hilo linaripoti kuhusu kuchapishwa kwa mwongozo wa kisheria utakaowasaidia mahakimu na wanasheria kukabiliana na masuala magumu ya kisheria ambayo yanaweza kutokea wakati wa “shambulizi lingine la kigaidi, uchafuzi mkubwa kutokana na miale ya mnururisho au kemikali, ama ugonjwa hatari wa kuambukiza unaoenea haraka.” Mwongozo huo uliochapishwa na mahakama za jiji la New York kwa muungano na shirika la mawakili la jiji hilo, ina orodha inayoweza kurejelewa upesi ya jinsi sheria zilizopo zinavyoweza kutoa mwongozo kwa mambo kama vile kuwatenga wagonjwa, kuhamisha watu wengi kutoka eneo moja kwa ghafula, kufanya msako bila idhini, kuwaua wanyama walioambukizwa ugonjwa, na kupuuza sheria kwa muda fulani.

Ndani ya Mito ya Zamani

Foronya safi zinaweza kuwa “zimeficha mambo yenye kuchukiza,” anasema Art Tucker, mwanasayansi mkuu wa tiba katika hospitali ya St. Barts, London. Gazeti The Times la London, ambalo liliripoti kuhusu uchunguzi wake linasema kwamba baada ya kutumiwa kwa miaka miwili, asilimia 33 ya uzito wa mto huwa ni “utitiri walio hai au waliokufa, mavi ya utitiri, ngozi iliyokufa na bakteria.” Mito ni mahali pazuri pa kujificha kwa vitu vinavyosababisha mizio, viini, na utitiri. Suluhisho la tatizo hilo ni nini? “Utitiri . . . hukauka na kufa wanapopigwa na miale ya jua,” linasema gazeti The Times, “ikimaanisha kwamba mbinu iliyotumiwa zamani ya kuanika matandiko nje husaidia kudhibiti utitiri.” Sabuni haiui utitiri, lakini wanaweza kufa ukiosha mito kwa maji yenye joto la zaidi ya Selsiasi 60, na wengi watatoka pamoja na maji.