Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ngome ya Terezín—Haikuweza Kuzuia Mateso

Ngome ya Terezín—Haikuweza Kuzuia Mateso

Ngome ya Terezín​—Haikuweza Kuzuia Mateso

KATIKATI ya majiji ya Dresden na Prague huko Ulaya ya kati kuna mji unaoitwa Theresienstadt (au Terezín). Mji huo una ngome kubwa sana iliyo na mitaro mikubwa. Ilijengwa ili kuzuia majeshi ya kigeni yasipenye nchini na pia ili kuwalinda wakazi wa maeneo yaliyo karibu.

Joseph wa Pili, mfalme wa Ujerumani na maliki wa Milki Takatifu ya Roma, aliagiza kwamba ngome hiyo ijengwe, naye alikuwapo wakati ardhi ilipokaguliwa na baadaye wakati jiwe la msingi lilipowekwa mwishoni mwa 1780. Ngome hiyo ilijengwa kwa heshima ya mama yake, Malkia Maria Theresa, na hivyo ikaitwa kwa jina la Kicheki Terezín, linalomaanisha “Mji wa Theresa.” * Inasemekana kwamba kila wakati kulikuwa na wafanyakazi 14,000 katika eneo la ujenzi. Sehemu kubwa ya kazi hiyo ilikamilishwa katika muda wa miaka minne.

Baada ya ujenzi kumalizika mnamo 1784, Terezín ilikuwa ndiyo ngome kubwa zaidi katika maeneo yaliyotawaliwa na familia ya kifalme ya Hapsburg. Mbinu za ujenzi zilizotumiwa zilikuwa za utaalamu wa hali ya juu ambao haukuwa umewahi kutumiwa kufikia wakati huo. Hata hivyo, hata kabla ya ujenzi kukamilika, mbinu za kijeshi zilikuwa zimebadilika sana.

Majeshi ya adui hayakuwa tena yakizingira ngome yalipovamia nchi nyingine. Yalikuwa yakizingira vijiji vilivyokuwa karibu na kuvipora. Kwa sababu hiyo, kufikia 1888, Terezín likaacha kuwa ngome ya kijeshi. Mitaro yake mipana ya nje ikageuzwa kuwa bustani maridadi zilizo na vijia na mabenchi.

Ngome na Mji

Ngome ya Terezín ilikuwa imekusudiwa iwe mji wenye ngome. Kulikuwa na makao kwa ajili ya wanajeshi, familia zao, na raia wengine.

Karibu na sehemu kuu ya ngome, kulikuwa na ngome ndogo ambayo ilitumiwa kama gereza la jeshi. Mapema katika miaka ya 1800, wapinzani wa kisiasa wa Milki ya Hapsburg walifungiwa humo. Miaka 100 hivi baadaye, wafungwa walitia ndani vijana waliohusika katika kuuawa kwa Dyuki Mkuu Francis Ferdinand huko Sarajevo mnamo 1914. Hawakupewa adhabu ya kifo kwa kuwa walikuwa chini ya umri wa miaka 20. Punde baadaye, wengi wao walikufa wakiwa gerezani. Waliteswa na wengine wao wakashikwa na kichaa. Gavrilo Princip, ambaye ndiye aliyemuua dyuki mkuu, alikufa ndani ya gereza hilo Vita vya Kwanza vya Ulimwengu vilipokuwa vikiendelea.

Ngome hiyo Ndogo ilikuwa na sifa ya kuwa gereza bovu zaidi katika milki ya Austria na Hungaria. Mara nyingi, wafungwa waliwekwa katika mashimo ya chini ya ardhi yenye baridi na yenye maji wakiwa wamefungwa minyororo mizito. Wakati wa Vita vya Pili vya Ulimwengu, ngome hiyo ilitumiwa kwa njia mbaya hata zaidi.

“Spa Terezín”—Ilikuwa Nini Hasa?

Baada ya Wanazi kuvamia na kuteka eneo ambalo sasa ni Jamhuri ya Cheki, walianza kuwapeleka Wayahudi kwenye sehemu kuu ya ngome hiyo mnamo 1941. Wanazi waligeuza mji wa Theresienstadt kuwa eneo lililotengwa kwa ajili ya Wayahudi. Walidai kwamba ilibidi kuwe na utengano huo wa kijamii ili kuepuka mizozo kati ya Wayahudi na watu ambao si Wayahudi. Ingawa watu kwa ujumla walifikiri Theresienstadt ni mji uliotengwa kwa ajili ya matibabu ya Wayahudi, Wanazi walikuwa wakipanga kisiri kuwaangamiza Wayahudi wote.

Katika sehemu ya mashariki ya Ulaya, Wanazi walikuwa wameanzisha kambi za vifo ambako Wayahudi kutoka Theresienstadt na maeneo kama hayo walisafirishwa hatua kwa hatua na kuuawa. * Ingawa tangu miaka ya katikati ya 1930 watu wengi walijua kwamba kambi hizo zilikuwepo, propaganda za Wanazi zilificha na kuonyesha kuwa maeneo hayo yalikuwa ya kurekebisha watu tabia. Hata hivyo, ripoti zilizidi kutolewa kuhusu hali katika kambi hizo. Kwa sababu hiyo, maofisa Wanazi walishinikizwa ili waeleze ni mambo gani yaliyokuwa yakitendeka katika kambi hizo. Kwa hiyo, Wanazi wakapanga njama ili kuwajibu watu wote ulimwenguni mashtaka hayo. Walifanyaje hivyo?

Katika mwaka wa 1944 na 1945, wakati wa Vita vya Pili vya Ulimwengu, wawakilishi wa Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu walialikwa wakague eneo kuu la ngome hiyo ili wajionee mambo yaliyokuwa yakitendeka. Hata hivyo, ili kuonyesha kwamba ngome hiyo ilikuwa eneo la kuwapa Wayahudi matibabu, Wanazi walifanya kazi kubwa sana ya kurembesha eneo hilo.

Majina matamu ya barabara yalichukua mahali pa nambari za majengo. Walijenga majengo ambayo walidai kuwa ni benki, shule ya chekechea, na maduka. Na katikati ya eneo hilo wakaanzisha mkahawa. Nyumba zilipakwa rangi nje, maua yakapandwa katika bustani katikati ya eneo hilo, na ukumbi fulani ukajengwa ambako muziki mtamu ulipigwa.

Baadaye, wawakilishi wa Msalaba Mwekundu walitembezwa kwenye eneo hilo. Waliruhusiwa kuzungumza na watu waliodai kuwa wawakilisha wa “serikali” ya Wayahudi. Hata hivyo, watu hao walikuwa wakazi walioteuliwa kwa uangalifu ambao walijibu maswali kama walivyokuwa wameagizwa na kuzoezwa na Wanazi. Mara mbili, Wanazi walifaulu kuwadanganya wawakilishi wa Msalaba Mwekundu walipokagua eneo hilo. Katika ripoti zao, wawakilishi hao walisema kimakosa kwamba Theresienstadt ni mji wa kawaida tu wa Wayahudi ulio na raia wanaotunzwa vizuri. Wawakilishi wa Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu walipoondoka Theresienstadt, Wayahudi walioachwa nyuma ya kuta za eneo hilo waliendelea kuteseka, kunyimwa chakula, na kufa. Ni wachache tu waliokuwa hai kufikia mwisho wa Vita vya Pili vya Ulimwengu.

Ngome Ndogo

Ngome Ndogo ilitumiwa na Wanazi kama gereza. Hali katika ngome hiyo ilikuwa mbaya sana kama tu ilivyokuwa katika kambi za mateso. Makumi ya maelfu ya wanaume na wanawake walifungwa katika Ngome hiyo Ndogo kwa muda tu, wakisubiri kupelekwa kwenye kambi nyingine kubwa katika eneo lililotawaliwa na Ujerumani.

Mashahidi wa Yehova 20 hivi kutoka Prague, Pilsen, na sehemu nyingine nchini humo walifungwa katika Ngome hiyo Ndogo. Walikuwa wamefanya kosa gani? Walikataa kuwategemeza Wanazi na hawakuunga mkono upande wowote katika siasa. Licha ya kazi ya kuhubiri kupigwa marufuku, Mashahidi waliendelea kuwaeleza watu wengine habari njema kutoka katika Biblia. Waliteseka kwa sababu tu ya imani yao, na wengine wakauawa au wakateswa hadi walipokufa.

Jambo Tunaloweza Kujifunza

Biblia inasema: “Msiweke tegemeo lenu katika watu wenye vyeo, wala katika mtu wa udongo, ambaye hana wokovu wowote. Roho yake hutoka, naye hurudi kwenye udongo wake; siku hiyo mawazo yake hupotea.” (Zaburi 146:3, 4) Ngome ya Terezín ni mfano mzuri sana wa jambo hilo.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 3 Malkia huyo alikuwa pia mama ya Marie Antoinette ambaye baadaye alikuwa malkia wa Ufaransa.

^ fu. 12 Kwa habari zaidi, ona matoleo ya Amkeni! ya Agosti 22, 1995, ukurasa wa 3-15, na Novemba 8, 1989 au Aprili 8, 1989 la Kiingereza, ukurasa wa 3-20.

[Sanduku katika ukurasa wa 20]

MASHAHIDI WA YEHOVA KATIKA NGOME NDOGO

Wengi wa Mashahidi wa Yehova waliofungwa huko Theresienstadt walihojiwa kwanza katika makao makuu ya Gestapo huko Prague. Kwa kawaida, walipotolewa Theresienstadt walipelekwa kwenye kambi za mateso huko Ujerumani. Walifauluje kukabiliana na hali ngumu gerezani na vilevile na kutengwa?

Mwanamke fulani Shahidi ambaye alifungwa huko Theresienstadt anakumbuka hivi: “Kwa sababu sikutaka kusahau mafundisho ya Biblia, niliyarudia tena na tena. Katika kila gereza nililohamishwa, nilijaribu kuona kama kuna Mashahidi wengine; na nilipopata habari kwamba wako, nilijaribu kuwasiliana nao. Wakati huohuo nilijitahidi kuwahubiria watu kadiri hali zilivyoruhusu.”

Njia yake ilifaulu. Aliendelea kuwa mwaminifu kwa Mungu muda wote aliokuwa amefungwa na hata katika miaka iliyofuata.

[Picha katika ukurasa wa 18]

Stempu inayoonyesha Terezín kana kwamba ni mahali pazuri wakati wa Vita vya Pili vya Ulimwengu

[Picha katika ukurasa wa 19]

Wafungwa wapya walielekezwa kwenye kambi. Ishara ya Kijerumani inasema: “Arbeit Macht Frei” (Kazi Hutokeza Uhuru)

[Picha katika ukurasa wa 19]

Vitanda vya mbao katika sehemu ya wanawake ya ngome

[Picha katika ukurasa wa 20]

Lango kuu la Ngome Ndogo

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 19]

Both photos: With courtesy of the Memorial Terezín