Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Teknolojia Imeenea kwa Kasi Sana

Teknolojia Imeenea kwa Kasi Sana

Teknolojia Imeenea kwa Kasi Sana

HUKO Albania, si jambo la ajabu kumwona mzee aliyepanda punda akizungumza kwenye simu yake ya mkononi. Huko India, maskini fulani anaacha kuombaomba ili apige au ajibu simu yake ya mkononi. Naam, simu za mkononi, kompyuta, na televisheni zimeenea kokote ulimwenguni kwa matajiri na maskini pia.

Kuongezeka kwa simu za mkononi kunaonyesha jinsi ambavyo teknolojia imeenea, na nyingi ya simu hizo si simu tu. Simu za hali ya juu humwezesha mtu kutumia Intaneti, kutuma na kupokea barua pepe na ujumbe mfupi, kutazama televisheni, kusikiliza muziki, kupiga picha, kumwelekeza mahali anapoenda kwa kutumia Mfumo wa Kupokea Habari Kutoka kwa Setilaiti (GPS), na—bila shaka—hata kupiga simu!

Kulingana na ripoti moja iliyotolewa katika gazeti Washington Post, simu fulani ya hali ya juu sana “sasa ina uwezo mkubwa wa kufanya mambo kuliko uwezo ambao Kituo cha Amerika Kaskazini cha Ulinzi wa Angani kilikuwa nao katika mwaka wa 1965.” Gazeti hilohilo linasema hivi pia: “Kwa kila wanadamu wawili duniani, mmoja ana simu ya mkononi,” na angalau nchi 30 zina simu nyingi kuliko watu. Kwa kweli, tunajionea “kuenea kwa kasi sana kwa teknolojia kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya wanadamu,” linasema gazeti hilo.

Ulimwenguni pote, karibu asilimia 60 ya watumiaji wa simu za mkononi wanaishi katika nchi zinazoendelea. Kwa sababu hiyo, simu za mkononi ndicho kifaa cha teknolojia kinachotumiwa zaidi na watu katika nchi hizo. Kwa mfano, nchini Afghanistan, kulikuwa na watumiaji wapya 140,000 hivi kila mwezi katika mwaka wa 2008, na katika miaka ya karibuni bara la Afrika limeshuhudia ongezeko la asilimia 50 hivi la watumiaji wa simu za mkononi kila mwaka.

Hata hivyo, maendeleo makubwa katika teknolojia ya mawasiliano yameleta matatizo. Simu za mkononi, peja, na kompyuta zinazoweza kubebwa zimefanya watu waweze kufikiwa kwa urahisi wakati wowote, mahali popote pale. Hilo limefanya watu wengine wahisi wamenaswa na teknolojia. Kwa upande ule mwingine, kuna “waraibu” wa teknolojia, ambao huhisi kwamba ni lazima wajue kila kitu kinachoendelea.

“Uraibu,” kukengeushwa, kuvurugwa—huenda hayo ndiyo matatizo makubwa zaidi yanayosababishwa na teknolojia ya mawasiliano na ya kutoa habari. * Lakini vifaa hivyo pia vina faida zake. Basi, unaweza kuvitumiaje kwa usawaziko, hekima, na kwa kuwajali wengine? Makala zinazofuata zitajibu swali hilo.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 7 Mfululizo wa makala hizi utazungumzia vifaa kama vile simu za mkononi, kompyuta, na televisheni, na pia kuhusu Intaneti. Kwa hiyo, isipokuwa iwe imeelezwa vingine, neno “teknolojia” linamaanisha vifaa hivyo.