Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Picha Maridadi “Zilizochorwa” kwa Mawe

Picha Maridadi “Zilizochorwa” kwa Mawe

Picha Maridadi “Zilizochorwa” kwa Mawe

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI ITALIA

KATI ya mbinu zote ambazo wasanii wametumia kutokeza picha za mandhari mbalimbali, mbinu ambayo mara nyingi inaitwa nakshi ya Florentine, au commesso, ni moja kati ya mbinu ngumu zaidi kutumiwa. Mbinu hiyo ya kutia nakshi ambayo hasa hutumiwa huko Florence, Italia, haitumii vipande vya mawe, vigae, au glasi zilizochongwa kwa maumbo ya kawaida kama mbinu nyingine za kutia nakshi. Badala yake, wasanii hutokeza picha kwa kutumia vipande vyembamba vya mawe vilivyochongwa kwa maumbo yasiyo ya kawaida. Vipande hivyo hukatwa kwa ustadi sana hivi kwamba huwezi kuona sehemu zilizounganishwa.

Wasanii wanaotengeneza nakshi ya Florentine hutumia aina nyingi sana za rangi. Lapis lazuli ni jiwe lenye rangi nyangavu ya bluu lenye alama nyeupe lililo na vipande vya nyengwe vya rangi ya dhahabu. Malakati ni jiwe lenye mistari ya rangi hafifu ya kijani na ile iliyokolea. Marumaru yenye mistari maridadi inapatikana katika rangi za manjano, kahawia, kijani, na nyekundu. Ageti, yaspi, shohamu, mawe mekundu, na aina nyingine ya mawe hufanyiza rangi mbalimbali ambazo wasanii hutumia kutokeza picha maridadi. Wao hutumia rangi na mistari ya mawe hayo kuonyesha mandhari zenye miamba, mimea, bahari iliyochafuka, au hata anga lenye mawingu.

Hii si mbinu mpya ya kutia nakshi. Inawezekana kwamba ilibuniwa katika Mashariki ya Karibu, kisha ikafika Roma kufikia karne ya kwanza K.W.K. na ikawa maarufu kwa kurembesha sakafu na kuta. Ingawa mbinu ya kutia nakshi ya Florentine ilitumiwa sana katika Enzi za Kati na za Bizantiamu, jiji la Watuskani la Florence lilifanya mbinu hiyo iwe maarufu kuanzia karne ya 16 na kuendelea. Hadi siku hizi, picha maridadi za nakshi ya Florentine zinapatikana katika majumba ya kifalme na ya makumbusho kotekote barani Ulaya.

“Kuchora” kwa kutumia mawe ni kazi ngumu. Gazeti moja linasema kwamba saa zinazotumiwa “hata kwa ajili ya kazi rahisi zinaweza kumshtua mtu anayechunguza wakati unaotumiwa kufanya kazi fulani.” Hivyo leo, kama ilivyokuwa zamani, watu wengi hushindwa kununua picha hizo kwa sababu wasanii wanaziuza kwa bei ghali sana.

Zinatengenezwa Jinsi Gani?

Kazi inaanza kwa kutumia mchoro. Nakala yake inakatwa katika vipande, kila kipande kikilingana na sehemu fulani ya picha. Msanii anapochagua kwa makini jiwe linalofaa kwa ajili ya kila sehemu anajaribu kutokeza mchoro huo kwa njia yake wala si tu kuuiga. Kila sehemu ya nakala hiyo inapachikwa kwa gundi kwenye kipande cha mawe kilichochaguliwa.

Kisha msanii anashika kila kipande ambacho upana wake ni milimita mbili au tatu hivi kwa kutumia kifaa fulani. Kisha akitumia msumeno wa pekee anakata kwa uangalifu vipande anavyohitaji (ona picha juu). Yeye hulainisha vipande hivyo kwa usahihi sana hivi kwamba anapoviunganisha haoni mwangaza wowote ukipita katikati ya vipande hivyo. Wazia jinsi ilivyo vigumu kufanya hivyo ikiwa vipande anavyokata ni vyembamba kama vikonyo vya mzabibu!

Baada ya vipande kukusanywa na kupachikwa kwenye bamba la mawe, vinalainishwa na kung’arishwa sana na kung’aa hivi kwamba huwezi kuona uzuri wake halisi unapotazama picha ya kawaida. Inastaajabisha sana kuona ustadi ambao wasanii hutumia kutokeza tofauti za rangi kwenye kipande kimoja cha jiwe ili kuonyesha jinsi mwangaza unavyopiga sehemu ya juu ya ua na kivuli chake kwa njia halisi. Matunda, vyombo vya kuwekea maua, vipepeo, ndege, na mandhari mbalimbali ni baadhi ya vitu ambavyo wasanii wabunifu wamechora.

Jambo moja lenye kupendeza kuhusu nakshi ya Florentine ni kwamba msanii hawezi kuamua vitu hususa atakavyotumia katika mchoro wake. Badala ya hivyo, lazima achague rangi, mawe, na vitu vingine kutokana tu na vile ambavyo Mungu ameumba. Kitabu kimoja kinasema hivi kuhusu mbinu hii: “Kupitia mawe maridadi unaweza kutafakari fahari na nguvu zisizoelezeka za Mungu ambaye anaunganisha umaridadi uliopo ulimwenguni katika mawe hayo madogo . . . , na hivyo kila wakati unajionea utukufu wenye kung’aa wa Mungu.”

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]

All photos pages 16 & 17: Su concessione del Ministero per i Beni e le Attività Culturali-Opificio delle Pietre Dure di Firenze, Archivio Fotografico