Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Puerto Riko—Nchi Yenye Utajiri

Puerto Riko—Nchi Yenye Utajiri

Puerto Riko—Nchi Yenye Utajiri

NOVEMBA 19, 1493, (19/11/1493) Christopher Columbus aliwasili kwenye bandari ya kisiwa cha Karibea akiwa katika msafara wa meli kutoka Hispania. Akiwa huko, alikiita kisiwa hicho San Juan Bautista (Mtakatifu Yohana Mbatizaji). Baada ya kukaa kwa muda mfupi na kununua bidhaa, aliendelea na safari yake ya pili ya uvumbuzi.

Mvumbuzi huyo hakupendezwa na fuo maridadi zilizojaa mitende na mimea mingine yenye kuvutia. Columbus alikuwa akitafuta visiwa vikubwa zaidi vyenye utajiri mwingi.

Ponce de León, Mhispania ambaye watu fulani wanasema aliandamana na Columbus kwenye safari hiyo, aliamua kurudi kwenye kisiwa hicho ambacho kilijulikana na wenyeji kuwa Boriquén. Kwa kuwa aliambiwa kwamba wenyeji walivalia mapambo ya dhahabu, aliamini vilima vya visiwa hivyo vilikuwa na dhahabu. Miaka 15 baadaye, alirudi ili achimbue dhahabu hiyo. Mnamo 1521 Wahispania walianzisha mji mkuu kwenye ufuo wa kaskazini wa kisiwa hicho. Kwa kuwa alitarajia atapata dhahabu nyingi, Ponce de León aliuita mji huo mpya Puerto Riko, jina linalomaanisha “Bandari Tajiri.” *

Ponce de León alikuwa amekosea. Kiasi kidogo cha dhahabu kilichokuwa Puerto Riko kilimalizika haraka, na matatizo ya kisiasa yakaongezeka. Mwishowe, Ponce de León alihamia jimbo ambalo leo linaitwa Florida, Marekani.

Ingawa kisiwa cha Puerto Riko kilikuwa na kiasi kidogo cha madini, punde si punde Wahispania walitambua kwamba bandari yake kuu ilikuwa muhimu. Katika karne ya 16, waligeuza mji mkuu wa kisiwa hicho kuwa bandari salama ya kulinda meli zilizobeba dhahabu kutoka Amerika hadi Hispania. Baada ya muda mfupi, San Juan ilijulikana kuwa “ngome imara zaidi ya Wahispania huko Amerika.”

Kuta imara zenye urefu wa mita 13 na upana wa kufikia mita 6 na ngome mbili kubwa zinatoa uthibitisho wa jitihada zisizo za kawaida zilizofanywa na watu wa San Juan ili kulinda mji wao. Bado watalii hupenda kutembelea San Juan wanapotalii maeneo ya Karibea. Wageni wanaweza kuwazia enzi za wakoloni wanapotembea kando ya kuta za mji huo na majengo ya zamani.

Kutembelea San Juan ya Zamani

Mji huo uliozingirwa na kuta unaojulikana kama San Juan ya Zamani unatofautiana na jiji la kisasa linalolizunguka. Mji wa San Juan ya Zamani unafanana na meli inayoelea. Karibu sehemu zote za mji huo zimezungukwa na bahari na rasi yake, au “omo,” imetokeza sana katika bahari ya Atlantiki. Mahali hapo panapofaa ndipo ngome ya Hispania inayoitwa El Morro iliyolinda mwingilio wa bandari ilipojengwa. Nyuma ya El Morro kuna ngome zilizo pande mbili za ufuo mwembamba wa rasi hiyo ambayo ina umbo la omo ya meli. Kilomita moja hivi upande wa mashariki kuna ngome kubwa inayoitwa San Cristóbal ambayo ililinda “tezi” lisishambuliwe kutoka nchi kavu. Kati ya ngome hizo mbili kuna mji wa San Juan ya Zamani ambao mnamo mwaka 1983 umewekwa na Shirika la UNESCO kuwa Eneo Linalostahili Kuhifadhiwa Ulimwenguni.

Mji huo wa zamani umekarabatiwa kwa uangalifu. Wenyeji wanapaka nyumba zao rangi ya chokaa, wanaweka maua maridadi barazani, na kujaza mimea ya kitropiki kwenye nyua zao. Mawe yaliyotumiwa kwenye barabara nyembamba zenye rangi ya bluu ya kijivu yalitoka kwenye migodi ya chuma huko Hispania. Uchafu kutoka katika migodi hiyo ulitengenezwa na kuwa mawe yaliyotumiwa kusawazisha meli kutoka Hispania zilizosafiri kwenda Puerto Riko.

Kwenye ngome za San Cristóbal, bado kuna mizinga ya zamani ya Hispania inayolinda bandari hiyo. Lakini badala ya meli zilizobeba dhahabu, sasa meli kubwa za watalii hutia nanga katika bandari hiyo. Hali tulivu na urafiki wa wenyeji wa kisiwa hicho hufanya mji huo upendwe na watalii. Bado magari yanaruhusu watu wavuke kwanza, hivyo mara nyingi madereva wanahitaji kusubiri huku watalii wakipiga picha.

Sehemu Nne Zinazopaswa Kuhifadhiwa

Ingawa asilimia 30 hivi ya watu wanaishi katika eneo la San Juan, Puerto Riko ina mambo mengine mengi yanayovutia. Kisiwa hicho ni kidogo, lakini hali ya hewa inatofautiana katika sehemu zake mbalimbali, na milima na mabonde yake hukifanya kiwe na unamna-unamna wa mimea na wanyama. Yafuatayo ni mambo manne tu ya pekee kati ya mifumo ya ikolojia ambayo serikali ya Puerto Riko imejitahidi kuhifadhi.

Msitu wa Taifa wa El Yunque ni hifadhi ya kulinda mojawapo ya misitu ya mvua inayobaki katika Karibea. Kuna maporomoko ya maji yanayorembesha milima yake. Aina fulani ya michungwa hufanya mimea ya kijani kibichi ya msitu huo ipendeze, huku mikangaga mikubwa ikipatikana pamoja na mimea inayotambaa na minazi. Ingawa wako karibu kutoweka, kasuku wachache wa Puerto Riko wanapatikana katika hifadhi hiyo, na coquí—chura mdogo wa mtini huko Puerto Riko—anachangia upatano wa msituni kwa kelele zake.

Ikiangaliwa kutoka mbali, milima ya El Yunque inaonekana kana kwamba imevaa ushungi wa fedha. Rangi hiyo inatokana na majani ya miti ya yagrumo, mmea ambao ulichipuka haraka baada ya uharibifu uliosababishwa na Kimbunga Hugo miaka kadhaa iliyopita. Ukuzi huo unaonekana kuwa ishara nzuri. “Msitu unaweza kukua tena baada ya kuathiriwa na misiba ya asili bila jitihada nyingi kutoka kwa wanadamu,” anaeleza mwanabiolojia wa msitu huo. “Hatari kubwa inasababishwa na wanadamu wanapokata miti.” Msitu huo una jamii 225 hivi za miti, jamii 100 za mikangaga, na jamii 50 za okidi. Kwa sababu una aina nyingi za mimea, msitu huo umefanywa kuwa Hifadhi ya Umoja wa Mataifa.

Hifadhi ya Guánica. Huenda ni asilimia 1 tu hivi ya misitu isiyo na mvua nyingi ambayo bado ipo ulimwenguni. Mojawapo ya misitu hiyo inapatikana mwendo wa saa chache tu kutoka El Yunque. Wataalamu fulani wa mimea wanasema kwamba huenda Guánica “ndio mfano bora wa msitu usio na mvua nyingi ulimwenguni.” Msitu huo ni makao ya ndege wengi wa asili wa Puerto Riko kutia ndani jamii 750 za mimea, na asilimia 7 ya mimea hiyo imo katika hatari ya kutoweka. Maua yake yasiyo ya kawaida huwavutia ndege wavumaji na vipepeo wengi. Kando ya msitu huo kuna fuo safi ambapo kasa wa rangi ya kijani kibichi na wale wenye ngozi laini mgongoni huja kutaga mayai.

Mikoko na Matumbawe. Hifadhi ya Guánica ina msitu wa mikoko kwenye eneo la pwani. “Hifadhi yetu inasaidia mikoko isitawi, kwani hakuna uchafuzi wa kemikali kutoka viwandani na mashambani,” anaeleza mlinzi mmoja wa msitu. “Mikoko hiyo inaandaa mahali pazuri pa kutaga mayai kwa samaki wanaoishi katika matumbawe.” Jambo lingine linalowavutia watalii ni ghuba zinazong’aa zinazotegemea mikoko, na baadhi ya ghuba hizo zinaweza kupatikana huko Puerto Riko.—Ona sanduku hapo chini.

Matumbawe yaliyo karibu na fuo hayajaathiriwa na uvuvi, na visiwa vidogo na matumbawe fulani chini ya bahari yamehifadhiwa kuwa mbuga za taifa. Bustani hizo zilizo chini ya bahari ni sehemu zinazofurahisha wapiga-mbizi ambao wanakutana ana kwa ana na kasa na nguva na pia samaki wengi wenye rangi mbalimbali.

Ingawa Puerto Riko haikumpendeza Columbus na iliwatamausha Wahispania matajiri waliotaka utajiri zaidi, inawapendeza wageni wa siku hizi. Kwa maoni yao, Puerto Riko imejaa utajiri wa asili.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 4 Muda mfupi baadaye, kutoelewana kati ya wachoraji wa ramani kulifanya jina la kisiwa hicho lihusianishwe na mji wake mkuu. Tangu wakati huo, kisiwa hicho chote ndicho kinaitwa Puerto Riko na si mji wake mkuu tu, San Juan.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 16]

KITUO CHA PEKEE CHA KUCHUNGUZA ANGA

Eneo moja linalostahili kutembelewa ni Kituo cha Kuchunguza Anga cha Arecibo, kilicho kilomita 80 magharibi ya San Juan. Kina darubini kubwa zaidi ulimwenguni yenye mawimbi ya redio kikiwa na kiakisi-nuru chenye umbo la sahani yenye kipenyo cha mita 305. Ukubwa wa darubini hiyo unawaruhusu wataalamu wa nyota kuchunguza vitu ambavyo haviwezi kuonwa na darubini nyingine.

[Hisani]

Courtesy Arecibo Observatory/ David Parker/Science Photo Library

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 17]

“KUOGELEA KATIKA NYOTA”

Kwenye kisiwa cha Vieques, mwendo mfupi kutoka pwani ya Puerto Riko, kuna ghuba ndogo inayoitwa Ghuba ya Bioluminescent. Ghuba hiyo inaitwa hivyo kwa sababu inasemekana kuwa na viumbe wengi zaidi ulimwenguni ambao wanaishi majini. Viumbe hao wadogo wanaoitwa dinoflagellate wanaposumbuliwa, wao humetameta na kutokeza mwangaza wa rangi ya kijani na bluu. Wanapofanya hivyo hilo hutokeza jambo la asili lisilo la kawaida kabisa.

Wageni wanapotembelea wangwa huo usiku, wao huona vitu vinavyometameta samaki wanapokimbia mbali na mashua yao. Samaki hao huonekana kama nyota za kijani zinazomweka kwenye maji meusi. Waogeleaji wanapoingia majini, kila jambo wanalofanya linaweza kuonekana gizani. Wanapoinua mikono yao kutoka majini, matone hudondoka kama nyota zinazometameta. Mgeni mmoja alisema hivi kwa mshangao: “Ni kama kuogelea katika nyota!”

[Picha katika ukurasa wa 15]

El Morro

[Picha katika ukurasa wa 15]

Mandhari ya mji wa zamani kutoka San Cristóbal

[Picha katika ukurasa wa 15]

San Juan ya Zamani

[Picha katika ukurasa wa 16]

Mkangaga katika msitu wa mvua wa El Yunque

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Pwani ya Guánica

[Hisani]

© Heeb Christian/age fotostock

[Picha katika ukurasa wa 17]

Kasuku wa Puerto Riko

[Picha katika ukurasa wa 17]

Matumbawe

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 14]

Passport Stock/age fotostock

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]

All photos: Passport Stock/age fotostock

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]

Parrots: U.S. Geological Survey/Photo by James W. Wiley; reef: © Stuart Westmorland 2005; swimmer: Steve Simonsen