Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Nyatisinga Aokolewa ili Asiangamizwe

Nyatisinga Aokolewa ili Asiangamizwe

Nyatisinga Aokolewa ili Asiangamizwe

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI POLAND

Wawindaji haramu walisisimuka. Walikuwa wamepata alama za nyayo za mnyama waliyekuwa wakimtafuta. Waliposonga mbele mwishowe walimwona mnyama huyo. Manyoya yake yalikuwa ya rangi ya kahawia na ndevu zake zilikuwa na rangi inayokaribia nyeusi. Pembe zake zilikuwa zimejipinda kuelekea upande wa ndani juu ya kichwa chake. Kwa kuwa nyama na ngozi yake inapendwa sana, wawindaji hao walijua kwamba wangepata pesa nyingi sana.

Risasi ya kwanza ilimwumiza mnyama huyo. Alijaribu kukimbilia msituni ili ajifiche lakini hakuweza. Risasi ya pili ililenga shabaha na mnyama huyo mwenye uzito wa nusu tani akaanguka na kufa. Wawindaji hao haramu hawakujua kwamba jambo walilokuwa wamefanya lingekumbukwa kwa muda mrefu. Tukio hilo lilitendeka Aprili (Mwezi wa 4) 1919, na walikuwa wamemuua nyatisinga wa mwisho aliyeishi msituni huko Ulaya. Jambo la kupendeza ni kwamba wakati huo kulikuwa na nyati wachache kwenye hifadhi za wanyama na katika mashamba ya watu binafsi.

HAPO zamani nyatisinga wa Ulaya (Bison bonasus) walikuwa wengi sana katika bara hilo. Nyati wa kiume aliyekomaa anaweza kuwa na uzito wa kilo 900 na anaweza kufikia kimo cha mita mbili kutoka kwenye kwato hadi mabegani. Wanyama hao wakubwa wameitwa maliki wa msituni.

Jambo linaloonekana wazi unapomwangalia nyatisinga ni kwamba sehemu yake ya mbele na ya nyuma hazitoshani. Mabega yake ni mapana na mazito, ana nundu kubwa, na sehemu yake ya nyuma ni ndogo. Ana ndevu na sehemu yake ya mbele imefunikwa kwa manyoya marefu huku sehemu yake ya nyuma ikiwa na manyoya mafupi.

Anakaribia Kutoweka

Inakadiriwa kwamba leo kuna maelfu kadhaa tu ya nyatisinga wa Ulaya. Ukulima na ukataji wa miti umewafanya wapoteze makao na pia wawindaji haramu waliwawinda sana. Kufikia karne ya nane, nyatisinga wa Ulaya waliopatikana huko Gaul (Ufaransa na Ubelgiji ya sasa) walikuwa wametoweka.

Katika karne ya 16, wafalme wa Poland walichukua hatua za kuwalinda wanyama hao. Mfalme wa kwanza kuchukua hatua hiyo alikuwa Sigismund Augustus wa Pili ambaye alitoa sheria kwamba kuwaua nyatisinga wa Ulaya ni uhalifu unaostahili adhabu ya kifo. Kwa nini? Dakt. Zbigniew Krasiński wa Mbuga ya Taifa ya Białowieza alisema hivi: “Kusudi lilikuwa kuwahifadhi wanyama hao ili wawindwe na wafalme na watumishi wao.” Licha ya adhabu hiyo kali, sheria hiyo haikuwalinda nyatisinga wa Ulaya na kufikia mwisho wa karne ya 18, nyatisinga walipatikana tu katika Msitu wa Białowieza huko mashariki ya Poland na huko Caucasia.

Mwishowe, katika karne ya 19 mambo yalianza kuwa mazuri. Baada ya Milki ya Urusi kuchukua Msitu wa Białowieza, Maliki Alexander wa Kwanza alitoa amri ya kuwalinda nyatisinga wa Ulaya. Baada ya muda, matokeo mazuri yalianza kuonekana. Idadi ya nyatisinga wa Ulaya iliongezeka polepole na kufikia mwaka wa 1857, karibu nyatisinga 1,900 wa ulaya walikuwa wakilindwa na serikali. Baadaye, vituo vilifunguliwa ili kuwalisha nyatisinga katika majira ya baridi kali. Pia, waliwatengenezea vidimbwi vya maji na kupanda mimea ambayo wao hula.

Kwa kusikitisha, mpango huo wa kuwahifadhi nyatisinga wa Ulaya haukudumu. Katika kipindi cha miaka 60, idadi yao ilipungua kwa asilimia 50. Vita vya Kwanza vya Ulimwengu vilikuwa pigo kubwa kwa nyatisinga wa Ulaya. Ingawa kulikuwa na sheria iliyotolewa Ujerumani ya “kuwahifadhi nyatisinga kama mali-asili,” wanyama hao waliangamizwa na majeshi ya Ujerumani yaliyokuwa yakikimbia, majeshi ya upinzani ya Urusi, na wawindaji haramu. Kama ilivyoelezwa mwanzoni mwa makala hii, nyatisinga wa Ulaya wa mwisho aliye msituni nchini Poland aliuawa mwaka wa 1919.

Idadi ya Nyatisinga Yaongezeka

Katika jitihada za kuwalinda wanyama hao, Shirika la Kimataifa la Kuwalinda Nyatisinga wa Ulaya lilianzishwa mnamo 1923. Jukumu lake la kwanza lilikuwa kuhesabu nyatisinga wa Ulaya wa asili waliokuwa kwenye hifadhi mbalimbali. * Matokeo yalionyesha kwamba bado kulikuwa na nyatisinga wa Ulaya 54 wa asili wa maeneo tambarare kwenye hifadhi fulani za wanyama ulimwenguni. Hata hivyo, si wote waliofaa kwa ajili ya kuzalisha. Baadhi yao walikuwa wazee sana, huku wengine wakiwa wagonjwa. Hatimaye, nyatisinga 12 walichaguliwa kuongezea idadi yao. Inajulikana kwamba nyatisinga wa Ulaya wa maeneo tambarare ambao sasa wanaishi walizaliwa na nyatisinga watano kati ya hao.

Mnamo 1929, nyatisinga wawili wa Ulaya wanaoishi kwenye maeneo tambarare walirudishwa msituni. Waliwekwa kwenye eneo walilokuwa wametayarishiwa kwenye Msitu wa Białowieza. Baada ya miaka kumi, idadi yao iliongezeka hadi kufikia 16.

Je, Ataokolewa Asiangamie?

Mwanzoni mwa karne ya 21, kulikuwa na nyatisinga wa Ulaya 2,900 hivi ulimwenguni pote. Nyati karibu 700 wa Ulaya walikuwa nchini Poland. Baada ya miaka mingi, nyatisinga wa Ulaya wameongezeka nchini Belarus, Kyrgyzstan, Lithuania, Ukrainia, na Urusi.

Lakini hilo halimaanishi kwamba nyatisinga wa Ulaya hawamo hatarini. Bado wanakabili hatari kutoka kwa wadudu, magonjwa, upungufu wa chakula, ukosefu wa maji, na wawindaji haramu. Pia, kasoro za chembe za urithi ni tatizo kubwa, kwa sababu hakuna wanyama wa kutosha wa kuzalisha. Kwa sababu hizo, nyatisinga wa Ulaya bado wako katika Orodha ya Mimea na Wanyama Waliomo Hatarini ulimwenguni.

Mwanadamu amejitahidi kumhifadhi mnyama huyo kufikia wakati wetu. Hata hivyo, Dakt. Krasiński aliyenukuliwa awali, anatukumbusha kwamba “kilichowapata nyatisinga wa Ulaya kinatupa mfano wa jinsi jamii inavyoweza kukabili hatari ya kutoweka baada ya muda mfupi na kisha kuokolewa kupitia jitihada nyingi.” Bado haijulikani ni jambo gani litakalompata mnyama huyo na wengine wengi. Lakini kwa sasa “maliki wa msituni” wameokolewa ili wasiangamie.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 13 Kuna jamii mbili za nyatisinga wa Ulaya—wale wa maeneo tambarare na wale wa Caucasia, au wa milimani. Nyatisinga wa mwisho wa milimani alikufa mnamo 1927. Hata hivyo, kabla ya hapo nyatisinga mwingine wa jamii hiyo alikuwa amezalisha na nyatisinga wa maeneo tambarare. Nyatisinga kadhaa waliozalishwa kwa njia hiyo na nyatisinga wa milimani bado wako.

[Picha katika ukurasa wa 10]

Nyatisinga wa Ulaya katika Mbuga ya Taifa ya Białowieza

[Hisani]

All photos: Białowieski Park Narodowy