Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Jifunze Kumhusu Mnyama Mdadisi Coati

Jifunze Kumhusu Mnyama Mdadisi Coati

Jifunze Kumhusu Mnyama Mdadisi Coati

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI BRAZILI

UNATEMBEA polepole msituni. Ghafula unaona kundi la wanyama wanaoitwa coati wakikukaribia. Unaingiwa na woga ukijiuliza ikiwa watakushambulia. Usiwe na wasiwasi! Hata ingawa wamewahi kuwauma watu, wanyama hao wadogo ambao ni wadadisi wanatazama tu mkoba wako. Nyakati zote wao hutafuta chakula. Kwa kweli, coati hula kitu chochote wanachopata, kutia ndani minyoo, mijusi, buibui, panya, matunda, na hata mayai ya ndege.

Tofauti na wanyama wengine wa jamii yake, coati wana miili na mikia mirefu na pia pua ndefu linalonyumbulika. Wakiwa na urefu wa sentimita 66—na mkia ulio na urefu karibu kama huo—wanyama hao wa kitropiki wa Amerika wanapatikana hasa kuanzia kusini-magharibi mwa Marekani mpaka kaskazini mwa Argentina.

Majike hutembea katika kikundi wakiwa 20 hivi, huku wa kiume wakitembea peke yao. Kila mwaka katika majira ya kujamiiana, dume mmoja hujiunga na kikundi cha majike. Baada ya majuma saba au nane, coati wa kike walio na mimba hujitenga na kikundi chao na kujenga juu ya miti nyumba ambamo watazalia. Kila jike atazaa watoto watatu ama wanne. Majuma sita hivi baada ya kuzaa, mama pamoja na watoto wake hujiunga tena na kikundi. Watoto wao wanafanana na mipira midogo ya manyoya.

Wanyama hao hunusa-nusa hewa na kuchimba ardhi kwa kucha zao wanapotembea msituni. Wanachukiwa na wakulima, kwa sababu wanaweza kuharibu kabisa mashamba ya mahindi na nyumba za kuku. Wanapowindwa, wanajua jinsi ya kujificha. Viumbe hao wadogo wajanja hukimbilia kwenye maficho yao mitini. Pia wana mbinu nyingine za kujificha. Wanaposikia mlio wa risasi au mtu akipiga makofi, wao huanguka ardhini na kujifanya wamekufa! Kabla wawindaji hawajawakaribia ili kuwashika, wao hutoweka!

Utakapotembelea Brazili, huenda ukakutana na kundi la coati. Ikiwa ndivyo, usiogope, hawatakudhuru. Lakini bila shaka watafurahi ukiwarushia mapochopocho!