Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

“Kiasi cha barafu ya [Aktiki] iliyoyeyuka mwaka huu [2007] kilitushtua sana kwa sababu kilipita rekodi za awali na kuzivunja kabisa.”—MARK SERREZE, KITUO CHA KITAIFA CHA KUHIFADHI HABARI ZA THELUJI NA BARAFU, MAREKANI.

Wataalamu wa mambo ya kiuchumi wa shirika la New Economics Foundation wanakadiria kwamba “ikiwa kila mtu angetumia vitu kama vile Wamarekani wanavyofanya, wangehitaji dunia 5.3 kuwategemeza . . . Wafaransa na Waingereza wangehitaji dunia 3.1, Wahispania 3.0, Wajerumani 2.5 na Wajapani 2.4.”—SHIRIKA LA HABARI LA REUTERS, UINGEREZA.

“Madhara Mengi Kuliko Faida”?

“Kutiwa damu iliyohifadhiwa kunaweza kuwa na madhara mengi kuliko faida kwa wagonjwa wengi,” inasema ripoti kutoka Kituo cha Tiba cha Chuo Kikuu cha Duke, huko Durham, North Carolina, Marekani. Uchunguzi umeonyesha kwamba wagonjwa wanaotiwa damu mishipani wana “visa vingi zaidi vya mshtuko wa moyo, matatizo ya moyo, kiharusi na hata kifo” kuliko wale ambao hawakutiwa damu mishipani. Kwa nini? “Oksidi nitriki katika chembe nyekundu za damu huanza kubadilika mara moja baada ya chembe nyekundu kutoka mwilini.” Oksidi nitriki ni muhimu ili kupanua mishipa ya damu na kuruhusu chembe nyekundu kupeleka oksijeni kwenye tishu za mwili. Ripoti hiyo inasema hivi: “Inaonekana kwamba mamilioni ya wagonjwa wanatiwa damu ambayo haiwezi kusafirisha oksijeni vizuri.”

Uraibu wa Televisheni huko Bhutan

Kwa makumi ya miaka serikali ya ufalme mdogo wa Bhutan huko Himalaya, ilikuwa imekataa televisheni zisiingizwe nchini humo. Lakini baada ya wakaaji wengi kulalamika kwamba hawangeweza kutazama mashindano ya kandanda ya Kombe la Dunia ya 1998, serikali ilikubali televisheni ziingizwe nchini humo mnamo 1999. Sasa watu wanaweza kutazama stesheni 40 na tayari wamekuwa waraibu wa sinema za Marekani na vipindi vya mfululizo vya kimapenzi vya Kihindi, inasema ripoti kutoka Bhutan. Badala ya kuketi pamoja wakiimba na kuongea kama walivyokuwa wakifanya hapo zamani, siku hizi familia hukusanyika ili kutazama televisheni. Mwanamke mmoja analalamika kwamba hana wakati wa kufanya jambo lolote kutia ndani kusali. “Hata ingawa mimi huzungusha gurudumu langu la sala,” mwanamke huyo alisema, “nyakati zote mimi hufikiria televisheni,” liliripoti The Peninsula, gazeti la kila siku la Qatar. “Lakini watu wengi wanahofia kwamba wakaaji wa Bhutan wataanza kununua vitu ambavyo hawahitaji, jambo ambalo limetukia sehemu nyingi za ulimwengu. ‘Televisheni na matangazo ya biashara yanafanya watu watamani vitu ambavyo hawawezi kununua.’”

Wafanyakazi Wanaovurugwa

Gazeti New Scientist linasema hivi: “Nyakati nyingine inaonekana kwamba kazi pekee ambazo mfanyakazi wa ofisi hufanya ni kujibu simu na ujumbe mbalimbali.” Watafiti waligundua kwamba kikundi fulani cha watu wanaofanya kazi ya mawasiliano walifanya kazi bila kuvurugwa kwa dakika tatu tu. Kwa kuwa mtu anaweza kuvurugwa kwa muda unaofikia saa mbili kila siku, wafanyakazi fulani wenye shughuli nyingi wanatumia kompyuta kutofautisha mambo ya dharura na yasiyo ya dharura. Madokezo yafuatayo yanaweza kutumiwa na kila mtu: “Uwe mnyoofu, . . . ikiwa una shughuli nyingi waambie watu kwamba huwezi kuzungumza nao,” na uwe na ujasiri “wa kufunga barua-pepe, kuzima simu, . . . mpaka umalize kazi yako.”