Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kwa Nini Umwone Daktari wa Meno?

Kwa Nini Umwone Daktari wa Meno?

Kwa Nini Umwone Daktari wa Meno?

KABLA ya utaalamu wa kisasa wa meno, ilikuwa kawaida watu kuwa na maumivu ya meno na kupoteza meno tangu ujanani. Sura za watu wengi ziliharibiwa kutokana na meno meusi, yenye mpangilio mbovu, au yaliyong’oka. Watu wengi wazee walikosa lishe bora au kufa kwa sababu hawakuwa na meno ya kutafunia. Leo, watu wengi wanaweza kukosa kupata maumivu ya meno, kudumisha meno yao, na kuyafanya yavutie. Wataalamu wa kisasa wa meno walifauluje kufanya mambo hayo matatu?

Utaalamu wa kuzuia magonjwa ya meno, unaokazia kujifunza kuhusu meno na kuchunguzwa kwa ukawaida, umesaidia sana kuepuka maumivu ya meno na kuzuia kung’olewa meno. Yesu alisema: “Wale walio na afya hawahitaji tabibu.” (Luka 5:31) Kwa hiyo, wengine wamefaidika sana kutokana elimu inayohusiana na kutunza kinywa hivi kwamba hawahitaji kutibiwa. * Hata hivyo, watu wengi hawapendi kwenda kwa daktari wa meno. Wengine wanapuuza kutibu meno kwa sababu hawajali. Na wengine wanaona gharama inayohusika kuwa kubwa sana. Nao wengine wanaogopa daktari wa meno. Kwa vyovyote vile, unapaswa kujiuliza: Daktari wa meno anaweza kunisaidiaje? Je, nitafaidika nikimwona? Ili tuthamini umuhimu wa utaalamu wa kuzuia magonjwa ya meno, tunapaswa kuelewa daktari anajaribu kuzuia nini hasa.

Jinsi Matatizo ya Meno Yanavyoanza

Madaktari wa meno wanaweza kukusaidia usipatwe na maumivu ya meno na using’olewe meno. Unaposhirikiana nao, madaktari hao wanaweza kuondoa madhara ya ukoga, ambao ni utando mwembamba wa bakteria unaonata kwenye meno. Bakteria hizo hula mabaki ya chakula. Zinabadili sukari kuwa asidi na kuvamia tabaka gumu la juu la meno (enamel), na kuifanya iwe na matundu. Matundu hayo yanapobomoka na kuwa shimo kubwa, jino huanza kuoza. Huenda usihisi chochote wakati huo, lakini jino linapooza kufikia sehemu zenye neva, unaweza kupata maumivu makali.

Bakteria zinazotokeza ukoga zina njia nyingine ya kukudhuru. Kama ukoga hausuguliwi vizuri, unaweza kuwa mgumu na kutengeneza tabaka la vijiwe (calculus) ambayo hufanya fizi zivimbe na kuachana na meno. Hilo hutokeza nafasi kati ya meno na fizi ambapo mabaki ya chakula hukwama na kuliwa na bakteria zinazoweza kuathiri fizi. Daktari wa meno anaweza kukusaidia kudhibiti hali hiyo, lakini ukipuuza tatizo hilo tishu inayozunguka meno yako inaweza kuharibika kabisa na kufanya meno yaanguke. Watu hupoteza meno zaidi kwa njia hii kuliko hata meno yanayooza.

Mate husaidia kulinda meno kwa kiasi fulani kutokana na bakteria. Iwe umekula mlo au biskuti tu, mate yanahitaji dakika 15 hadi dakika 45 kuondoa mabaki ya chakula na kupunguza kiasi cha asidi kwenye ukoga wa meno. Muda huo unategemea kiwango cha sukari na mabaki ya chakula yaliyonata kwenye meno. Inaonekana katika kipindi hiki ndipo meno yako huharibika. Hivyo, kiwango cha uharibifu unaofanywa kwenye meno yako kinategemea mara ambazo unakula na kiwango cha vitafunio vyenye sukari unavyotumia wala si kiasi cha sukari unachokula. Kwa kuwa kiwango cha mate ni kidogo unapolala, jambo baya zaidi ni kula au kunywa kitu chenye sukari na kisha ulale bila kupiga mswaki. Lakini kutafuna big-G (bazooka) isiyo na sukari baada ya milo huongeza mate na kusaidia kulinda meno yako.

Kuzuia Kuharibika kwa Meno

Madaktari wa meno wanapendekeza uchunguzwe meno mara moja au mbili kwa mwaka, ikitegemea hali ya meno yako. Katika uchunguzi daktari atakupiga picha za eksirei, na kuchunguza meno yako kwa uangalifu ikiwa yameoza. Akitumia dawa za ganzi na mashine ya kutoboa, anaweza kuziba mashimo yoyote anayopata bila kukuumiza. Kwa wale ambao ni waoga sana, madaktari wachache sasa wanatumia mionzi ya leza au jeli ya kuyeyusha uozo, ambayo inaweza kupunguza au hata kufanya usihitaji kutobolewa. Kwa watoto, madaktari hao hukazia fikira sana meno yanayoanza kuota tena kuangalia kama yana nyufa kwenye sehemu ya juu ambayo itafanya iwe vigumu kusafisha kwa kutumia mswaki. Huenda madaktari wakapendekeza kufunika nyufa hizo kwa plastiki ya aina fulani ili kufanya iwe rahisi kuosha, na hivyo kuyalinda dhidi ya kuoza.

Kwa watu wazima, madaktari wa meno huhangaikia sana kuzuia ugonjwa wa fizi. Kwa hiyo, daktari akipata vijiwe vya aina fulani, ataviondoa. Watu wengi hawasugui sehemu fulani ya meno yao kila mara wanapopiga mswaki, hivyo daktari anaweza kukuonyesha jinsi unavyoweza kuboresha mbinu zako za kupiga mswaki. Madaktari fulani huwaelekeza wagonjwa wao kwa wataalamu wa afya ya meno ili wawafundishe kufanya hivyo.

Kurekebisha Meno Yaliyoharibika

Ikiwa meno yako yameharibika, yameng’oka, au yameota vibaya, utafurahi kujua kwamba madaktari wana njia nyingi mpya za kuyarekebisha. Hata hivyo, unahitaji pesa nyingi ili kurekebisha meno, hivyo jihadhari usipite mapato yako. Lakini watu wengi huona kwamba kurekebisha meno ni jambo muhimu haidhuru gharama yake. Huenda daktari akakuwezesha kutafuna tena. Au anaweza kufanya tabasamu lako lipendeze, na hilo ni jambo muhimu sana, kwani meno yaliyoharibika yanaweza kuathiri sana maisha yako.

Ikiwa meno yako ya mbele yamevunjika au yana rangi isiyo ya kawaida, huenda daktari akapendekeza yafunikwe, labda kwa kutumia kitu fulani kinachofanana na meno. Kifuniko hicho huunganishwa na jino lililoharibika na kulifanya liwe na umbo na sura nzuri. Ikiwa jino limeharibika zaidi, daktari anaweza kupendekeza kutumia kifuniko cha aina nyingine kilicho kama “taji” ambacho kinavishwa juu ya jino. “Taji” hiyo hufunika kabisa jino na kulifanya liwe na sura mpya kabisa kwa kutumia dhahabu au kitu kingine kinachofanana na jino la kawaida.

Daktari anaweza kufanya nini kuhusu meno yaliyong’oka? Anaweza kuweka meno bandia yanayoweza kutolewa, au anaweza kuweka kitu kinachoshikilia meno bandia (bridge). Mbinu nyingine inayozidi kuwa maarufu ni kupandikiza. Daktari hufanyiza msingi kwa kutumia titani ndani ya taya mahali ambapo jino lilikuwa, na baada ya mfupa na fizi kukua, anaingiza jino bandia kwenye msingi huo. Ni sawa tu na kuwa na jino halisi.

Meno yaliyoota vibaya yanaweza kumwaibisha mtu na ni vigumu sana kuyasafisha, na hivyo ni rahisi kupata magonjwa. Ikiwa meno hayakutani vizuri unapotafuna yanaweza kutokeza maumivu na kufanya iwe vigumu kutafuna. Inafurahisha kwamba madaktari wanaweza kusuluhisha matatizo hayo kwa kutumia vyuma. Kwa sababu ya maendeleo ya kisasa, vyuma hivyo havionekani kwa urahisi na havihitaji kusogezwa-sogezwa.

Madaktari wengine wanakazia fikira kutibu harufu mbaya kinywani. Watu wengi huwa na harufu mbaya mara kwa mara, na wengine kila wakati. Kuna sababu kadhaa zinazosababisha hali hiyo. Madaktari fulani wana ujuzi wa kutambua hali hiyo inasababishwa na nini. Mara nyingi inasababishwa na bakteria, ambazo kwa kawaida zinapatikana kwenye sehemu ya nyuma ya ulimi. Kupiga mswaki au kukwangua ulimi kunaweza kusaidia, kama tu kuongeza mate kwa kutafuna big-G. Kusafisha kinywa chako ni muhimu hasa baada ya kula vitu vinavyotokana na maziwa, nyama, au samaki.

Kukabiliana na Woga

Ikiwa wewe huogopa sana kumwona daktari wa meno, daktari anaweza kukusaidia kukabiliana na woga wako. Kwa hiyo, mweleze unavyohisi. Zungumza naye kuhusu ishara unayoweza kutoa unapohisi maumivu au woga. Wagonjwa wengi wameona jambo hilo huwapa ujasiri.

Huenda unaogopa kulaumiwa au kuaibishwa na daktari kwa kukosa kutunza meno yako. Hata hivyo, kwa kuwa kufanya hivyo kunaweza kumpotezea wateja, huhitaji kuogopa. Madaktari wengi hupenda kuzungumza na mteja kwa upole.

Watu wengi huogopa kumtembelea daktari wa meno kwa sababu ya gharama inayohusika. Lakini ikiwa unaweza kuchunguzwa sasa, utaepuka matatizo na gharama kubwa zaidi wakati ujao. Katika maeneo mengi kuna huduma za matibabu ya meno yanayowafaa watu wa viwango tofauti kifedha. Hata hospitali yenye vifaa vichache zaidi itakuwa na kifaa cha eksirei na kifaa cha kutoboa meno. Madaktari wanaweza kumtibu mgonjwa bila kumsababishia maumivu mengi. Gharama ya ganzi ni ya chini sana hivi kwamba watu wengi wanaweza kuimudu, hata wale wasiokuwa na pesa nyingi.

Madaktari wa meno wamejitolea kupunguza maumivu, si kuyaongeza. Kuna maendeleo mengi sana katika matibabu ya meno tangu siku za mababu zako. Kwa sababu meno yenye afya yanachangia afya nzuri kote mwilini na yanaweza kukusaidia ufurahie maisha zaidi, ni vizuri upange kumwona daktari wa meno. Unaweza kufurahia.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 3 Makala hii inakazia kile ambacho daktari wa meno anaweza kufanya ili kusaidia mgonjwa. Ukitaka kujua kile ambacho wewe unaweza kufanya ili utunze meno yako, tafadhali ona makala “Jinsi Unavyoweza Kutunza Meno Yako,” katika gazeti la Novemba 8, 2005 (8/11/2005), la Amkeni!

[Picha katika ukurasa wa 29]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Sehemu za Jino Lenye Afya

Kifuniko

Enamel

Dentin

Sehemu yenye mishipa ya damu na neva

Mzizi

Fizi (gingiva)

Mfupa

[Picha katika ukurasa wa 29]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Kuoza kwa Jino

Matundu

Kujaza mashimo hufanya matundu yasizidi kupanuka

[Picha katika ukurasa wa 29]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Ugonjwa wa Fizi

Ukoga unapaswa kusuguliwa kwa mswaki au kuondolewa kwa uzi mwembamba

Vijiwe vinaweza kuondolewa na daktari tu

Fizi zilizoachana na meno

[Picha katika ukurasa wa 30]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Kurekebisha Meno

Kitu kinachowekwa juu ya jino

“Taji”

Kupandikiza

“Bridge” hufunika pande zote za nafasi ya jino na kushikilia jino bandia